Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewasilisha bungeni Hotuba ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2022/23 na 2023/24 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23.
Akiwasilisha hotuba hiyo leo Aprili 24, 2023, Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha taratibu zote za kupata Ithibati ya Kitabu ‘Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Chimbuko, Misingi na Maendeleo’ kwa ajili ya kutumika kama kitabu cha ziada kwa shule za sekondari nchini.
Amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu namna Muungano huu adhimu ulivyoasisiwa pamoja na faida zake ili kuulinda na kuuenzi.
Aidha, Waziri Jafo amesema kuwa Ofisi imeendelea kuhimiza umuhimu wa wizara, idara na taasisi zisizo za Muungano kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu, sera, sheria, utaalamu na wataalamu na hadi kufikia Machi, 2023 vikao 12 vya ushirikiano vimefanyika baina ya wizara.
Pia, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu masuala ya Muungano yanayosimamiwa na wizara, taasisi na idara za Muungano kwa faida ya pande zote mbili za Muungano na kuwa kati ya taasisi 33 za Muungano, 27 zina Ofisi Zanzibar na hivyo kusogeza huduma karibu na wananchi.
Dkt. Jafo amesema kutokana na hatua hiyo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na utambuzi na usajili wa wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kutoa ithibati ya mitaala kwa vyuo vikuu vya Tanzania Bara na Zanzibar iliyofanywa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni Udahili wa wanafunzi wa Shahada ya kwanza katika Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania Bara na Zanzibar kupitia TCU na mafunzo kwa vyuo na shule za sekondari kuhusu Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa pande zote za Muungano. yaliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Kwa upande wa Hifadhi ya Mazingira Dkt. Jafo amesema katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Uhifadhi wa Bonde la Ruaha Mkuu, Ofisi imeshiriki katika utatuzi wa mgogoro wa ardhi katika Bonde la Mto Ruaha katika eneo la Ihefu ambalo ni chanzo kikuu cha maji kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Utatuzi wa mgogoro huo ulihusisha Mawaziri kutoka Wizara nane za Kisekta, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumuiya za Wafugaji, Wawekezaji katika mashamba ya mpunga, wakulima wadogo wa mpunga na Wananchi wa Wilaya za Mbarali na Chunya.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais, itaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango kazi huo ili kuhifadhi mazingira ya bonde hilo na ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu.
Waziri Jafo ameomba kuidhinishiwa jumla ya Sh. 54,102,084,000 kwa mwaka wa fedha wa 2023/24