Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenan aliyeuliza kuhusu utoaji wa taarifa ya mazoezi ya upandaji wa miti, Dkt. Jafo amesema Ilani ya Uchaguzi imeelekeza kila halmashauri nchini kupanda miti milioni 1.5 hivyo, takwimu hizo zinaonesha namna Serikali inavyoendelea na utekelezaji wake.
Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis alisema Serikali imetunga na inasimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo ili kuzuia ukataji holela wa miti katika maeneo ya milimani na miinuko.
Amesema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kalenga aliyeuliza ni lini Serikali itatunga sheria kali ya kuzuia ukataji miti holela hasa kwenye maeneo yenye milima na miinuko ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Naibu Waziri Khamis ametaja Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mazingira Sura 191, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Misitu Sura 323 ambazo zina vifungu mahususi kuhusu hifadhi ya mazingira na Ulinzi wa milima, vilima na miinuko.
Amesema sanjari na kutunga sheria, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha mazingira ya nchi yanalindwa na kuhifadhiwa vizuri zikiwemo kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Hatua za Haraka Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2006 unaoweka lengo la kila wilaya kupanda miti milioni 1.5) kila mwaka na Mkakati wa Taifa wa Kupanda na Kutunza Miti wa miaka mitano (2016/17 – 2020/2021).
Ameongeza kuwa ili kuongeza jitihada za uhifadhi katika maeneo ya milima na miinuko, Ofisi ya Makamu wa Rais itashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mamlaka za Serikali za Mtaa na Sekta Binafsi katika kutoa elimu na kusimamia sheria zilizopo kwa sasa.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 Kifungu cha 58(2) kinaelekeza kuhusu hifadhi ya mazingira na Ulinzi wa milima, vilima na miinuko; na Sera ya Misitu ya mwaka 1998 imeelekeza utaratibu wa kutunza na kuhifadhi milima na miinuko. Aidha, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999; na Sheria ya Misitu Sura 323, zimeweka utaratibu wa kisheria wa kudhibiti uharibifu wa mazingira hususan ukataji miti holela katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya milima na miinuko.
Katika hatua nyingine akijibu swali la Mhe. Khamis amepiga marufuku shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji ndani ya mita 60 na miinuko na kuelekeza upandaji wa miti ya kutosha kwatika maeneo hayo.
Alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Kiswaga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira aliyeuliza mpango wa Serikali wa kutoa tamko la zuio la kufanya shughuli za kibinadamu kwenye miinuko
Itakumbukwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 Kifungu cha 58 (2) kinaelekeza kuhusu hifadhi ya mazingira na ulinzi wa milima, vilima na miinuko na Sera ya Misitu ya mwaka 1998 imeelekeza utaratibu wa kutunza na kuhifadhi milima na miinuko.
Halikadhalika, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Misitu Sura 323, zimeweka utaratibu wa kisheria wa kudhibiti uharibifu wa mazingira hususan ukataji miti holela katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya milima na miinuko.