Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha
Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalumu Dk Dorothy Gwajima amesema bado kunahitajika msukumo mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii katika mikoa ya Arusha na Manyara,ambayo bado kiwango cha unyanyasaji ni kikubwa ili kujenga jamii yenye usawa yakiwemo makundi maalumu.
Ameyasema hayo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa alipokuwa akipokea taarifa ya kamati mbalimbali za maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wanawake ulimwenguni Machi 8, mwaka huu na kusema kuwa ameridhika na maandalizi .

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuonyesha nguvu ya wanawake katika uchumi hivyo kuwafuata machozi wanawake kutokana na mifumo kandamizi zilizopo,maadhimisho hayo yakomboe fikira na hivyo kwenda pamoja ukombozi wa Jamii pasipo itikadi yeyote .
Gwajima amesema kuwa kuna watu wanatakiwa kufunguliwa kutoka kwenye changamoto ya minyororo na hatimae kuwepo na jamii iliyoyo huru.

Amesema kuwa, Mkutano wa Dunia uliofanyika Beijing Nchini China mwaka 1995 uliona kulikuwepo na kundi kubwa la masikini katika nchi zinazoendelea ambapo katika miji na Vijijini umasikini upo katika sura mbili tofauti ambapo vijijini kiwango cha umasikini ni mbaya zaidi na waathirika zaidi ni wanawake.
Gwajima ameongeza kuwa, wanawake ndio waathirika wakubwa wananyanyapaliwa wameathiriwa na shughuli za kiuchumi, hawajui biashara na shughuli zingine wamebakia tegemezi mwenza wake akifatiki basi ndio mwisho wa maisha yake .

Amefafanua kuwa, mkutano huo wa wanawake Dunia uliofanyika Beijing ilikuwa na maazimio 12 ,ikiwemo kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuzijua haki za kisheria ,kuwawezesha kupata mafunzo ya ajira na Elimu ,kuwepo uwakilishi wa wanawake. kwenye Uongozi kupitia majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi.
“Kuwawezesha wanawake kisheria na Uongozi ,Elimu kwa umma na huduma kupitia jukwaa la maendeleo ya Jamii na hapa nchini kumeshaanzishwa Baraza uwezeshaji wanawake kiuchumi.”amesema .

Amesema sasa ni wakati wa Wizara mbalimbali, taasisi, NGOS kuamka na kuungana pamoja kupaza sauti ili kukomesha ukatili katika jamii.
Amefafanua kuwa hiyo itakuwa ni kuwafuta machozi wanawake kutokana na mifumo yote kandamizi na hilo ndilo lengo la Wizara kukomesha ukatili wa kijinsia hivyo maadhimisho hayo yatumike kukomboa fikira na kwenda pamoja katika ukombozi pasipo itikadi yeyote.
