Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam Dar es Salaam
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wahitimu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii kutokubweteka na kiwango cha elimu walichokipata bali wajiendeleze zaidi kwa maslahi mapana ya Taifa, maendeleo yao na jamii zinazowazunguka.
Ameyasema hayo leo Disemba 11, 2024 wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii kampasi ya Kijitonyama na mahafali ya 7 katika Kampasi ya Kisangara iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Waziri Dkt. Gwajima amewapongeza kwa kuhitimu katika programu mbalimbali za mafunzo chuoni hapo, ambapo amesema hatua hiyo iongeze chachu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Taifa.
“Rai yangu kwenu, kutokana na ukweli kwamba nafasi za ajira katika sekta ya umma ni chache. Tumieni utaalamu mliopata ili kujitafutia ajira binafsi. Napenda kuwakumbusha kudumisha uzalendo, utii na maadili…kufanya hivyo mtaweza kuisaidia jamii na Taifa letu kwa ujumla.
“Pia niwasisitize msibweteke na kiwango cha elimu mlichokipata jiendelezeeni zaidi kwa maslahi mapana ya Taifa na kwa maendeleo yenu na jamii zinazowazunguka,” amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha amewapongeza wahadhiri, wafanyakazi waendeshaji, na wadau wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika kuwawezesha wahitimu hao kufikia hatua hiyo muhimu kitaaluma.
“Hongereni pia kwa kuanzisha mitaala mipya inayolenga kuzalisha wataalamu katika fani za kazi za Jamii, Watoto na Vijana, Masoko na Ujasiriamali, Utatuzi Mbadala wa Migogoro Mahala pa Kazi na Saikolojia. Hatua hii ni ya kujivunia na inaongeza fursa na wigo wa watanzania wengi kupata elimu ya juu.
“Ni wito wangu kwa Chuo kuendelea kuwa wabunifu ili kuendana na mahitaji ya wakati na soko. Ni imani wataalamu wanaotokana na mitaala hii mipya, watasaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii yetu katika kipindi hiki cha utandawazi.
“Nataka kuwahakikishia kwamba, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabili Chuo hususan za uboreshaji wa miundo,” amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa bodi ya Magavana Chuo cha Ustawi wa Jamii, Sophia Simba, Kaimu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt. Lulu Mahai amesema mwelekeo wa Chuo ni kuendelea kutekeleza dira yake kwa vitendo na weledi wa hali ya juu katika kutoa mafunzo, kufanya utafiti, na kutoa ushauri elekezi kulingana na mahitaji ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Kama sehemu ya utekelezaji wa dira yetu na kuandaa kizazi bora cha kuendeleza Taifa letu, Chuo kimeanzisha programu ya Elimu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambayo kwa sasa inatolewa katika ngazi ya Stashahada katika Kampasi ya Kisangara.
“Lengo letu ni kutoa mafunzo katika programu hiyo hadi ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamili. Hii itaifanya Kampasi ya Kisangara kuwa kituo cha umahiri katika mafunzo ya Elimu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto,” amesema Dk. Mahai.
Awali Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Joyce Nyoni amesema katika mahafali hayo, kuna jumla ya wahitimu wapatao 3121 ambapo asilimia 65.5 ni wanawake na asilimia 34.6 ni wanaume) ambao watatunikiwa vyeti vyao katika fani za Ustawi wa Jamii, Kazi za Jamii kwa Vijana na Watoto, Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Mahusiano Kazini na Menejimenti ya Sekta ya Umma, Menejimenti ya Rasilimali Watu na Uongozi wa Biashara katika ngazi mbalimbali.
“Chuo kinajivunia mafanikio mbalimbali kiliyoyapata katika mwaka wa fedha 2023/2024 – 2024/2025 ikiwemo kuongeza udahili wa wanafunzi hadi kufikia jumla ya wanafunzi wote 5512 kwa mwaka wa masomo 2024/2025 ikilinganishwa na 5457 katika mwaka wa masomo 2023/2024.
“Pia chuo kimeendelea kufadhili Mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watumishi wake na chuo kiko katika hatua za mwisho za tafiti tatu (3) ambazo ni Vikwazo dhidi ya ushughulikiaji wa Matukio ya Ukatili wa Kingono kwa Watoto mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Mara, Changamoto zinazowakumba Watoto walio katika Programu za Kuondoa Uraibu wa Madawa ya Kulevya Dar es Salaam pamoja na Utekelezaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii katika Sekta Isiyo Rasmi mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Manyara.