Serikali imezitaka benki ziwe tayari kupokea Hatimiliki za Kimila kwa ajili ya kuwasaidia wahusika kupata mikopo.
Wakati ikitoa wito huo, Serikali pia imezipongeza benki ambazo tayari zimezitambua Hatimiliki za Kimila na hivyo kuwawezesha wananchi kupata mikopo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2013/2014 bungeni juzi, amewahimiza wananchi kushirikiana na Halmashauri zao kuhakiki na kupima maeneo yao na kupata Hati za Hakimiliki za Kimila.
Amesema hati hizo zina umuhimu mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kuzitumia kama dhamana ya mikopo kwenye taasisi za kifedha na kuepusha migogoro ya ardhi.
“Sina budi kuzishukuru benki ambazo zimetambua kwamba Hatimiliki za Kimila zinaweza kutumika kuchukua mikopo. Hapo hapo ninahimiza benki na taasisi nyingine za fedha kutoa ushirikiano na kutambua kwamba Hatimiliki za Kimila zina nguvu ya kisheria katika kutumika kama dhamana.
“Hii itapunguza adha kwa wananchi wengi kulazimika kutafuta hatimiliki za kawaida ili kupata mikopo, jambo ambalo ni gumu zaidi maana linahitaji kwanza ardhi za vijiji kuhaulishwa na Mheshimiwa Rais kabla hatimiliki kama hizo kutolewa,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Profesa Tibaijuka amesema mwaka 2013/2014, Wizara itaendelea kutoa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji na kuhamasisha Halmashauri za Wilaya 28 zilizo kwenye maeneo ya ukanda wa SAGCOT (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania) kuanzisha mchakato wa uhakiki wa maslahi katika ardhi ya kijiji na utoaji wa Hati za Hakimilki za Kimila.
“Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Halmashauri za Wilaya, na wadau wengine, itaendelea kuratibu utayarishaji na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila 50,000 nchini.
“Hati hizo zinawezesha wananchi kiuchumi, kwa mfano, wananchi wenye hati hizo katika Halmashauri za Wilaya za Mbozi na Ileje wameweza kupata mikopo kwa kutumia hati hizo yenye jumla ya Sh bilioni 26 kutoka Benki za CRDB, Stanbic, NMB, Mwananchi na Mfuko wa Pembejeo,” amesema.