đź“ŚNIRC,Songea


Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewaasa wafugaji wa jamii ya Wasukuma wanaoishi katika kata ya Ndalila Wilayani Songea, kuhakikisha kuwa wanaishi kwa amani na wakulima wa jamii zingine wilayani humo

“Nimewaletea salamu kutoka kwa rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nawaomba sana wafugaji tuishi na wakulima kwa amani.Tusiingize ngombe shambani.Mkae kwa amani na watu waliowapokea” amesema.

Bashe amesema hayo akiwa katika kata ya Njalila Wilayani Songea wakati wa mwendelezo wa ziara yake kukagua miradi ya kilimo katika mikoa mbali mbali nchini. Pia Waziri Bashe amezungumza na wananchi kuhusu kero zao na mipango ya serikali katika kutatua kero hizo. Alielekeza viongozi wa taasisi za serikali kuchukua hatua na kufanya usanifu wa barabara na bwawa kwa ajili ya kumwagilia hekari 6000, pamoja na kujenga zahanati na kituo cha afya.

“Mkurugenzi wa Umwagiliaji usimame, injinia wa Umwagiliaji Mkoa pia yupo hapa, kwa mwaka huu tutaanza na usanifu ambapo wataalamu watakuja kwa ajili ya kujua gharama, na masuala mengine muhimu kabla ya Kuanza utekelezaji”, amesema Waziri Bashe.

Bashe ameelekeza viongozi mbali mbali wa taasisi za serikali zinazohusika na kero zilizo ibuliwa na wananchi hao kuchukua hatua.”Serikali ifanye usanifu wa bara bara kwa ushirikiano wa tarura na tume ya Umwagiliaji.Tutaanza usanifu kujua gharama, za bwawa, bara bara na ujenzi wa miundo mbinu ya shamba”, amesema Bashe.

Mheshimiwa Bashe amebainisha mpango wa wizara kununua mazao kutoka kwa wakulima, kwa lengo la kuwaepusha wakulima na hasara za kuuza mazao yao kwa bei ya chini,”Mwenyekiti wa Skimu kasema mnauza mpunga kwa elfu sitini kwa gunia, serikali itafanya jambo moja.Tutauangalia mpunga mliovuna na tutanunua gunia moja la kg 90 kwa shilingi 81,000 na serikali itaununua wote” alisema waziri Bashe.

Katika ziara hiyo,Waziri Bashe aliwahakikishia wakulima kuwa serikali inaendelea na maboresho katika utoaji wa huduma za msingi kwa wakulima, ikiwemo utoaji wa mbegu za ruzuku na mbolea.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kununua mahindi yote yaliyovunwa hadi yatakapokwisha kabisa, hata yale machafu ambayo huwa yanatupwa.

Waziri Bashe aliwataka wakulima kuleta mahindi katika vituo kabla ya mvua na kuongeza idadi ya chekecheke na mashine za kisasa za kusafisha mahindi.

Pia, alitembelea shamba la uzalishaji wa kahawa Avivi katika Kata ya Kilagano, Wilaya ya Songea, na kuwasihi wawekezaji kuchangia maendeleo ya jamii kwa kuwachimbia visima vya umwagiliaji.

Ziara ya Waziri Bashe inaendelea katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kukagua hatua zilizofikiwa katika uibuaji, ujenzi, na uendelezaji wa miradi ya kilimo.

Mkoani Ruvuma, waziri Baahe anaendelea na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kutembelea wakulima wa mpunga katika Kata ya Njalila.

Kwa upande wa wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma,Waziri Bashe alisisitiza kuwa serikali haitakubali wakulima kuibiwa na kwamba bei elekezi za vijijini zitatolewa.

“Watakaonunua mahindi kwa shilingi 300 tutashughulika nao,” alisema Bashe.

Bashe pia amelitaka shirika la WFP kuunga mkono juhudi za serikali kwa kununua mahindi kwa bei ya shilingi 700 kwa kilo moja.

Bonde la mto Njalila lipo Wilaya ya Songea, Kata ya Kilagano, Kijiji cha Kilagano na limepakana na wilaya ya Mbinga upande wa mashariki mwa bonde. Bonde hili linapatikana umbali wa kilometa 93 kutoka Manispaa ya Songea. Bonde hili linatumika kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kama kilimo cha mazao mchanganyiko (mpunga, mahindi, ndizi, miwa, mbogamboga) na ufugaji wa wanyama (ng’ombe, mbuzi, kondoo). Kilimo hufanyika zaidi wakati wa masika, lakini hupungua wakati wa kiangazi kutokana na uhaba wa maji ya umwagiliaji.

Barabara ya kwenda bonde hilo ina urefu wa km 93 kutoka Manispaa ya Songea, lakini kipande cha km 35 kina changamoto za madaraja/makalavati 5 na sehemu tatu zenye miinuko na udongo wa utelezi wakati wa masika. Barabara hii ipo chini ya TANROAD na TARURA na imeingizwa katika mpango wa maendeleo. Mradi huu unahitaji barabara za mashambani ili kuiunganisha skimu na barabara ya Njalila na Ndatila kwa ajili ya kufikisha mazao sokoni na miji jirani.

Please follow and like us:
Pin Share