Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amezindua kampeni ya Dawasa Mtaa kwa Mtaa ambayo inalenga kuondoa changamoto mbalimbali kwa wananchi ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana.

Kampeni hiyo itakayosambaa nchi nzima inalenga kuongeza uelewa na utoaji wa huduma za maji, kusikiliza changamoto na kuwafikia wateja wengi zaidi ili wawe huru kutoa maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa na Mamlaka za maji ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Agosti 26, 2024 kwenye uzinduzi wa Kampeni hiyo uliofanyika Tegeta, Waziri Aweso amesema msingi wa kampeni hiyo ni utekelezaji wa maazimio ya ziara ya siku tano aliyoifanya katika mkoa wa Dar es Salaam.

“Sote tunafahamu kuwa maji hayana mbadala, kwahiyo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji kwa kutambua wanaohangaika na huduma hii ni kina Mama, na Rais Samia Suluhu Hassan hataki kusikia hilo… tumekuja na kampeni hii kuona watu wanapata huduma kwa wakati,” amesema Waziri Aweso.

Amefafanua kuwa, kampeni hiyo itakuwa shirikishi kuanzia kwa wananchi hadi viongozi mbalimbali.

“Katika kila kazi kuna faida lakini maeneno matupu ni hasara….hivyo nitoe wito kwa Mamlaka husika, mkaifanye kampeni hii kua faida na kutatua changamoto na kuondoa maneno ambayo si ya msingi.

“Tukishirikisha tutafanikiwa na tusiposhirikisha tutakwama tu, na mnapaswa kwenda sehemu zote zenye huduma na hata maeneo yasiyokuwa na huduma mnapaswa kwenda kuwasikiliza na kuwaeleza mipango yenu,” amesema

Awali, Katibu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema watendaji wa mamlaka hizo watakuwa wanatoa elimu kwa wananchi jinsi ya kusoma mita.

“Kumekuwa na malalamiko ya watu kubambikiwa bili tunachotaka kwanza kuwaelimisha wananchi wajue kusoma bili ili iwe rahisi kujua ukweli lakini pia kupitia kampeni hiyo tutawanganishia maji,” amesema

Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo Chama cha Mapinduzi CCM, Mkoa wa Dar es Salaam Ally Bananga amesema: “Kero zipo ila malengo yetu ni kumtua Mama ndoo kichwani, kama kuna kero ni muhimu zikatatuliwa haraka na muda wote mnapaswa kuwa tayari kuwasikiliza wananchi,”.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Mkama Bwire amesema Mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa huduma ya maji na uimarishaji wa huduma bora kwa Wananchi.

Please follow and like us:
Pin Share