Na Isri Mohamed

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametengua nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chato (CHAWASSA), Mhandisi Mari Misango, kwa tuhuma za utovu wa nidhamu kazini.

Waziri Aweso ametoa uamuzi huo akiwa kwenye ziara ya siku moja wilayani Chato mkoani Geita, baada ya Mhandisi Misango kufika katika ziara hiyo akiwa amelewa hali iliyomfanya ashindwe kutimiza majukumu yake.

Aweso amesema mtumishi huyo amekuwa akilalamikiwa kwa vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyosababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake vyema pamoja na kulalamikiwa na watumishi anaowaongoza.

Waziri Aweso amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri kumuweka pembeni katika nafasi ya uongozi mtumishi huyo na ametuma salamu kwa watendaji wote wa sekta ya maji nchini kuzingatia nidhamu katika kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amemteua Mhandisi Isaack Joseph Mgeni kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji ya Chato ambapo awali alikuwa Meneja wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Mamlaka ya Maji Geita (GEUWASA).

Waziri Aweso amefanya maamuzi hayo alipotembelea Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Chato unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 38 baada ya Maelekezo ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Dkt. Emmanuel Nchimbi na kusisitiza mradi huu unahitaji uangalizi wa karibu.