Wiki chache baada ya Gazeti la JAMHURI, kutoa taarifa juu ya viongozi wa Bandari ya Dar es Salaam wanaotajwa kutumia kampuni wanayoimiliki kupata zabuni licha ya kutokuwa na sifa, Serikali imeingilia kati na kuvunja mtandao unaogawa kazi kimizengwe.
Tayari Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ameuagiza uongozi wa Bandari kuchunguza kampuni zote zinazotoa huduma mbalimbali bandarini kuboresha utendaji na kuepuka mgongano wa maslahi binafsi minongoni wa watumishi wa Bandari.
Profesa Mbarawa alitoa maagizo hayo Machi 29, mwaka huu ikiwa ni siku moja kabla ya baadhi ya Wahariri kuwa na warsha ya siku mbili katika ukumbi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Dar es Salaam.
Kabla ya warsha hiyo, Prof. Mbarawa alifanya ziara nyingine ya kushtukiza akizuru eneo la kupakulia mafuta yanayoingia nchini (KOJ) Kurasini.
Katika toleo la Machi 17, mwaka huu, Gazeti la JAMHURI liliripoti kuwapo kwa fukuto la mgogoro bandarini unaotokana na zabuni AE/016/2012/DSM/NC/01B ya kutoa huduma za kupakua na kupakia mizigo bandarini, iliyotangazwa mwaka 2013 kisha ikatolewa kwa mizengwe kwa kampuni ambayo ya Hai Sub Suppliers ambayo viongozi wa Bandari wana uhusiano nayo.
Zabuni hiyo ilitangazwa kwa nia ya kupata mrithi wa Kampuni Hai Sub Suppliers, ambayo ipo bila mkataba wa kudumu kwa muda mrefu. Mkataba ulikuwa usainiwe Machi mosi, mwaka huu baada ya kampuni hiyo na nyingine kumaliza mikataba yao.
Hata hivyo, kutokana na mvutano wa kisheria, hadi sasa zabuni haijatolewa kwa kampuni yoyote, baada ya nia ya kuipa Hai Sub Suppliers kuzimwa, hali iliyoulazimu uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kuziongezea muda wa mwezi mmoja hadi mitatu kusubiri atakapopatikana mzabuni mwingine.
Mbali ya Hai Sub Suppliers, kampuni nyingine zilizokuwa na zabuni ndogo ni Portable Enterprises na Freight Meridian.
Waziri Mbarawa alifanya ziara ya kushtukiza na baada ya ziara yake, aliagiza uongozi wa Bandari kuangalia namna ya kuepusha migogoro baina ya kampuni zinazotoa huduma bandarini.
Mbarawa ameutaka uongozi wa Bandari kutotoa zabuni yoyote kwa kampuni zinazomilikiwa na wafanyakazi wa bandari.
“Haiwezekani mfanyakazi wa bandari akawa na kampuni inatoa huduma bandarini, hapo ni lazima kutakuwa na mgongano wa kimaslahi,” anasema Waziri Mbarawa.
Kaimu Meneja wa Bandari Dar es Salaam, Hebel Mhanga alithibitishia JAMHURI kuwa kazi ya kuchunguza kampuni hizo kabla ya kutoa zabuni mpya inaendelea.
Anasema vitengo vya Bandari ndivyo vinavyochunguza. Alivitaja vitengo hivyo kuwa ni Idara ya Sheria na ya Manunuzi ambayo itakwenda na mapendezo kabla ya menejimenti kuteua kampuni inayopaswa.
JAMHURI lilipewa taarifa kuwa kitendo kinachofanywa na Bandari kutumia kampuni yao waliyotumia ujanja wa kumtanguliza mfanyakazi wa chini aonekane ndiye mwenye kampuni (bila kujali mgongano wa maslahi), ni cha hatari.
Kampuni ya Hai Sub Suppliers ilipewa kila kazi ya Bandari ya Dar es Salaam, hali inayotishia hata usalama wa Bandari. Inaaminika imehodhi asimilia 90 ya kazi zote.
Kampuni hiyo ilikuwa inapokea kati ya Sh milioni 300 na 400 kwa mwezi kutoka Bandari, malipo yake yalianza kuongezeka baada ya Bandari kumkaimisha Mhanga.
Mhanga alianza kukaimu kazi hiyo Desemba, 2013 na ilipofika Mei, 2015 inaelezwa alianza kuzinyang’anya kazi kampuni nyingine na kuzirundika kwa Kampuni ya Hai Sub Suppliers, iliyotajwa na Mahakama kuwa haina sifa ya kufanya kazi za Bandari.
Kabla ya kuvunjwa mtandao huo, Kampuni ya Hai Sub Suppliers ilihodhi kazi katika gati 7 kati ya 8 sambamba na maghala 7 kati ya 8, imepewa kazi ya usafi wa ofisi, usafi wa jumla, kushusha na kupakia malori na mabehewa.
Kampuni ya Portable Enterprise Limited imepewa kazi moja kwenye gati Na 8 na Kampuni ya Freight Meridian imepewa kazi moja tu katika ghala Na 8. Mkataba wa awali wa Hai Sub Suppliers ulikuwa wa kupakua na kupakia meli za magari.
Katika hali isiyoelezeka, kampuni hii ilipata mkataba mnono wa kufanya kazi na taasisi kubwa kama Bandari bila kuwa na sifa stahiki. Tangu mwaka 2012 ilipopewa mkataba wa kwanza, Hai Sub Suppliers kumbukumbu zinaonesha haikuwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN) badala yake ilikuwa inatumia Na 102-303-229, ambayo ni namba ya mtu binafsi anayejulikana kwa jina la Hidaya Ibrahim Amri.
Ilipofika Mei 22, 2015 ikiwa imekwishafanya kazi miaka zaidi ya mitano na Bandari, ndipo kampuni hii iliposajiliwa Brela na kisha Mei 25, 2015 ilipata TIN namba 127-110-069, kisha ikaomba ipewe zabuni kubwa zaidi na ikapigiwa chapuo na uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kuwa ndiye mshindi.
Januari 19, mwaka huu Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma (PPAA), ilitoa hukumu juu ya kesi iliyofunguliwa na kampuni za– Nagla General Services Limited, Portable Enterprises Limited na Carnival Investment Limited wakipinga upendeleo unaovunja sheria kwa kuipatia zabuni Hai Sub Suppliers bila kuwa na sifa.
Katika hukumu hiyo, Bandari ya Dar es Salaam ilitakiwa kusitisha utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Hai Sub Suppliers Limited, kwani haikuwa na uzoefu wa miaka miwili unaotakiwa kisheria. Uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam unajenga hoja kuwa Hai Sub Suppliers ni taasisi ile ile kwani ilichofanya ni kujiondoa katika kufanya biashara na Bandari kama mtu binafsi (sole proprietor) na kugeuka kampuni ilipofika mwaka 2015.
JAMHURI imezungumza na mfanyakazi wa Bandari, ambaye ni mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Hai Sub Supplier, Yusufu Ibrahim, ambaye anamiliki asilimia 50 ya kampuni na kusema: “Ni kweli nilikuwa namiliki kampuni hii, lakini nimefilisika.”
Mhanga kwa upande wake, alisema yeye hahusiki na kampuni hiyo anasingiziwa.
Kuhusu Kampuni ya Hai Sub Suppliers kufanya shughuli karibu zote za Bandari akadai imezipata kwa mujibu wa sheria na taratibu za zabuni.
Hata hivyo, Mhanga alisema naye anapata wasiwasi na hofu kuona Kampuni ya Hai Sub Suppliers ikipewa kazi karibu zote za Bandari kwani kiusalama ni hatari shughuli za Bandari kuhodhiwa na kampuni moja.