Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Desemba 5, 2023) ameshuhudia kazi ya kusomba matope kwenye mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara, ikianza kwenye barabara kuu ya kutoka Babati hadi Singida.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo, Waziri Mkuu amesema idadi ya watu waliokufa katika maafa hayo imefikia 65 ambapo watoto wawili waliokuwa wamelazwa wameaga dunia.
Ametumia fursa hiyo kuwafikishia salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba amekatisha ziara yake nje ya nchi na yuko njiani kurejea nyumbani.
“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapa pole sana na sisi Serikali tutaendelea kutekeleza maelekezo yake ya kuwahudumia na kurejesha hali ya utulivu.”
“Kazi inayofanyika sasa ni kuondoa tope lote ili tupate level ya zamani na watu waweze kuendelea na kazi zao. Tuna makamanda 1,265 wa vikosi vyetu vya ulinzi, na wako hapa katika maeneo tofauti. Wataendelea kufanya kazi ili kuhakikisha tunarejesha mji wa Katesh katika hali ya kawaida. Malengo yetu ndani ya siku mbili hadi tatu hali ya kawaida irejee,” ameongeza.
Amesema maagizo ya Mheshimiwa Rais kuhusu kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wote yanazingatiwa, watu walioko kambini wanahudumiwa na kwamba iko timu ya wataalam kutoka Serikalini ambayo inafanya tathmini ya athari za maafa na mwishoni itatoa taarifa rasmi.
Mapema, Waziri Mkuu aliwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na kutembelea wodi ya watoto, wanaume na wanawake.
Pia alikutana na timu ya madaktari bingwa kutoka Dodoma na Arusha inayoongozwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ernest Ibenzi ambaye alisema timu yake ina watu 21 wakiwemo madaktari bingwa 12 ambapo sita wanatoka Dodoma na wengine sita wanatoka Arusha. “Hawa tisa ni madaktari wasaidizi, wataalamu wa usingizi na wauguzi wa vyumba vya upasuaji,” alisema.