Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima, amewataka askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuepuka tamaa hasa vitendo vya kupokea rushwa.
Silima aliyasema hayo hivi karibuni katika sherehe za kufunga mafunzo ya awali kwa askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, zilizofanyika katika viwanja vya Jeshi, Kikosi cha Anga (Air Wing) 603 KJ jijini Dar es Salaam.
Silima, aliyekuwa mgeni rasmi wa sherehe hizo za wahitimu 100 wa mafunzo hayo, alisema kuwa “Si hoja kuajiriwa, hoja ni ama kuachishwa kazi au kushindwa kazi. Najua mna ndoto nyingi. Ili zitimie epukeni tamaa ya utajiri wa haraka haraka. Epuka kutoa na kupokea rushwa. Msitumie mafunzo mliyoyapata kwenye vitendo vya uhalifu, wizi, ujambazi, biashara ya dawa za kulevya ama kushiriki kwenye ugaidi,” alisema Silima; na kungeza: “Msipoyaepuka matendo haya maovu, mwisho wenu utakuwa ni jela.”
Silima alionya askari hao kuacha tabia za ulevi na uasherati, kwani vitendo hivyo husababisha maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), kifo na kutotimiza ndoto walizojiwekea.
Silima alisema kuwa amefarijika baada ya kusikia kuwa askari hao 100 wote wamefaulu kwenye mafunzo ya darasani na vitendo. Kwani mafunzo ya kijeshi huwa yanahitaji uvumilivu na ubunifu.
“Tuna matarajio makubwa kwenu. Sasa ni wajibu wenu kuwadhihirishia Watanzania kwa vitendo. Muwe waadilifu kama mlivyoapa kwenye kiapo chenu. Maovu mtayaepuka kwa kumcha Mungu. Mafanikio hayaletwi kwa uhalifu bali nidhamu, upendo, ushirikiano na kujituma katika mema,” alisisitiza.
Awali katika risala yao kwa mgeni rasmi, wahitimu wa mafunzo hayo walisema; “Mafunzo ya uzimajimoto na uokoaji yanakabiliwa na changamoto ambazo zinayumbisha mafunzo yao. Mafunzo yalikuwa na upungufu wa vifaa vya kujifunzia. Hata fedha za kujikimu katika mafunzo zilichelewa; hatukuzipata kwa wakati. Muda wa mafunzo nao ni mfupi. Miezi mitatu. Tunaomba muda wa mafunzo uongezwe. Itawezesha askari watakaohitimu kuiva katika masuala ya zimamoto na uokoaji.”
Naibu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Lwidino Mgumba, aliwataka wahitimu kuwa na moyo wa kujituma wa kulitumikia Taifa.
“Lengo kubwa la mafunzo ni kuondoa upungufu wa askari wa Zimamoto. Tofauti na ilivyoelezwa awali kuwa mafunzo yalijimuisha wanafunzi 100 na wote wamehitimu, ukweli ni kwamba mafunzo yalijumuisha wanafunzi 101 walioitimu ni 100. Mmoja alitoroka usiku baada ya kuona mafunzo ni magumu,” alisema Mgumba na kuongeza: “Askari hawa 100 waliohitimu wamefunzwa na kufikia viwango vyote vilivyowekwa na jeshi.”
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nayo imesema iko tayari kuendelea kuboresha huduma za zimamoto na uokoaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Mhandisi Thomas Haule, alisema, “Sisi wa viwanja vya ndege ni wadau wakubwa wa zimamoto. Hatuwezi kufanya kazi bila huduma ya zima moto. Zimamoto na uokoaji ni moja ya huduma nyeti kwetu. Tuko tayari kuboresha huduma za zimamoto na uokoaji zifike katika viwango vya kimataifa,” alisema Mhandisi Haule.
“Jeshi la Zimamoto ndilo linalohakikisha usalama wa abiria na mizigo. Hivyo ni lazima tushiriki katika kuhakikisha tuna vifaa na vitendea kazi vingine vya zimamoto,” alisema Haule.
Miaka 14 ya Mamlaka imenunua magari zaidi ya 10. Fedha za ununuzi zimetokana na mkopo na za ndani ya Mamlaka. Hadi sasa viwanja tisa vinakidhi huduma za zimamoto, alieleza Haule.
“Kwa sasa tupo kwenye mchakato wa upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege. Upanuzi na ujenzi utakwenda sambamba na uboreshwaji wa huduma za zimamoto na uokoaji,” alisema Haule.
Hii ni awamu ya pili kwa mafunzo hayo kutoa wahitimu. Awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ilifanyika mwaka jana.
ends
*****
NA DENIS PATRICK
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ameweka hadharani misaada na michango anayokusanya kwa ajili ya kuwakomboa watoto wa kike.
Profesa Tibaijuka amefanya hivyo hivi karibuni Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 14 na mahafali ya 12 kwa wanafunzi 78 wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Barbro Johansson.
Uamuzi wa Tibaijuka ambaye ni Mwenyekiti Mwanzilishi wa taasisi ya Joha Trust inayomiliki Shule hiyo ya Barbro Johansson na ile ya Kajumulo, yanakuja siku chache baada ya gazeti moja la kila wiki kuripoti habari iliyohusisha msaada alioupokea kutoka kwa James Rugemalira, ambaye anatuhumiwa kwenye ufisadi wa fedha za IPTL.
Habari hiyo ilihusisha msaada huo na akaunti ya Escrow wakati huu Watanzania wakisubiri Ripoti ya Uchunguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuainisha kama tuhuma inayomkabili mtoa msaada ni ufisadi ama la.
Profesa Tibaijuka alisema: “Msimame imara dhidi ya fitina, majungu, wivu na mizengwe iliyomo kwenye jamii. Katika kuzunguka kwangu kwenye nchi zilizoendelea, wenzetu wanaendesha mambo kwa uwazi na ndivyo tunavyofanya hapa Barbro Johansson.
“Hapa hatubabaishi wala hatutafuti hela ya kula, tunajenga mustakabali bora wa watoto wa kike Tanzania. Harakati hizi zilianza tangu wakati ule wa Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA). Kwa sasa taasisi inamiliki shule mbili. Moja ni hii iliyopo Dar es Salaam na nyingine iko mkoani Kagera. Mpango wa taasisi ni kuwa na shule kila mkoa,” alisema.
Anasema; “Hakuna ukombozi bila ya kuwezeshwa na kuungwa mkono. Katika Azimio la Musoma walitaka kutuaminisha kuwa wanawake hawawezi. Wakasema watoto wa kike wajiunge na elimu kwa alama maalum. Tukasema hapana. Tukafanya utafiti tukagundua tatizo si kwamba mwanamke ni dhaifu bali ni mazingira anakotoka mtu.
“Baada ya shule za kimishionari za wasichana kutaifishwa, wasichana walikosa shule ya kuwaanda kuwa msaada kwao na jamii inayowazunguka. Hivyo sisi tukaja na wazo la kuanzisha taasisi ya kuwawezesha watoto wa kike,” anaeleza Prof Tibaijuka.
Alisema taasisi inapokea wanafunzi kutoka familia zote — zenye uwezo na zisizo na uwezo wa kugharamia masomo. Mkuu wa shule na timu yake hawawajibiki kujua fedha za kuwalipia wasio na uwezo zinakotoka wapi, kwani wao kazi yao ni kupokea wanafunzi na kuendesha shule.
“Mwanzo tulikuwa tukiwatumia maofisa elimu. Waliwajibika kutukusanyia watoto wahitaji. Baadaye tukagundua baadhi ya wanaotuletea si wahitaji. Ni watoto wao, ndugu zao, watoto wa ndugu zao ama majirani, tukasitisha kuwatumia maofisa elimu,” alisema.
Alisema kwamba ni jukumu letu kuhakikisha kila mwanafunzi aliyepo Barbro analipia gharama zote za elimu. Tumekuwa tukipata fedha kutoka nje ya nchi. Kuanzia za ujenzi wa majengo, uendeshaji na kugharimia wanafunzi wale wasiojiweza, anaeleza.
Profesa alieleza kuwa tangu harakati za kumkomboa mtoto wa kike zianze, wametumia zaidi ya bilioni 32. Katika fedha hizo asilimia 38 zimetoka kwa wazazi na asilimia iliyobaki imetoka kwa wahisani. Tumepokea misaada kutoka kwa wahisani wa ndani na nje ya nchi.
Alitaja baadhi ya misaada iliyopokewa kuwa ni ni Sh 8.8 bilioni kutoka Serikali ya Sweden, bilioni 1.7 kutoka Joha Trust ya Sweden, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo mwaka 2000 iliipatia ardhi taasisi hiyo, yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni moja, kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Alisema Waziri Mkuu wa Bahrain alichangia Sh 313 milioni. Wafanyabiashara kama Reginald Mengi alichangia Sh 200 milioni, Fida Hussein Sh 120 milioni kila mwaka, Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliandikia dibaji kwenye mpango mkakati wao ambao wanautumia kukusanyia fedha.
Profesa Tibaijuka alisema, “Wahisani wetu wakuu ambao wanatoka nchini Sweden, walitueleza kuwa kitu ambacho hakina wenyewe hakiwezi kusimama na kuwa endelevu abadani. Hivyo tukalazimika kutafuta na kutumia wahisani wa ndani baada ya wahisani wa nje kututaka kutoendelea kuwa tegemezi kwao. Walitaka mradi huu uwe endelevu,” alisema.
“Tulipopatiwa Sh 1.6 bilioni kutoka kwa Rugemalila, gazeti hilo likaandika kichwa cha habari cha utatanishi. Suala lenyewe halikuwa siri wala si siri. Kwa sasa Tanzania hatuna sheria ya kuchangisha michango. Ile ya maadili iko wazi na tumeitekeleza kwa kuweka wazi mapato na matumizi yetu,” alisema Profesa Tibaijuka.
Taasisi hiyo inaongozwa na kujumuisha watu waadilifu na kwamba haipokei pesa mkononi na kwamba imepata cheti safi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya ukaguzi wa hesabu za mapato na matumizi.
“Siyo rahisi shule kulipa mkopo. Ndiyo maana inafika wakati tunaweka rehani mali zetu ili kutimiza malengo ya kumkomboa mwanamke kielimu. Shule hizi ni taasisi zinazoendeshwa kama huduma, si biashara,” anaeleza Profesa Tibaijuka.
Wakati huo huo, Balozi Paul Rupia kwa niaba ya Bodi ya Shule alisema: “Kwa maendeleo tuliyoyafikia tunawashukuru wazazi, walezi, uongozi na wafanyakazi wa shule. Pia shukrani za pekee kwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kutupatia eneo hili la shule, kwani nakumbuka kipindi kile kulizuka mizengwe… bila ya yeye tusingepata eneo hili.”
Mkuu wa Shule, Halima Kamote, alisema; “Wanafunzi wanafundishwa kusimamia haki zao pamoja na za wengine. Shule inaendelea kuwafikia wanafunzi wanaotoka kwenye familia zenye uhitaji. Kwa sasa asilimia 25 ya wanafunzi tulionao ni wanaotokea kwenye familia zenye uhitaji.”
Naye mgeni rasmi katika shughuli hiyo, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda, alisema, “Naomba Mungu akutie moyo wa kuendeleza harakati za kumkomboa mtoto wa kike. Utekelezaji wa harakati za Joha Trust za kumpatia mtoto wa kike elimu, ni uungaji mkono wa mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Leo umefanya kitu vizuri kuweka mambo hadharani.”
“Tanzania ina nia ya kutoa elimu bora. Ushiriki wa taasisi binafsi ikiwamo Joha Trust Fund utawezesha Tanzania kufikia malengo ya elimu. Suala la kufadhili wasichana wenye sifa za elimu kupata elimu ni jukumu letu sote. Kuwa na kipato kidogo si tiketi ya kukosa elimu iliyo bora,” alisema Mapunda.
“Elimu mnayopata si mwisho. Ni jukumu lenu kujiendeleza kielimu. Elimu mliyopata itafungua milango ya maendeleo kwenu na vizazi vyenu,” alisema Mapunda.