Dk. Shukuru Kawambwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kwa kusema kweli hajafanya lolote zuri la kumsifia tangu alipoteuliwa kuwa waziri.

Kwa hiyo, baada ya kutangaza matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika  mwaka jana, matokeo ambayo yalikuwa mabaya zaidi tangu nchi hii ilipopata Uhuru, kelele za kumtaka waziri huyo ajiuzulu zilisikia kutoka pande zote za nchi, lakini yeye anaona hana hatia. Amekataa kujiuzulu.


Kwa hiyo, mgomo baridi wa walimu utaendelea kwa sababu tunaendelea kuwa na waziri ambaye ameshindwa kushughulikia matatizo na kero za walimu. Tutaendelea kuwa na utitiri wa vitabu vya kiada vinavyonufaisha zaidi wakuu na watendaji wa wizara, badala ya kunufaisha wanafunzi.


Tutaendelea kuwa na wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi wakiwa hawajui kusoma na kuandika, kwa kuwa badala ya kuanza kujifunza masomo matatu ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kama ilivyozoeleka, masomo hayo yamefutwa na sasa wanafunzi wa darasa la kwanza wanafundishwa masomo saba, licha ya kuwa na umri mdogo kwa sababu tu idadi kubwa ya masomo inataka idadi kubwa ya vitabu vinavyonufaisha waliopo wizarani, kwa kuwapatia chochote kutoka kwa wachapaji.


Masomo ya Uraia na Historia yataendelea kupuuzwa kwa kuwekwa vipindi viwili tu kwa juma, huku somo la Kiingereza likiwa vipindi sita. Somo la Uraia  linalohusu maisha ya kila siku ya Taifa la Watanzania, litaendelea kufundishwa shule za sekondari katika lugha ya Kiingereza kama kwamba tuko Uingereza.

 

Kwa maana hiyo, masomo ya Stadi za Kazi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyokusudiwa kuwandaa vijana wanaorudi nyumbani baada ya kumaliza elimu ya msingi kujiajiri, litaendelea kuongeza vijana wasio na ajira kwa kuwa  ni masomo yenye vitabu tu vinavyonufaisha watendaji wa wizara, huku madarasani kukiwa hakuna vitabu vya kufundisha masomo hayo wala walimu walioandaliwa kufundisha masomo hayo.


Walimu wataendelea kukemewa shuleni na wakaguzi wa shule, kwa kufundisha vibaya masomo ambayo hawakuelezwa namna ya kufundisha vizuri kwa kufanyiwa semina kabla ya kukaguliwa.

 

Kwa hiyo, mtihani wa Maarifa ya Jamii unaojumuisha masomo matatu ya Uraia, Historia na Jiografia utaendelea kufanyika shule za msingi wakati wanafunzi huulizwa juu juu maswali ya masomo hayo yaliyokusudiwa kuwajengea uzalendo wanafunzi, huku somo lenyewe la Maarifa ya Jamii likiwa limefutwa siku nyingi.


Shule zitaendelea kutumia vitabu vya kiada ambavyo walimu wameona siku nyingi kwamba havifai, huku wizara ikiendelea kuwataka wachapishaji waendelee kuvichapisha kwa kuwa watendaji wa wizara wananufaika na vitabu hivyo visivyofaa kuendelea kutumika shuleni.

 

Kwa hiyo, tutaendelea kuwa na wizara yenye watendaji jeuri na wakaidi wasiotaka kusikia maoni ya wananchi na wadau wa elimu juu ya elimu kana kwamba masuala ya elimu ni ya majumbani mwao.

 

Kwa kifupi, Watanzania tutaendelea kuwa na wizara iliyooza kwa sababu waziri anang’ang’ania kuendelea kuongoza wizara iliyomshinda, na hataki kumpisha mtu mwenye uwezo.

Tusidanganyike, tatizo la elimu Tanzania si mfumo mbaya wa elimu bali ni uongozi mbaya ulioshindwa kusimamia elimu Tanzania.

 

Wamekaa kusimamia maslahi yao, tutaunda kila namna ya tume kuchunguza matatizo ya elimu, lakini tutabaki palepale kama wizara itaendelea kuongozwa na genge la sasa, lililokaa pale si kwa sababu ya kuboresha elimu Tanzania, bali kwa kuboresha maisha yao.


Kwa hiyo, tusipoteze wakati, rais alete wizarani waziri mpya, naibu waziri mpya, katibu mkuu mpya na kamishna mpya wa elimu mpya. Wasidekezwe.