pg 1Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha, ametajwa kwenye orodha ya watu wanaotuhumiwa kuihujumu Serikali kwa kuvujisha siri mbalimbali kwa raia wa kigeni.

Tayari kuna taarifa kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimepanga kumhoji juu ya ushirika wake kwa raia wa Sweden anayetajwa kuwa ni ‘jasusi’ kinara wa migogoro katika eneo la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha.

Kwa siku kadhaa sasa, vyombo hivyo vipo Loliondo, na tayari watu kadhaa wakiwamo wanasiasa, viongozi na wanachama wa asasi zisizo za Serikali (NGOs); wamekamatwa na kuhojiwa.

Pia wamo walimu wawili wa shule za sekondari za Loliondo na Digodigo zilizoko mkoani humo.

Kuhusishwa kwa Nasha kwenye sakata hili kunatokana na taarifa za kiintelejensia zilizowezesha kunaswa kwa mawasiliano yake na jasusi huyo raia wa Sweden, Susanna Nordlund.

Susanna, mwalimu wa lugha ya Kispaniola aliyeacha kazi hiyo na kuamua kukusanya fedha sehemu mbalimbali duniani kwa kigezo cha utetezi wa wafugaji wa Loliondo, anatajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya ujinjifu wa amani kati ya wananchi kwa upande mmoja dhidi ya wawekezaji na Serikali kwa upande wa pili.

Amekuwa akiitukana na kuidhalilisha Serikali ya Tanzania na viongozi wake kupitia mitandao mbalimbali ambayo baadhi anaiendesha na mingine huuza habari. Miongoni mwa mitandao anayoshirikiana nayo ni Avaaz.

Wiki iliyopita, alipopata taarifa za kukamatwa na hatimaye kuachiwa kwa walimu Supuk Maoi wa Shule ya Sekondari Loliondo; na Clinton Kairung wa Sekondari ya Digodigo; aliandika haya kuhusu Serikali: “Great, Now lets hope that those bastards haven’t achieve their objectives”;  akimaanisha ‘hawa wanaharamu (Serikali) hawakufanikisha malengo yao.’

Kwa msaada wa NGOs, Susanna aiingia nchini mwaka 2010 akijitambulisha na kupewa viza ya utalii, lakini akatiwa hatiani baada ya kubainika anaendesha mikutano ya uchochezi. Alipigwa faini ya dola 400 za Marekani. Akapewa hati ya kufukuzwa nchini (PI Na. 0039131) iliyotolewa Februari 12, 2010 Arusha.

Mwanzoni mwa mwaka huu, kwa nyakati mbili tofauti ameandika barua Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiomba aondolewe PI, huku akihadaa kuwa yeye ni mtalii. Lakini kazi zake nyingi ambazo baadhi ziko kwenye mitandao ya wazi na mingine ya siri, zinakinzana na ukweli huo.

Hati yake ya kusafiria yenye namba 12011727 aliyoipata Sweden Februari 8, 2001 ikagongwa muhuri kuonesha kuwa hatakiwi kuingia Tanzania.

Aliporejea Sweden akafungua blog ya “View from the Termite Mound”. Huko akajaza makala zinazoendelea kuichafua Tanzania, akitaka kuuaminisha ulimwengu kuwa Serikali inawaonea na kuwaua wananchi (wafugaji) wa Loliondo.

Susanna alibadili hati ya kusafiria na kurejea nchini Tanzania Septemba 2011 kupitia mpaka wa Namanga akitumia hati yenye namba 825 623 97 iliyotolewa Sweden.

Alipitia Namanga akitokea Kenya ambako NGOs nyingi za Ngorongoro, ama zinamilikiwa, au zina ushirikiano mkubwa na Wakenya. 

Hapo Namanga alipewa viza ya utalii. Aliingia kwa kutumia hati hiyo na kufikia katika hoteli ya Abba iliyoko Arusha kisha akaenda Loliondo na kuzuru vijiji vya Ololosokwan, Mondorosi, Sukenya, Soitsambu na Kirtalo.

Baada ya hapo akaandika makala nyingi za uchochezi zilizolenga kuwafanya wananchi waichukie Serikali. Alirejea nchini Juni, 2013 kwa kupitia hapo hapo Namanga na kupewa viza ya utalii. Akafikia katika hoteli ile ile ya Abba jijini Arusha kabla ya kuzuru vijiji vya Ololosokwan, Mondorosi, Sukenya na Kirtalo kwa lengo linaloelezwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa ni uchochezi.

Juni 17, mwaka jana akiwa na PI, aliingia nchini kupitia upenyo wake wa Namanga na kupatiwa viza ya utalii! Wawezeshaji wa mpango huo ni NGOs rafiki zake. Alifikia Monjis Guest House, Arusha ambako alikaa kwa siku tatu kisha akaenda Loliondo Juni 20. Loliondo alifikia Oloip Lodge iliyopo Wasso. Juni 23, alikamatwa na kurejeshwa kwao kupitia Kenya.

Hivi karibuni alifika Narok na Porsmoru ambako ni mpakani kwa Tanzania na Kenya; na akawa anafanya mawasiliano na watu wake walioko Tanzania.

 

Ushirika wake la Waziri Nasha, wenzake

Susanna, kabla na hasa baada ya kupata PI, amehakikisha anajenga mtandao wake wenye kumwezesha kupata taarifa zote zinazoihusu Serikali katika ngazi ya vijiji hadi Taifa.

Duru za usalama zinaonesha kuwa miongoni mwa wadau wake wakuu kwenye habari ni Naibu Waziri Nasha, walimu hao wawili na mwanaharakati mwingine, Samwel Nangiria.

“Samwel Nangiria anawasiliana sana na Susanna na mamluki wengi kwa mambo mazito, ndiye anayemtafutia na kumpatia mikataba na nyaraka za siri za Serikali. Amekuwa akituma taarifa hadi Avaaz ambao kwa kiasi fulani wamesaidia kuupotosha ulimwengu juu ya ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu-Makutano,” kimesema chanzo chetu.

Ushahidi kuwa Nangiria na Susanna wamekuwa wakipata fedha nyingi kutoka Avaaz na kwingineko, uko kwenye maombi aliyoyaandika kwa asasi hiyo Juni 17, mwaka huu. Kwenye hitimisho la barua yake aliandika maneno haya: “I’am writing to update you as well as requesting for financial support from willing individual members of Avaaz to support my defense. I would need around 20,000 USD to both support my defense as well as do a re-location at the moment to safer places, following serious security incidences i mentioned above.

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya kimataifa wamekuwa wakipelekwa Loliondo kwa kificho, kwa ushirika wa NGOs, na wanaharakati.

Fabruari 12, mwaka juzi, Nangiria alimwandikia mmoja wa wadau wake taarifa hii: “Hope you are doing well. There has been such developments regarding preparation for Alj Stream program. I understand you are coming as well. Am in Loliondo busy with Thursday community meeting. I thought of coming to the stream as well. Am looking for a land line here in Loliondo and make sure that i come. Once i get i will let you know. We have an Aljazeera reporter from Nairobi here on the ground. She will be here till the community meeting. She will be happy to link up with you. Her email: [email protected] and phone number + 254 715 424 946.” 

Siku hiyo hiyo, Nangiria alimwandikia mtu mwingine barua pepe akimweleza: “On the other side, Nyalndu (Waziri Nyalandu) is coming this week. Some reliable sources have informed us. In this connection, the community meeting on thursday is becoming more relevant. We are really busy organizing. We are requesting your support to the local media to cover the meeting. Good enough that we already have international reporters on the ground (Reuters and Aljazeera). 

Thanks and i will keep you posted with the development on the ground.”

“Kwa taarifa za waandishi hao wa Aljazeera na Reuters ulimwengu uliaminishwa kuwa Serikali ya Tanzania inakusudia kuwafukuza Wamasai kutoka Loliondo, Ngorongoro na kuiuza Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa Waraabu. Ikamlazimu Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, kukanusha taarifa hizo za uzushi,” kimesema chanzo chetu. 

 

Naibu Waziri Nasha

Nasha anakiri kuwa na uhusiano na Susanna, lakini anadai kwamba hawajawahi kuonana ana kwa ana.

Katika mazungumzo yake na JAMHURI, anasema: “Nawasiliana naye kwenye email  (barua pepe) lakini hata leo nikikutana naye barabarani, simfahamu maana sijawahi kukutana naye.”

Juni 11, mwaka huu kwenye mawasiliano kati ya Susanna na Mwalimu Clinton, Susanna anamtaarifu Mwalimu huyo kwamba Nasha alimweleza wasifu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba. Wakati huo Susanna alikuwa akihaha kuondolewa PI akiwa amekwama awali baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

Kabla ya kuandika barua kuomba kuondolewa PI, Susanna alihakikisha anawashirikisha wafuasi wake wakuu ili wampe hoja na mtiririko wa namna ya kuandika barua yake kwa Waziri Mwigulu ili aondolewe PI hiyo. JAMHURI lina ushahidi unaonesha kuwa miongoni mwa waliopelekewa nakala wakiombwa “kusaidia mtiririko wa barua” ni Naibu Waziri Nasha.

Uhusiano wa Nasha na Susanna unathibitishwa na taarifa kadhaa, ikiwamo ya Desemba Mosi, mwaka juzi wakati akimjibu mmoja wa wanaharakati wenzake aitwaye Ben. Katika majibu hayo, Nasha akitambua kuwa taarifa zote muhimu zimeshapelekwa kwa Susanna, akamwelekeza Ben kwa kusema: “Hi Ben, This is good. I have made a few suggestions as you can see from the attached document. I will also encourage you to use Sussana’s most recent blog article to get information on recent threats.”

Baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kumkamata Mwalimu Clinton, Susanna akawa anawasiliana na Mwalimu Sapuk kujua kama Nasha yupo Loliondo ili aweze kuhakikisha anaachiwa huru; na akajibiwa kuwa Naibu Waziri huyo tayari alikuwa eneo hilo.

Wakati fulani, baada ya Clinton kuwasiliana na Nasha juu ya taarifa za yeye (Mwalimu Clinton) kusakwa na vyombo vya ulinzi na usalama, haya ndiyo yaliyokuwa mawasiliano yao.

Baada ya Mwalimu Clinton kumweleza mpango wa kukamatwa, Nasha akamwandikia: “Nimesikia. Hawatakufanya kitu. Wewe sema hukujua kama (Susanna) ameingia nchini kinyume na sheria. Si kosa kumfahamu au kwenda naye kijijini. Kosa ni kumsaidia kutenda makosa. Wakikukamata niambie nitakuja kukusaidia.”

Mwalimu Clinton naye akajibu hivi: “Nakushukuru bro, wakija kunihoji nitawaambia sitaongea mpaka ni (niwe) na wakili. Mambo huku wazee wanakukubali ila fanya hima uje uwaone.”

Taarifa za Mwalimu Clinton kusakwa na vyombo vya dola zilimfikia Susanna, naye akawasiliana na Mwalimu Supuk kujua ukweli.

Akasema: “Supuk, says you’ve been arrested since yesterday! Is it true?…And those bastards can’t arrest for seeing me in Kenya. It would be insane.”

Yaani, ‘Supuk, anasema umekamatwa tangu jana! Je, ni kweli? …Wanaharamu hawawezi kukukamata kwa kuniona mimi nikiwa Kenya. Itakuwa uendawazimu.’

Novemba na Desemba mwaka jana, Nasha, aliwasiliana na Susanna mara kadhaa kuhusu kukamatwa kwa ng’ombe zaidi ya 7,000 waliokuwa wameingizwa kilometa 20 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).

Mawasiliano mbalimbali kati ya Susanna, Sapuk na Clinton, yanaonesha namna raia huyo wa Sweden alivyokuwa akihamasisha kutopokewa kwa viongozi na pia kutotekelezwa kwa maagizo watakayotoa. JAMHURI ina kurasa zaidi ya 1,000 zenye kuonesha mawasiliano kati ya Susanna na watu mbalimbali kuanzia mwaka 2011.

 

 Kauli ya Nasha

 JAMHURI: Kuna taarifa za wewe kuhusishwa na Susanna, raia wa Sweden. Je, unamfahamu?

NASHA: Namfahamu, hatujawahi kuonana. Lakini namfahamu kwa maana tumekuwa tunawasiliana kwenye mtandao… lakini vilevile ni mtu anayefahamika sana na watu wengi Ngorongoro …vilevile watu wa Civil Society wanamfahamu. Lakini kuhusu hatujawahi kuonana, tukikutana barabarani sitamtambua. Nimeona picha yake nafikiri mara moja sijui wapi.

JAMHURI: Umekuwa ukiwasiliana naye ukimpa maelezo anayohitaji?

NASHA: Iko hivi; yule dada ni mtu wa aina gani. Ni mtu ambaye anatafuta taarifa kuhusu Loliondo kwa hiyo source yake ya taarifa ni watu ambao wanakuwa naye kwa ukaribu. Kwa hiyo kila wakati anakuandikia ‘kuna taarifa…kuna taarifa’, hata ukijitahidi kutotaka kumpa atakusumbua mpaka utajikuta unampa kwa sababu mara nyingi unajua ana blog, unafahamu. Anaandika kwenye blog yake taarifa kutoka kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na miye. Kwa hiyo kama unayo, unampa. Kama huna unamwambia huna.

JAMHURI: Sasa upo serikalini, unajua huyu mtu alipewa amri ya kuondoka nchini (PI) mara mbili, lakini bado unawasiliana naye. Katika hali hii huoni unawekwa kwenye mazingira ya kuihujumu Serikali yako?

NASHA: (Kicheko). Hilo swali unataka niibebe stori yako. Iko hivi, huyo dada nina hakika amewasiliana na watu wengi sana hata baada ya kupata hiyo PI. Anawasiliana na DC (Mkuu wa Wilaya), anawasiliana na mtu yeyote. Mimi nafikiri hata kama mtu kapigwa PI haimaanishi kwamba hawezi sasa kupata habari kutoka kwa mtu yeyote ilimradi nature yenyewe ya habari siyo nature ambayo ina uhalifu ndani yake kama mimi ninavyoelewa. 

Kwa hiyo kama mfano mimi unaniuliza habari ya Loliondo labda imetokea fujo, nikakueleza hazijatokea fujo hali imekuwa nzuri, sijui ina mahusiano gani na mtu kupigwa PI. Kupigwa PI maana yake huruhusiwi kuingia nchini, haimaanishi kwamba hutakiwi kuwasiliana na raia wa Tanzania au kiongozi wa Serikali. Nadhani kinacho-mater zaidi ni content (maudhui), kile ninachowasiliana naye.

JAMHURI: Barua yake ya kuomba kuondolewa PI alikushirikisha. Akidai anakuja kama mtalii, unadhani kweli anachofanya ni mambo ya utalii au ni nje ya utalii?

NASHA: Kwanza, unaposema amemwandikia Kitwanga (Charles Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) na Mwigulu (Mwingulu Nchemba ambaye ni Waziri wa sasa wa Mambo ya Ndani ya Nchi) na kuni-copy, anaandika ni list saved; yeye anakuwa na watu wengi ambao anawasiliana nao, kwa hiyo siyo communication (mawasiliano) ya mimi na yeye; na ndio maana kama hawa watu ambao labda amekuonyesha hakuna sehemu yoyote ambayo mimi nimeongea naye kuhusu hilo ombi lake (la kuondolewa PI).

Kuhusu hiyo anaomba PI yake iwe revoked (kubatilisha) mimi sijazungumza naye kuhusu hiyo. Sijamshauri kuhusu hilo. Na nikueleze kuhusu haya mambo yake hasa ya PI na nini, ukifuatilia mazungumzo mimi na yeye tunaongea sana mambo ambayo mimi nina interest nayo; lakini kuhusu hiyo PI hajaniandikia mimi binafsi-ame copy kwenye group la watu wengi. 

JAMHURI: Susanna akizungumza na Sapuk, kuna mahali amekunukuu kuwa wewe umempa wasifu wa Mwigulu Nchemba.

NASHA: Ameandika wapi hiyo?

JAMHURI: Kwenye mtandao.

NASHA: Hiyo sikumbuki, lakini kwamba mimi nimpe wasifu wa Mwigulu, kwamba ni mtu wa aina gani, sikumbuki kama tumefanya mjadala kama huo. Hiyo kama ameandika yeye sikumbuki. Najaribu kukupa ukweli wangu wote. Sina cha kuficha, lakini hiyo sidhani kama nimefanya mazungumzo naye. Uzuri ni kwamba hawa Polisi wanayo yote ambayo niliwasiliana na Susanna, na mimi mara nyingi niko kwenye facebook, kwenye messenger…wanayo zote.

JAMHURI: Mwalimu Sapuk na Mwalimu Clinton unajua walikamatwa kwa tuhuma zipi?

NASHA: Mimi ninachofahamu ni kwamba kwa sababu ambayo mimi…wakati Clinton anakamatwa kwanza nilikuwa Ngorongoro nimeenda imenikuta nikiwa Loliondo. Ndugu zake Clinton waliniomba tusaidie kumuombea dhamana kwa sababu ni Mwalimu hataweza kukimbia. Lakini inachosemekana kwa sababu sijamwuliza au sijapata mtu wa kumwuliza sawasawa inasemekana kuwa wamekatwa kwa sababu wanawasiliana na Susanna ambaye anachafua Serikali. Sikupata mtu aliyenieleza kwa undani.

JAMHURI: Kwa mtazamo wako, Susanna si mtu tishio hasa ukizingatia yale anayokuwa anakuuliza?

NASHA: Mimi ninavyomwelewa, namwelewa kama ni blogger, namwelewa kama mtu anayefanya utafiti, namwelewa kwamba ni activist (mwanaharakati), mtu ambaye ana uchungu fulani na wawekezaji Loliondo.

JAMHURI: Kuna sehemu ametumia maneno makali kama bastards (wanaharamu) akiwalenga viongozi wa Tanzania.

NASHA: Wewe ni mwandishi wa habari mzuri, una uelewa mkubwa kuhusu mambo. Yeye ni haiba yake, ukiuliza watu kuhusu chat zangu, mara nyingine ananiongelesha maneno mabaya. Ukiniuliza ni mtu wa aina gani nitakueleza kwamba ni mtu ambaye kama anaumia sana hadi kumfanya karibia anachanganyikiwa! 

Anaongea maneno mabaya hata kwenye facebook na mimi mara nyingine namwambia sikiliza haimaanishi kama mtu hakubaliani na hoja yako lazima umtukane. Kwa hiyo kuhusu kwamba ameongea lugha mbaya, ni kweli. Na wapo watu wa aina hiyo duniani, ni wengi. Nafikiri umeshakutana na watu wanakuwa na hasira zao. Kuhusu kama ni threat (tishio) kwa usalama wa Loliondo nafikiri baadaye ningependa wewe kukuuliza kwa sababu nimefuatilia makala zako kwa muda mrefu unafikiri ideal situation (hali mwafaka), nini kitaondoa mgogoro wa Loliondo.

Ukiniuliza kwamba yeye kama ni threat (tishio) kwa utulivu wa Loliondo, mimi sidhani kwa sababu mimi nafikiri utulivu wa Loliondo upo mikononi mwetu sisi kama nchi ni namna gani tunaweza tuka-encourage (kuhamasisha) kuwe na maelewano. Kama umekuwa na interest (maslahi) ya kunifuatilia nimekuwa nikifanya nini mimi najaribu kuijenga hiyo harmony (makubaliano) hata kama ilivyotokea juzi imesikitisha kwa sababu nafikiri kidogo tulikuwa tuanze kupata amani Loliondo.

Naamini wawekezaji bado wanaweza wakabaki pale, inawezekana wananchi wakaendelea kubaki na ardhi yao, cha maana ni kwamba namna gani wanaweza wenyewe kutumia ardhi kwa pamoja kwa sababu nature ya matumizi ya ardhi kwamba ardhi ni ya wanavijiji, lakini pia imetolewa kwa Game Controlled Area (Pori Tengefu). Game Controlled Area karibu 42 zilizoko kote nchini ziko katika ardhi ya vijiji. Kwa sababu unahitaji kuwinda kwa amani, ni vizuri muongee vizuri na wanavijiji ili muangalie ni kwa namna gani mnaweza kutumia hiyo ardhi kwa pamoja. Kwa hiyo nafikiri sisi wenyewe tukiweza kuelewana, hata huyo Susanna na wengine-wapo Wazungu wengi wanalia kuhusu Loliondo, tena wengine wanaandika vibaya zaidi. Unajua mgogoro ulianza tangu mwaka 1992 kuna vitu vimeandikwa vibaya, watu wameshutumiwa, vitu vimeandikwa vingi. Sisi kama hatumpi nafasi ya kupata cha kuandika kwa sababu tumeshatulia, mimi nafikiri amani ya Loliondo itapatikana tu na mimi naamini katika hiki kipindi cha miaka mitano itapatikana tu.

 

 Vinara wa NGOs Ngorongoro

Bodi ya Shirika la UCRT – Ujamaa Community Resource Team:

 (1) Alais ole-Morindat ni Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Bodi ya UCRT. Ni Mwenyekiti wa zamani wa Shirika la Tanzania Natural Resource Forum (TNRF) (2) Maanda Sinyati Ngoitiko ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Pastoral Women’s Council na ni Mfanyakazi wa PWC pia, ni Mjumbe wa Bodi ya Tanzania Natural Resource Forum (TNRF), ni Diwani wa Viti Maalum (Chadema) Wilaya ya Ngorongoro.

(3) Kiaro Orminis ole Kubany – ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Arash.

(4) Edward Thomas Porokwa – ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa PINGOS FORUM Ngazi ya Mikoa (Arusha na Manyara) – Pastoralist Indigenous NGO’s Forum

(5) Carol Sorenson – Mtaalamu Mshauri wa Tanzania Natural Resource Forum (TNRF). Huyu ni raia wa kigeni.

(6) Daudi Dean Peterson – Mkurugenzi Mtendaji wa Dorobo Tours Limited, ni raia wa kigeni kutoka Marekani. Ndorobo Tours Limited na Ndorobo Fund ni yao. Ni Waanzilishi wa Mashirika ya UCRT & PWC kwa ajili ya kulinda maslahi yao katika wilaya za Ngorongoro, Kiteto, Simanjiro, Monduli, Longido, maeneo ya Tanga na Morogoro.

 

Wafanyakazi wa Shirika la Ujamaa Community Resource Team:

(1) Edward Loure – ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ujamaa Community Resource Team.

(2) Sinandei Makko ni Afisa Mipango wa Shirika UCRT Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo.

(3) Paine Eulalia Makko – anashughulikia masuala ya jinsia.

(4) Elikarimu Gayewi – Afisa Mipango Wilaya ya Hanang.

 (5) Edward Lekaita – ni Mwanasheria Mshauri kwa wilaya za Kiteto na Simanjiro.

 (6) Jamboi Baramayegu – ni Afisa Mipango Wilaya ya Longido.

 (7) Partala Dismas Meitaya – ni Afisa Mipango kwa Wawindaji na Waokota Matunda Wilaya ya Hanang.

(8) Richard Humay Baallow – Afisa Maendeleo Vijijini kwa Wawindaji na Waokota Matunda Hanang.

 Wafanyakazi wa Shirika la Pastoral Women’s Council (PWC):

 (1) Maanda Sinyati Ngoitiko – ni Afisa Utawa wa PWC.

 (1) Mary Morindat – Diwani Viti Maalumu Wilaya ya Monduli

(2) Noorparakwo Makko – Mwenyekiti na Mjumbe wa Kikundi cha Maendeleo ya Akina Mama.

(3) Taleng’o Leshoko – Mwenyekiti na Mjumbe wa Kikundi cha Maendeleo ya Akina Mama.

(4) Sion Keriene – Diwani Viti Maalumu Ketumbeine, Wilaya ya Longido.

(5) Noongipa Alais – Mwenyekiti na Mjumbe wa Kikundi cha Akina Mama Sakala, Tarafa ya Loliondo.

(6) Edward Thomas Porokwa – Mkurugenzi Msaidizi wa UCRT & Mkurugenzi Mkuu wa PINGOS FORUM.

(7) Fatuma Ngorisa – Mwenyekiti na Mjumbe wa Kikundi cha Akina Mama Malambo, Tarafa ya Sale, Mke wa Elias Ngorisa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

(8) Martine Kanjwel – Diwani Kata ya Soit-Sambu, kutoka Kijiji cha Kirtallo na Mkazi wa Kijiji cha Mundorosi.

(9) Dismas Meitaya – Afisa Mipango wa Shirika la UCRT.

Ukweli kuhusu Ngorongoro

Historia

Wilaya ya Ngorongoro ni moja kati ya wilaya tano zinazounda Mkoa wa Arusha. Kaskazini inapakana na Kenya, Mashariki kuna wilaya za Monduli na Longido, Kusini ipo Wilaya ya Karatu na Magharibi inapakana na Mkoa wa Mara.  Wilaya imegawanywa katika maeneo matatu ya kiutawala; Kusini mwa Ngorongoro kuna Mamlaka ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority) yenye matumizi mseto ya ardhi; Kaskazini kuna Loliondo inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti; Tarafa ya Loliondo inajumuisha Pori Tengefu (Loliondo Game Controlled Area –LGCA). Eneo hili limetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, wafugaji wa asili, kilimo na utalii wa kiikoloji.

LGCA ni eneo lenye vitega uchumi vingi. Baadhi ya vitega uchumi katika eneo hili ni:-

*Otterlo Business Corporation Ltd (OBC). Hawa wana leseni ya kuwawezesha kufanya shughuli za uwindaji wa kitalii katika LGCA kama zilivyo kampuni nyingine 60 katika maeneo mbalimbali nchini.

*End Beyond: Hawa wameweka kambi ya kudumu na kiwanja cha ndege ambacho baadaye Serikali ilikifunga Shughuli zao zinaweza kuonakena katika tovuti yao ya www.kleinscamp.com

*Thomson Safaris: Hawa wanaendesha shughuli zao za utalii wa asili katika maeneo ya Sukenya, Soitsambu. www.thomsonsafaris.com 

*Dorobo Tours and Safaris: Hawa wanaendesha utalii wa kiikolojia. [http://www.tanzanianorphans.org/dorobo.html] na [http://www.marilynmason.com/dorobo.html]

*Sokwe Asilia: Hawa wana kambi za kudumu na za muda. www.asiliaafrica.com 

*Nomad Safaris: Kampuni hii inamiliki kambi. www.nomad-tanzania.com

Haishangazi kuona kuwa hitimisho la yote haya ni mambo makuu matatu. Mosi, masilahi kutokana na utalii. Pili, vita ya kiuchumi, na tatu, huwezi kushindwa kubaini kuwa washindani wengi katika vita hii wanasukumwa na ukwasi uliopo Loliondo-wanalitaka eneo hilo. 

Hoja hizi ndizo zinazosababisha uwepo wa nguvu za kisiasa zinazopenyezwa kupitia ushindani wa kibishara. Kila kundi linajitahidi kujiwekea mazingira ya kuhakikisha linafaidi mazao ya utalii katika Loliondo. 

Utafiti unaonesha kuwa Loliondo ni eneo pekee lenye vivutio vya aina ya kipekee katika mazingira ya asili ambavyo vinavutia watu wengi. Hali hiyo imewafanya washindani wengi, hasa wafanyabiashara watumie mbinu mbalimbali kuhakikisha wanafaidi rasilimali katika eneo hilo. 

Wanaojiita waharakati, kwa kelele zao nyingi za kutunga, na kwa kujali masilahi yao, wameifanya Serikali ya Tanzania iingilie kati suala la Loliondo na kutoa matamko mbalimbali.

Hata hivyo, baada ya matamko hayo, NGOs na wadau wao wamejipanga kuendeleza mapambano. Kwa mfano, kabla ya msimamo wa Serikali hapakuwapo kundi lililojitambulisha kama (Avaaz) ambalo limeshiriki katika kuukuza mgogoro huu hata ukaweza kuvuma duniani. Kana kwamba jambo limefikia machweo, kundi hilo likajitokeza na kujitangaza kama la wanaharakati wa haki za binadamu. Vyovyote iwavyo, matamko yake yanaonyesha wito wake kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa OBC Ltd inanyang’anywa leseni.

Lakini jambo ambalo linazua maswali mengi ni kuhusu wawekezaji wengine walioko Loliondo. Kwanini hawahusishwi katika mpango wa kuondolewa au kwenye tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu? Hapa huhitaji maarifa zaidi kutambua kuwa mlengwa kwa mpango wote huu ni OBC. 

Kwanini wengine hawaguswi? Mbona hawapigiwi kelele licha ya ukweli kwamba hawana lolote la maana wanaloifanyia jamii ya Loliondo?  Ilitarajiwa kuwa kama suala ni la wafugaji ndani ya Loliondo, wawekezaji wengine nao wangesakamwa. 

Chukulia himaya za kampuni za Klein’s Camp, Dorobo Tours & Safaris; je, ni rafiki wa wafugaji? Jibu ni hapana. Suala hapa si kampuni gani, bali kwanini mkakati huu umeelekezwa kwa kampuni moja pekee miongoni mwa kampuni nyingi zilizoko ndani ya eneo moja la Loliondo.

Wanaojiita watetezi wa haki za binadamu wana ajenda yao mahsusi. Wakati fulani kulikuwa na kutoelewana kati ya wafugaji wa Kijiji cha Ololosokwan na kampuni ya Kleins Camp; Thomson dhidi ya Sukenya. Iliripotiwa kuwa baadhi ya watu walipoteza maisha. 

NGONET, PINGOS Forum, Oxfam Ireland na wengine walilifikisha suala hili katika Universal Periodic Review of Human Right process (UPR-process). Mbona hawasemi lolote? Kitu gani kiliwazima?

 

Ushiriki wa NGOs

 Ushiriki wa NGOs katika migogoro ya Loliondo si jambo jipya. Kinachoonekana kuwa kipya ni aina ya kampeni. Uongo uliibuliwa wakati fulani kuwa Serikali inataka kuwaondoa wafugaji wa Kimasai ili kupisha uwindaji wa kitalii. 

Kampuni inayotajwa kuwapo kwenye mpango wa kupewa eneo hilo ni OBC. Uzushi huo uliibua taharuki kubwa. Ilikuwa kampeni yenye malengo nyuma yake. Hao wanaoendesha propaganda hizi hawazungumzi lolote la kuwahusu wawekezaji wengine walioko Loliondo. 

Hii ni sababu tosha kwamba suala si la Wamasai wafugaji kuondolewa Loliondo au kupokwa ardhi, bali ni OBC ndiyo inayotakiwa iondoke. Kama sivyo, wawekezaji wengine waliopo eneo hilo, tena wasio na msaada wowote kwa jamii, nao wangehusishwa.

Pia ikumbukwe kuwa Oxfam ni shirika linaloongozwa na Wazungu. Ortello ni kampuni ya Waarabu. Wanaochochea vurugu hizi ni kampuni za Wazungu. Haihitaji akili kubwa kutambua kwamba hapa Mwarabu anapigwa vita ili Wazungu walitwae eneo hilo.

Kinachoenezwa kwamba ni mgogoro kati ya OBC na wafugaji katika LGCA si kinachochochea mgogoro kati ya pande hizo mbili. Inajulikana wazi kwamba OBC inachangia kwa kiwango kikubwa mno maendeleo na ustawi wa wafugaji katika eneo hilo, inasomesha watoto wengi hadi vyuo vikuu, inachangia maendeleo ya Wilaya ya Ngorongoro, sambamba na kuchangia pato la Taifa. Lakini mtu anaweza kujiuliza, inakuwaje kampuni inayoongoza kutoa huduma kama hizi ionekane kuwa haina manufaa kwa Loliondo na Taifa, lakini zile zisizochangia hapo dawati zionekane ni za maana.

NGOs zenye mlengo wa kibiashara zinashirikiana na Oxfam Ireland. Shirika hilo la misaada ndilo linalofadhili NGONET, Ujamaa Community Resource Trust (U-CRT) na PINGOS. Asasi hizi ndizo zinazosabambaza sumu ya chuki. Wakati fulani walizusha uongo wa kwamba Serikali inataka kuwaondoa wafugaji Loliondo. Kinachopaswa kuhojiwa hapa ni kwamba iweje asasi hizi za kibiashara ziitumie Oxfam Ireland ambayo miaka kadhaa iliyopita ilifunga miradi yake Loliondo? 

Kuna ushahidi unaojitosheleza kuwa baadhi ya NGOs hizi zinazoendeleza chokochoko zinafadhiliwa moja kwa moja na Sokwe Asilia na Rubin Hurt Safaris; NGONET kupitia Tanzania Natural Resources Forum (TNRF); ilhali Dorobo Tours and Safaris inafadhili U-CRT na PWC. NGOs hizi zimekuwa zikijihusisha na masuala ya Loliondo kwa miongo kadhaa sasa. 

Upo ushahidi usio na shaka kwamba karibu robo tatu ya madiwani wa Ngorongoro kwa wakati fulani, ama ni waajiriwa kwenye NGOs hizo, au ni sehemu ya wamiliki wake. Hawa ndiyo wanaopambana kuhakikisha kuwa OBC inaondolewa. Endapo ikiondolewa, ardhi yote ya vijiji itakuwa chini ya vijiji. Kwa sababu hiyo, madiwani kama mawakala wa Wazungu, watashiriki kuanzisha WMA na kwa sababu hiyo watakuwa na biashara kubwa na nono zaidi.

Kadhalika, mtandao wa Avaaz ambao sasa umevalia njuga uongo huu, unataka kujionesha kuwa imeguswa mno na suala la wafugaji katika Loliondo. Hata hivyo, hakuna ushahidi unaoonesha kuwa wamechukua hatua kama hizo kwa maeneo mengine nje ya Loliondo. 

Je, hii ni kutaka kusema kwamba wafugaji katika maeneo mengine nchini Tanzania hawakabiliwi na changamoto zinazofanana na zile za Loliondo? Kwa hakika yapo maeneo mengine nchini, lakini Loliondo ndipo penye kile wanachokitaka, hasa kutokana na ukweli kwamba kunapatikana wanyamapori wa aina zote ambao ni kivutio kikuu cha kampuni za uwindaji wa kitalii. 

NGOs zimekuwa zikienda nje zaidi ya kile ambacho zimekuwa zikijinasibu nacho, yaani kuwatetea wafugaji. Zimekuwa na masilahi na kampuni za utalii ambazo zimetajwa hapo juu. Oxfam Ireland , PINGO’s Forum, U-CRT, NGONET na Pastoral Women Council (PWC) zimekuwa zikihaha kuwa na uhusiano wa karibu wa kibiashara na kampuni za kitalii na mashirika mengine ya kimataifa ndani na nje ya Tanzania. 

Kinachonyamaziwa, na ambacho kwa muda mrefu hakijawekwa wazi ni kwamba NGOs hizi hazijihusishi moja kwa moja na kwa uwazi na masuala ya kibiashara, lakini nyuma yake ni za kibiashara zaidi. 

Dorobo Tours and Safaris ndiyo wafadhili na waendesha mambo mengi ya U-CRT na PWC.

Kulithibitisha hilo ni kwamba ofisi za U-CRT na PWC zipo ndani ya ardhi inayomilikiwa na Dorobo Tours and Safari. Ushirikiano huu hauhitaji maono ya ziada kuweza kutambua kilichofichika. Unaweza kujiuliza, inawezekanaje kwa NGO inayojihusisha na ‘haki za matumizi ya maliasili’ iwe pamoja na kampuni ambayo kazi yake ni kusaka faida? Hapa ikumbukwe kuwa ni kampuni hizi hizi zinazojihusisha na biashara za utalii ambazo zinalalamikiwa kwamba zinapora rasilimali za nchi na kuiacha jamii husika ikiwa masikini.

Kadhalika, David Peterson akiwa mmoja wa wakurugenzi wa Dorobo Tours and Safaris na vile vile U-CRT. Kwa hali kama hii huhitaji kuhangaika kujua ni kwanini U-CRT na PWC wanajihusisha mno kwenye mgogoro wa Loliondo. Katika kuthibitisha haya, tovuti ya Dorobo Tours and Safaris imeweka bayana.  Waweza kujionea haya kupitia [http://www.tanzanianorphans.org/dorobo.html]

na [http://www.marilynmason.com/dorobo.html]

 Kadhalika, Sokwe Asilia imekuwa na masilahi Loliondo; na kwa kuyalinda wamejipenyeza kwenye NGOs.  Wamefanya hivyo kupitia asasi ya “Honey Guide Foundation” ambayo inaifadhili TNRF. Muhimu hapa ni kwamba David Bell ni mmoja wa wajumbe mahiri kabisa wa Kamati ya Utendaji ya TNRF na pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa nyumba za wageni na kambi za Sokwe Asilia. Anapatikana zaidi katika kambi ya Suyan iliyo katika Kijiji cha Ololosokwan, Loliondo. 

 Katika “klabu” yao ya TNRF, Keith Roberts ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji, lakini pia ndiye anayeendesha Friedkin Conservation Fund ambayo inaendesha shughuli zake katika vitalu mbalimbali sehemu nyingi nchini Tanzania. Kiu yao ni kuongeza kitalu kingine cha Loliondo!

Ni wazi kwamba wafugaji katika maeneo mengine nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Wafugaji waliopo Kilosa, Bunda, Mvomero, Kilombero, Mbarali, Rufiji na sehemu mbalimbali za Tanzania wanahitaji kusaidiwa kuyakabili matatizo wanayopata. Lakini hawa wanaojiita wawekezaji, wakiwamo Oxfam kupitia NGOs mbalimbali wamejikita Loliondo pekee kana kwamba hakuna wafugaji sehemu nyingine za Tanzania.

Hapa ikumbukwe kuwa hata Jumuiya ya Ulaya (EU) ni miongoni mwa wachochezi wa mgogoro katika Loliondo. Hawa ndiyo wamekuwa wakijinasibu kwa kutaka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inadumu. Walishiriki kupinga ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu-Musoma. Lengo lao ni kuilinda Serengeti. Na ni hawa hawa wanaojua kwamba bila kuilinda Loliondo, Serengeti haipo!

Haya mataifa ya EU ndiko yule jasusi Susanna amekuwa akipokea mamilioni ya fedha na kuzigawa kwa NGOs ili zochochee migogoro isiyokoma. NGOs zinajua kula yao itaendelea kuwapo endapo migogoro itaendelea kudumu.

 

Uamuzi wa kugawa eneo

Serikali ilifanya uamuzi wa kuliondoa eneo la kilomita za mraba 2,500 kutoka Pori Tengefu la Loliondo na kuwapatia wananchi ili walimiliki kisheria na kuitumia ardhi hiyo kwa hiyari yao kwa ajili ya kuwaletea maendeleo. Eneo lililobaki la kilomita za mraba 1,500 likapangwa liendelee kuwa Pori Tengefu na kumilikiwa na Wizara kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009.

Serikali ilifanya hivyo kwa sababu kuu tatu: Mosi, ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori; Pili, ni sehemu ya mapito ya wanyamapori (ushoroba); na Tatu, ni vyanzo vya maji. 

Eneo hilo lilipangwa liendelee kuwa chini ya Wizara, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo-ekolojia wa Serengeti. Serikali ilichukua uamuzi huo kwa kuelewa kwamba mazingira ya uhifadhi ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mfumo-ekolojia na kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Lakini baada ya uamuzi huo kumekuwapo maoni ya kupotosha kutoka kwa NGOs na mawakala wao kupotosha ukweli wa mambo. Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya16 Vifungu Na. 4, 5 na 6 vinampa nguvu Waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali yenye lengo la kuleta manufaa kwa wananchi na kulinda uhifadhi.

Waziri alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa za utafiti na uchunguzi ambazo ziliwahi kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori(TAWIRI). 

Pia alizingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliokuwapo. Mojawapo ya tume hizo ni Tume ya Waziri Mkuu ya mwaka 2010 ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka wizara kenda, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro.

 

Hitimisho 

Watanzania na walimwengu hawapaswi kufundishwa tena kutambua nani wapo nyuma ya mchezo huu mbaya wa Loliondo. 

Kinachopaswa kujulikana sasa, na ambacho tunapaswa kwenda mbali zaidi, ni kujua ni nani hasa huyo mkubwa aliye nyuma ya “sinema” hii yote. Bila kukwepesha maneno, ni wazi kuwa Oxfam na kampuni za kigeni kupitia NGOs ndiyo wapo nyuma ya mchezo huu mbaya.  Hawa ndiyo wafadhili wakuu wa vikundi hivi. 

Wametafuta uongo wa kila aina kuhalalisha vurugu na migogoro isiyokoma katika Loliondo. Hakuna Serikali yoyote duniani ambayo inaongozwa na NGOs.

Uamuzi wa Serikali kwa Loliondo, hauna manufaa kwa Loliondo na Tanzania pekee, bali kwa ulimwengu mzima wa uhifadhi. Urithi wa wanyamapori unastahili kulindwa kwa busara zote. Wananchi wa Loliondo wana haki ya kuishi Loliondo na kuendesha shughuli zao, lakini haki hiyo haimaanishi kuwa wana haki ya kuzuia uhifadhi wa vyanzo vya maji, mapitio na mazalio ya wanyamapori. Bila kuwa na Loliondo kama “buffer zone”, Serengeti haipo.

Huu ndio wakati kwa Serikali ya Awamu ya Tano kumaliza mgogoro wa Loliondo. Lililo muhimu, ni kuzichunguza hizi NGOs ili zile zitakazobainika kuwa ni chanzo cha vurugu kwa maslahi ya wenye nazo, zifutwe.