Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mary Masanja (Mb) amekagua mradi wa kitalu cha miche ya miti wenye thamani ya shilingi milioni 43 unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza.

Akizungumza leo katika ziara,Masanja amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuitunza miche ya miti watakayokabidhiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili iweze kuleta matokeo chanya ya kuhifadhi mazingira.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb)(kulia) akikagua miche ya miti katika kitalu kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakati za ziara yake ya kikazi leo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali na wengine ni Maafisa wa TFS pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wilaya ya Magu.

“Tuwaombe wananchi miche hii watakapogawiwa waitunze vizuri kwa ajili ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo” amesisitiza .

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo, awamu ya kwanza zimetolewa fedha kiasi cha shilingi milioni 17 kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ambapo Serikali itaendelea kutoa fedha kwa awamu nyingine ili kukamilisha mradi.

Ameongeza kuwa lengo la uanzishwaji wa kitalu hicho ni kupunguza athari za uharibifu wa mazingira hususan katika Mkoa wa Mwanza ambapo kwa sasa utekelezaji wake umeanzia Wilaya ya Magu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kali amesema kupitia kitalu hicho wananchi wa Wilaya ya Magu watanufaika sana kwa sababu miche itapelekwa kwenye maeneo ambayo yalikwishaharibika ili kuyarudisha kwenye asili yake ya awali.

Aidha,Kali ametoa rai kwa wananchi kuitunza na kuilinda miche ya miti watakayokabidhiwa .

“Kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake na kwa wale wafugaji msiingize mifugo kwenye maeneo ambayo tumepanda miti”amesema Kali.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(wa pili kutoka kulia) akitoa maelekezo kuhusu kusimamia vizuri mradi wa kitalu cha miche ya miti kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakati za ziara yake ya kikazi leo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali na wengine ni Maafisa wa TFS pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wilaya ya Magu.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Kanda ya Ziwa, Thomas Moshi amesema kitalu hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha miche laki tatu kwa mwaka, hivyo kuendelea kuihudumia jamii ili kuhakikisha maeneo ambayo hayana miti uoto wa asili unarudi.

Amesema wananchi wanatakiwa kuelimishwa ili waweze kujua faida za miti katika kuleta nishati mbadala, kuleta mvua na pia kutumika kama mitishamba ya dawa za asili.Kitalu hicho kimefadhiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Mfuko wa Misitu Tanzania kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.