Mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA) umedumu kwa miaka miwili sasa, huku Waziri wa Maji akitajwa kuwa chanzo cha mkwamo huo.
Wakati Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, akitajwa kuwa chanzo kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni masilahi yake binafsi, yeye anasema anataka kuona haki inatendeka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA wa sasa, Nzinyangwa Mchany.
Tangazo la kujazwa nafasi hiyo lilitolewa kwa mara ya kwanza na Wizara ya Maji, Oktoba 2017 na waombaji zaidi ya 60 walijitokeza kuomba nafasi hiyo na kufanyiwa usaili wakati huo Waziri wa Maji akiwa Mhandisi Isack Kamwelwe. Kwa sasa Kamwelwe ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Kazi yote hiyo ikafutwa kwa maelekezo ya Waziri mpya, Mbarawa.
Machi, mwaka huu kukatolewa tangazo la pili kwa nafasi hiyo hiyo – ikiwa ni kutii maelekezo ya Waziri Mbarawa.
Taarifa kutoka ndani ya Wizara ya Maji zinathibitisha kuwa mchakato wa mwanzo ulikwenda vizuri kuanzia kwenye usaili, upekuzi (vetting) na majina matatu yaliyokidhi vigezo yalirejeshwa kwa waziri.
Mbarawa akiwa bado waziri mpya kwenye hiyo wizara, akajenga hoja ya kupinga majina hayo matatu akisema yeye hakushiriki kwenye mchakato huo, bali aliyakuta mezani, akimaanisha mtangulizi wake ndiye aliyefanya kazi hiyo.
“Ndiyo maana utaona tangazo lilirudiwa Machi, mwaka huu [2019]. Hiyo ilikuwa ni baada ya waziri kugoma kuchagua mmoja katika majina aliyoyakuta mezani kwake…mchakato ukaanza upya kabisa.
“Tangazo la mwanzo liliwavutia washindani 60, miongoni mwa waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni pamoja na Nzinyangwa Mchany, lakini hakufaulu kuingia kwenye mchujo,” kimesema chanzo chetu.
Kamati ya kuchuja majina ya walioomba iliundwa na wajumbe kutoka Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati, Baraza la Walaji la EWURA (EWURA CCC) na mjumbe mwingine kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Mmoja wa wajumbe wa mchakato huo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, ameliambia JAMHURI kwamba Kaimu Mkurugenzi Mkuu anayepigiwa upatu na Mbarawa hakuwahi kufikia wastani wa alama zilizowekwa ili kukidhi vigezo vya kuteuliwa; ukiachilia mbali michakato mingine inayoambatana na kufaulu usaili.
“Nimeshiriki kwenye interview (usaili) zote tatu za huyo ndugu, sikumbuki kama amewahi kufikia hata nusu ya alama zinazotakiwa mtu kushinda…hadi amefanya interview ya peke yake, wakati walioshindwa ni wengi – lakini bado hali ilikuwa tete.
“Nashangaa hao wakubwa huko wizarani sijui wana masilahi gani na huyu mtu, maana kwa hiki kinachoendelea sasa bila shaka washindani wake wanaweza kulalamika kwamba hapakuwa na ushindani wa haki, maana wao hawakupewa nafasi ya kufanyiwa usaili kwa mara ya pili.
“Binafsi kwa kweli nimekuwa nikishangaa kuhusu maelekezo ya Waziri wa Maji, maana inaonekana anamtaka huyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, lakini anapingana na mchakato wa upatikanaji wake, ningekuwa kwenye nafasi ya kumshauri ningemwambia amteue bila kuhangaika na hizi interviews,” kimesema chanzo chetu.
Hatua ya kufanyiwa usaili wa peke yake ni maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Lauren Ndumbaro. Sheria, kanuni na taratibu zinaeleza bayana hatua zinazopaswa kufuatwa ili kumpata Mkurugenzi Mkuu wa EWURA.
JAMHURI limemtafuta Dk. Ndumbaro atoe ufafanuzi wa jambo hilo, lakini akataka suala hilo aulizwe Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo.
Kwa upande wake, Profesa Mkumbo, ameulizwa na kusema serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo.
“Sitaki kusema chochote kuhusu suala hili, ila nikwambie tu kwamba jambo hilo linaendelea kufanyiwa kazi na serikali,” amesema Profesa Kitila.
JAMHURI limezungumza na Mchany, lakini ameshindwa kueleza sababu zilizomwezesha kufanyiwa usaili wa upendeleo akiwa peke yake baada ya ule uliowashirikisha washindani wengine.
Pia ametaka suala la usaili ziulizwe mamlaka zilizomuita kwenye usaili.
“Kwani mimi nilijiita? Chochote kinachohusiana na kuitwa kwangu kwa mara nyingine kwenye interview aulizwe Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,” amesema.
Mahojiano kati ya JAMHURI na Mchany yalikuwa hivi:
JAMHURI: Kuna taarifa kwamba umeitwa kwenye usaili ambao haukuhusisha washindani wako katika nafasi hiyo, ukweli ni upi?
Mchany: Wewe nani kakuambia niliitwa na kufanya interview peke yangu? Una uhakika na jambo hilo?
JAMHURI: Ndiyo maana tumekutafuta ili utuhakikishie suala hilo, twambie nini kimetokea hadi uitwe peke yako.
Mchany: Naomba masuala hayo aulizwe Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.
JAMHURI: Kuna suala la umri wako (miaka 57), maana moja ya kanuni za EWURA ni walau kumpata Mkurugenzi Mkuu ambaye ataweza kutumikia taasisi hiyo kwa vipindi viwili vya miaka minne, minne, wewe hautaweza hata kutumikia kipindi kimoja bila kuomba kuongezewa muda, unadhani hiyo nafasi inakufaa?
Mchany: Wewe unataka kufahamu umri wangu ili iweje? Tafadhali muulize mwajiri wangu maana kila kitu kinachonihusu mimi kiko kwake.
JAMHURI: Kwani unaona ugumu gani kunitajia umri wako sahihi?
Mchany: Nimekwambia wasiliana na mwajiri wangu, mbona hutaki kunielewa?
Gazeti la JAMHURI limezungumza na Profesa Mbarawa kuhusu mchakato wa kupatikana Mkurugenzi Mkuu wa EWURA. Mahojiano yamekuwa hivi:
JAMHURI: Mheshimiwa Waziri, tumesikia kwamba kwa masilahi yako binafsi unavuruga mchakato wa kupatikana Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, nini maoni yako?
Profesa Mbarawa: Nafikiri jambo hilo tuliache maana linafanyiwa kazi na mamlaka za juu, sitaki liende kwenye public (hadharani).
JAMHURI: Kwa nini hutaki liende kwenye public?
Profesa Mbarawa: Mamlaka zenyewe zitaamua…inabidi tupate baraka za viongozi, ninajua vitu vingi sana ila kwa sasa acha nikae kimya. Bora likae hivyo, naamini lilivyofanyika ni kwa nia njema kabisa.
JAMHURI: Kwa nini unaonekana kumkingia kifua Kaimu Mkurugenzi wa EWURA katika mchakato wote huu?
Profesa Mbarawa: Maisha haya ya duniani tunapita…sitaki kumwonea mtu, maana najua kuna kesho, ni maisha tu.
JAMHURI: Uchunguzi wetu umebaini kwamba huyo unayemkingia kifua tayari ameshafeli kwenye usaili mara tatu, unalijua hilo?
Profesa Mbarawa: Nimesema sipendi kumwonea mtu, tusubiri mamlaka zitaamua. Lakini si sahihi kutaka kudhulumu haki ya mtu. Mimi ni waziri ambaye chini ya wizara yangu kuna wakurugenzi wakuu wengi, ninazo mamlaka kadhaa za maji, kwa nini watu wanasema kuhusu hili tu?
JAMHURI: Zipo taarifa kwamba umehongwa Sh milioni 50 ili kuhakikisha huyo mtu anakuwa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, hilo unalizungumziaje?
Profesa Mbarawa: Mimi nimeshughulika na makandarasi wengi nikiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambako kuna makandarasi wengi; je, umewahi kusikia kuhusu mimi kujihusisha na rushwa? Wewe si mhariri wa kwanza kunihoji kuhusu tuhuma hizo, tukikutana tutazungumza kwa uhuru zaidi.
Mimi nimechagua wakurugenzi wakuu kadhaa akiwemo yule wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini na Majini (SUMATRA). Hivyo kulaumiwa katika kazi hizi ni vitu vya kawaida, lakini nasisitiza kwamba kuna leo na kesho nitaondoka wizarani. Siwezi kuchukua hizo Sh milioni 50.
JAMHURI: Kwa nini unadhani wanakusingizia kwamba umechukua rushwa ya Sh milioni 50?
Profesa Mbarawa: Hiyo inafanywa makusudi ili kuniongezea presha kufanya uamuzi juu ya jambo hili la Mkurugenzi Mkuu wa EWURA. Kuna watu wana masilahi yao na nikuhakikishie kwamba sitayumbishwa na hizo presha zinazokuja.
JAMHURI: Huyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA ambaye unampigania kama ulivyosema kwamba hupendi kumwonea mtu, mbona ana miaka 57, na sheria ya EWURA inataka walau Mkurugenzi Mkuu aweze kutumikia vipindi viwili vya miaka minne minne, hilo unalifahamu?
Profesa Mbarawa: Nimesema tusubiri mamlaka zitasema, tena jambo lenyewe limefikia hatua nzuri sana…sitaki kuvunja kiapo changu cha uwaziri kwa kusema kinachoendelea, wakati naapa nilishika msahafu…
Suala la umri ni kweli sheria ya EWURA inaelekeza kwamba Mkurugenzi Mkuu anatakiwa kutumikia mihula miwili ya miaka minne minne, lakini tambua kwamba umri siyo tatizo kama mamlaka zikiona ‘potential’ ndani yake, ipo rekodi ya wakurugenzi ambao wameteuliwa huku wakiwa na umri zaidi ya huo, wengine wanateuliwa kutoka nje ya mfumo huu wa serikali.
Hiyo yote ni namna nchi inavyoona mhusika anastahili kuitumikia. Tambua jambo moja, huyo mtu anayesemwa si ndugu yangu wala hatoki Pemba. Waziri ni sawa na kocha wa timu ya soka, anajua ni wakati gani amtumie mshambuliaji yupi, anaweza kumwingiza mchezaji ndani ya dakika tano akafunga goli.
Usuli
EWURA ni mamlaka ya udhibiti inayojitegemea iliyoanzishwa Februari 2006 chini ya Sheria ya Udhibiti wa Nishati na Maji (cap. 414). Inasimamia udhibiti wa kiteknolojia na kiuchumi katika sekta tatu ambazo ni umeme, mafuta na maji. Awali ilikuwa inasimamia na gesi pia, ila imehamishiwa kwa Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).
Tangu kuanzishwa kwake, wakurugenzi wakuu wa EWURA wamekuwa ni Haruna Masebu na Felix Ngalamgosi; kabla ya Mchany kukaimu nafasi hiyo.
Akiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Mbarawa alikabiliwa na tuhuma kama hizi za sasa kwa kuhakikisha nafasi ya juu ya TCRA inashikwa na mtu ambaye kwa taarifa za kiuchunguzi hakuwa na sifa. Baadaye Rais Magufuli aliingilia kati na kuweka uongozi makini wa sasa chini ya Mhandisi James Kilaba.