Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene, Alhamisi iliyopita alishindwa kuzuia hisia zake, pale alipolipa sifa Gazeti la JAMHURI huku akisimamia ubomoaji wa mgahawa uliojengwa katika eneo la wazi jijini.
Akiwa eneo la tukio, katikati ya barabara za Samora na India akisimamia ubomoaji wa jengo hilo, Simbachawene anasema, “Ahsante sana JAMHURI” iliyoibua taarifa za ujenzi huo holela. Operesheni hii ni mwendelezo wa kuyakomboa maeneo yote ya wazi, kwa sababu sheria ziko wazi ikiwamo Sheria namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 na waliohusika wamefanya uhuni wa hali ya juu,” anasema.
Naibu waziri huyo anasema sheria imefafanua vizuri kwamba maeneo yote ya wazi ni kwa ajili ya matumizi ya umma, na hakuna ruhusa kujenga majengo ya biashara au makazi ndani ya maeneo hayo.
Amesema kitendo kilifanywa na uongozi wa Manispaa ya Ilala kuruhusu kujengwa jengo la mgahawa ndani ya bustani ya Samora na kuharibu mazingira ya eneo hilo kwa madai kuwa wanaendeleza maeneo ya wazi, ni uhuni na waliohusika na uhuni huu ndani ya Manispaa hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Jengo la mgahawa huo lililokuwa likiendelezwa na kampuni ya Easy Payment Limited, limebomolewa mwishoni mwa wiki iliyopita chini ya usimamizi wa Simbachawene na maofisa wengine wa wizara.
Hatua hiyo imekuja baada ya Gazeti la JAMHURI kuandika habari ya uchunguzi kuhusu viongozi wa Jiji la Dar es Salaam ‘kuuza’ eneo hilo la wazi kwa kampuni hiyo ambayo haipo kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wala wamiliki wake hawajulikani.
Uchunguzi wa gazeti hili uliodumu kwa kipindi cha miezi mitatu, ulibaini kuwa hakuna jina lolote la kampuni ya Easy Payment Limited lililoorodheshwa miongoni mwa kampuni zilizosajiliwa kwa wakala huyo kwenye vitabu au kwa njia ya electroniki.
Taarifa zinasema kwamba tangu enzi za ukoloni na baadaye Uhuru wa Tanganyika (Tanzania), eneo hilo lilitengwa na jiji kwa matumizi ya bustani ya kupumzika, na mwaka 2010 liliboreshwa zaidi kwa kuwekwa choo cha umma kwa sababu ya ongezeko la watu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Februari 8, 2012 eneo hilo ‘lilivamiwa’ na Kampuni ya Easy Payment Limited mara baada ya kusaini mkataba unaoelezwa kuwa ni kwa ajili ya kuliboresha huku viongozi wa Manispaa ya Ilala wakibariki kitendo hicho.
Mafundi wa kampuni hiyo walikuwa wanafanya shughuli za kuendeleza eneo hilo usiku tu kwa kujenga mgahawa mkubwa uliopewa jina la Harold. Imeelezwa kwamba mkataba huo utadumu kwa kipindi cha miaka mitano.
Kitendo cha kampuni hiyo kuendesha shughuli zake za ujenzi wa jengo ndani ya eneo hilo bila kibali cha ujenzi, kimeelezwa na wananchi wanaoishi jirani na bustani hiyo kuwa ni mkakati wa baadhi ya viongozi kupora maeneo ya wazi yaliyopo katikati ya jiji.
Juma Suleiman anayefanya shughuli zake za biashara Mtaa wa India, anasema kuwa jambo linalowashangaza ni shughuli za ujenzi wa jengo la kudumu ndani ya bustani hiyo zinazofanyika kwa kuvizia nyakati za usiku bila kibali cha ujenzi huku Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, akitembelea mara kwa mara.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kingine cha habari (jina tunalo), walipeleka taarifa za uvamizi wa eneo hilo kwa Mtendaji Kata ya Mchafukoge, Yusuph Mkwawa, Julai 11, mwaka jana na alipopeleka amri ya kusitisha ujenzi, wahusika hawakuipokea huku wakidai uongozi wa Manispaa unafahamu kinachoendelea.
Mkwawa alipohojiwa kuhusu taarifa hizo akasema, “Nafahamu jambo hili. Nakumbuka mwezi Julai niliambatana na Ofisa Mkaguzi wa Majengo wa Kata hadi eneo la tukio ili kuwakabidhi nakala ya amri ya kusitisha ujenzi, lakini waligoma kuipokea kwa madai kuwa viongozi wa Manispaa wanafahamu suala hilo.”
Ofisa Mkaguzi wa Majengo wa Kata hiyo, Dotto Muhombolage, alipohojiwa na JAMHURI anaeleza kuwa Juni 23, mwaka jana aliagizwa na mkuu wake wa kazi (Mhandisi wa Manispaa) kupeleka nakala ya amri ya kusitisha shughuli za ujenzi ndani ya bustani hiyo, lakini hakuna aliyepokea.
Muhombolage anaeleza, baada ya wahusika kukataa kuipokea nakala hiyo, aliamua kubandika kwenye uzio wa mabati uliozungushwa katika eneo hilo ili wahusika wanaposoma wasitishe ujenzi huo.
“Kipindi hicho niliagizwa kupeleka nakala ya amri ya kusitisha ujenzi ndani ya bustani hiyo unaofanyika bila kibali cha ujenzi, kulikuwa na mchanga na kokoto tu huku miti ya kivuli iliyopandwa muda mrefu ikikatwa yote na anayejenga ndani ya eneo hilo,” anaeleza.
Anasema Julai 2 aliagizwa tena na mhandisi kupeleka nakala nyingine (remainder), nayo pia haikupokewa na wahusika na hivyo kuamua kuibandika tena kwenye uzio wa mabati uliozungushwa katika eneo hilo.
Hata hivyo, alieleza kuwa hafahamu lolote kuhusu hatua zilizochukuliwa hadi wakati huo na anayeweza kuzungumzia hilo ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgulumi.
Chanzo chetu kimeeleza kuwa mkataba wa kubadilisha matumizi ya eneo hilo ulioanza Januari 20, 2012 hadi Januari 2017 unadaiwa kughushiwa na uongozi wa kampuni hiyo kwa msaada mkubwa wa vigogo wa Manispaa hiyo, kwa lengo la kujimilikisha eneo la wazi kinyume cha sheria.
“Hawa jamaa hawakuwa na kibali cha ujenzi ndani ya eneo hilo, mkataba wao unatia shaka na kinachofanyika eneo hilo ni uharibifu wa mazingira na mandhari ya jiji, na kinachotajwa kuwa kuweka vivutio na kuboresha bustani hiyo ni utapeli mtupu,” kinaeleza chanzo hicho.
JAMHURI ilipomtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Mgulumi, ili kuelezea uvamizi wa eneo hilo la wazi, hakuweza kupatikana, na alipotumiwa ujumbe mfupi (sms) wa maswali katika simu yake ya kiganjani hakutoa jibu lolote.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Silaa, anayedaiwa kukagua shughuli za ujenzi unaofanyika bila kibali nyakati za usiku, alipotafutwa na Gazeti la JAMHURI kwa simu yake ya kiganjani, anasema kwamba wanachokifanya ni kuendeleza tu maeneo hayo na kwamba tayari wamefanya uendelezaji hata eneo lililo jirani na Hospitali ya Ocean Road, jijini.
Aliyekuwa Mwanasheria wa Manispaa hiyo, John Wanga, ambaye ni miongoni mwa watu waliosaini mkataba huo unaodaiwa kuwa ni wa kitapeli, na sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema haelewi chochote na mwenye maelezo ya kutosha ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Easy Payment Limited, Hillary John, hakuweza kupatikana wakati jengo lake lilipokuwa likibomolewa na Manispaa ya Ilala kwa katapila lenye namba za usajili SM 3937 ndani ya eneo hilo la wazi.