Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
IMEELEZWA kuwa wazazi wana jukumu la kuwaendeleza watoto wao kwa kuwapatia elimu bora na kuwafundisha stadi za maisha.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mwalimu Irene Muthemba wakati wa mahafali ya 19 ya kidato cha Sita ya Shule Huria ya Ukonga Skillful.
Alisema elimu ndio ufunguo wa maisha na njia ya kumsaidia mtoto kuondokana na ujinga pamoja na kuwa na maisha bora.
“Nichukue fursa hii kutoa wito kwa wazazi watengenezee mazingira mazuri ya elimu watoto wao ili wasije kusumbua baadae. Kwahiyo mtoto anapofeli usimuache nyumbani mpe fursa nyingine ya kuweza kujiendekeza kielimu,” alisema Mwalimu Mathemba.

Alitoa wito kwa wanafunzi kutokukata tamaa na badala yake wasome kwa bidii ili waweze kufikia ndoto zao.
“Yote yanawezekana ukiweka nia na malengo. Mshikeni elimu msimuache aende zake maana shetani hayuko mbali, nyinyi wote safari mlizozipita msishangae ni agizo la Mungu
“Someni, elimu ni agizo kutoka kwa Mungu, soma usikate tamaa, pambana mpaka kieleweke kwani ukiwa na elimu unakuwa na chanzo kizuri na msingi mzuri wa maisha,” alisema.
Aidha aliupongeza uongozi wa shule Huria ya Ukonga Skillful na walimu kwa ujumla kwa kutoa elimu na malezi bora kwa wanafunzi hao.
Awali Mwasisi wa Shule Huria ya Ukonga Skillful, Diodorus Tabaro amesema mahafali hayo yamehusisha wanafunzi 78 kutoka Shule ya Ukonga Skillful Makao makuu pamoja na Tawi la Mbezi Louis.

Amefafanua kuwa wanafunzi hao wamegawanyika katika michepuo ya Sayansi, Biashara na Sanaa.
Amesema tangu shule hiyo ianzishwe miaka 19 iliyopita imefanikiwa kufaulisha wanafunzi wengi kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali vilivyopo hapa nchini.
“Miaka 19 imekuwa safari ya milima na mabonde, ya kuwanyanyua Watanzania katika kupata elimu. Tupo kwaajili ya kutumika ili yule waliyemuona hawezi wampigie saluti na kumuheshimu.
“Mwaka jana waliohitimu asilimia 98 wamefaulu vizuri, wameenda vyuo vikuu na tunaomba na mwaka huu wafaulu vizuri. Sisi tunaamini hatuwezi kufanikiwa bila mkono wa Mungu,” amesema Tabaro.
Akisoma risala, Mmoja wa wahitimu, Suzanne Martin amesema wamejiandaa vyema kufanya mtihani wa mwisho wa kumaliza kidato cha Sita.
“Walimu wamefanya kazi kubwa kuhakikisha tumefanya mitihani mingi ya kutosha ambayo itatusaidia kumuongezea uwezo pamoja na ujasiri katika mtihani Wetu wa mwisho,” amesema Suzanne.