Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha
Wazazi wa jamii ya Kimasai wamemuomba Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum , Dorothy Gwajima, kuingilia kati kitendo cha watoto wao kuchukuliwa kinyemela kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita kwa kuahidiwa ufadhili wa masomo.
Wamedai kuwa tangu wachukuliwe hadi sasa hawajui watoto wao walipo na wamekosa ushirikiano kwa waliohusika kuwachukua .
Aidha wazazi hao ambao wametokea kitongoji cha Olobo kilichopo kijiji cha Lopolun kata ya Olorien na Magaiduru katika tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha walidai kuwa watoto wao wamesikia wapo mkoani Arusha na wamebadilishwa majina na kupewa majina ya kiislamu.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Januari 19, 2025 katika ofisi za Shirika la MIMUTIE WOMEN ORGANIZATION lililopo mkoani Arusha ,wazazi wa watoto hao ambao ni Nalangu Koila ,Naramat Ngai na Leyaley Salangat wamesema kuwa, mwaka 2015 watoto watatu wote wanawake wajulikanao kwa majina ya Seyo Koila, Kitindi Ngai na Timbiyani Salangati walichukuliwa chini ya usimamizi wa Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ngorongoro ajulikanaye kwa jina la Benezeth Bwikizo .
Wemesema kuwa, watoto hao walichukuliwa kwa taarifa kwamba wanakwenda kupatiwa ufadhili wa kusomeshwa na wakati watoto hao wanachukuliwa mwaka huo walikuwa na umri wa miaka mitano na hadi sasa watoto hawajarudishwa kwa wazazi wao na wala wazazi wao hawana taarifa ya watoto wao walipo.
“Tangu watoto hawa wanachukuliwa sisi tulikuwa hatujui watoto wanapelekwa sehemu gani, kwani alikuja mtu mmoja aitwaye Mepukori ambaye kwa mwaka huo alikuwa Mwenyekiti wa Kitongoji na Oloboo na ndiye alieenda kwa wazazi wa watoto hao na kudai kuwa ameagizwa na Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ngorongoro Benezeth Bwikizo aje kutafuta watoto ambao hawana uwezo ili wasaidiwe “amesema mzazi Naramat Ngai
Aidha wamesema kuwa, Mepukori ndiye aliyechukua watoto hao mikononi kwa wazazi wao na kuwapeleka kwa Benezeti baada ya watoto hao kufikishwa kwa Benezeti alibadili taarifa za watoto hao na kuwaandikisha kama watoto yatima , na wazazi walipouliza kuhusu watoto wao hawakupewa taarifa yeyote ya mahali watoto hao walipo na mtu ambaye aliwachukua watoto hao kwa wakati huo.
“Wakati watoto hao wanachukuliwa na kusafirishwa siyo ndugu wa watoto au wazazi wa watoto waliyejua ni wapi watoto wao walikuwa wanapelekwa na hakukuwa na makubaliano yeyote yaliyofanyika kati ya waliochukua watoto kwa wazazi ,waliotoa idhini ya watoto hao kuchukuliwa, yaani afisa ustawi wa jamii na wala makubaliano kati ya aliyechukua watoto na wazazi wa watoto hao.” Wamedai wazazi hao.
Aidha baadaye wazazi walipohoji kuhusu mahali Benezeti alipowapeleka watoto, Benezeti aliwaambia wazazi hao wawasiliane na mtu ambaye yupo na watoto, mtu ambaye wazazi hao walikuwa hawamfahamu kwa wakati huo.
Hata hivyo wazazi hao wamesema kuwa, baadaye mwaka 2021 mwenyekiti mpya wa kitongoji cha Oloboo alifuatilia suala hili baada ya wanakijiji wengine kusimama wakitaka watoto hao warejeshwe makwao ndipo Benezeth alipomkutanisha mwenyekiti huyo ambaye ni Mohamed katika Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mount Meru na kusema kuwa huyo ndiye aliyewachukua watoto hao na mwenyekiti aliweza kuwaona watoto hao lakini hakupata nafasi ya kuzungumza nao chochote.
Wakati huo huo ,Shirika la Kutetea Haki za Watoto na Wanawake la MIMUTIE WOMEN ORGANIZATION limeingilia kati sakata la kupotea kwa watoto hao baada ya kupata taarifa ya kuchukuliwa kwa watoto hao katika mazingira ya kutatanisha .
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo ,Rose Njillo amesema kuwa, waliamua kufuatilia kwa huyo Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo ambapo alisema ni kweli kuwa watoto hao wamechukuliwa lakini aligoma kutoa ukweli wa taratibu za kisheria zilizotumika kuwachukua watoto hao na pia aligoma kutoa taarifa inayoonyesha jinsi watoto hao walivyochukuliwa na kusema taarifa hiyo anaweza kuitoa mahakamani pekee yake.
“Pia baada ya Benezeth kuulizwa zaidi ,alisema kuwa suala hili litaendelea kufuatiliwa, basi atasimamisha ufadhili wa watoto hao ,na kusema kama mnataka kuwarudisha hao watoto je mnaweza kurudisha gharama zilizotumika kuwatunza hao watoto “alisema Bwikizo.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema kuwa,wao kama wanaharakati wa masuala ya ulinzi na usalama wa watoto ,wanaamini kwamba watoto wana haki ya kuwaona wazazi wao hata kama waliishi katika mazingira magumu na wazazi wana haki ya kuwaona watoto wao.
Hao wao kama watetezi wamemuomba Waziri Gwajima kuingilia kati na kuwachukulia hatua wote waliohusika kuwachukua watoto hao wa jamii ya kimasai bila idhini ya wazazi wao kwa lengo la kujinufaisha,huku wakilitaka Jeshi la Polisi kuingilia kati na kuchukua hatua kwa wale waliobainika kushiriki mpango wa kuchukua watoto hao na kuwapeleka kusikojulikana.
Wamedai wahusika wa tukio hilo hawana tofauti na watu wanaofanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu .
Kwa upande wa Afisa Ustawi wa Jamii akihojiwa na waandishi wa habari kwa njia ya simu juu ya tuhuma hizo alisema hawezi kuzngumzia sula hilo hadi atakapopewa idhini ya kuzungumzia na bosi wake ambaye hakumweka bayana ni yupi.
“Siwezi kuzungumzia suala hilo.kwani mimi sio msemaji hadi nitakapopewa idhini na mkuu wangu wa kazi “amesema Benezeth Bwikizo.