*Ni ya kulinda Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki
*Kampuni ya kigeni iliyopata kazi ya kulinda haipo eneo la mradi
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kampuni ya Ulinzi ya Garda World Tanzania Limited inayomilikiwa na raia wa Canada hapa nchini inadaiwa kutumia ‘ujanja’ kupata zabuni ya kazi ya ulinzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Kampuni hiyo yenye ofisi zake Mtaa wa Lucy Lameck, Mikocheni jijini Dar es Salaam ilijisajili kuwa kampuni ya kizawa ikikusudia kutumia fursa hiyo kuomba zabuni ya ulinzi katika mradi huo, lakini baada ya kupata ikatumia kampuni nyingine kutoa huduma kinyume cha sera na sheria za EACOP.
Kwa mujibu wa sera na sheria za utekelezaji wa EACOP, kampuni za wazawa ndizo pekee zinazopaswa kupewa kipaumbele katika utoaji wa baadhi ya huduma zilizoanzishwa katika mradi huo ikiwamo ya ulinzi.
“Garda World Tanzania Limited ndiyo inayomiliki Kampuni ya Garda World Kenya Kazi Security (T) Ltd, ambayo ina asilimia 50 ya hisa za Kampuni ya Ultimate Security. Ilitumia uwezo wake wa kiushawishi kupata zabuni ya ulinzi kwenye mradi wa EACOP kwa kutumia Garda World West Security Limited.
“Lakini inatumia walinzi wa kampuni yake nyingine ya KK Security kutoa huduma ya ulinzi katika ofisi za EACOP zilizoko Masaki na saiti (mradi unakotekelezwa). Jambo hili si halali. Kazi hii ilipaswa kufanywa na kampuni za ulinzi za wazawa zilizopo hapa hapa nchini,” kinaeleza chanzo chetu (jina linahifadhiwa) kilichopo ndani ya Garda World Tanzania Limited.
Pamoja na ukweli kwamba Garda World West Security Limited haipo kwenye eneo la mradi lakini ndiyo inayotumiwa na wakurugenzi wa Garda World Tanzania Limited kuomba fedha serikalini na kuelekeza ziende wapi.
Kwa mujibu wa chanzo hicho maelekezo hayo huonyesha kwamba yametolewa na Garda World West Security Limited lakini kiuhalisia yanakuwa yametolewa na Garda World Tanzania Limited.
Katika kuthibitisha madai hayo JAMHURI imeshuhudia ankara ya madai namba PVS10000507 ya Desemba Mosi, 2022 iliyotolewa na Garda World West Security Limited yenye thamani ya Sh 14,285,530, VAT Sh 2,571,395.40 huku jumla yake ikiwa ni Sh 16,856,925.40 kwenda EACOP.
Licha ya ankara hiyo kuandaliwa Desemba Mosi, 2022 lakini inaonyesha kwamba imepokewa Novemba 30, 2022 na Regina Charles wa EACOP na imeelekeza fedha hizo ziingizwe katika akaunti namba 103895100026 ya Benki ya NCBA ya Kampuni ya Kenya Kazi Security (T) Ltd.
Pia JAMHURI imeona mwenendo wa kampuni hiyo inavyoandaa ankara zake nyingine ikielekeza namna malipo yao yanavyotakiwa kufanywa.
Katika ankara hizo, Garda World West Security inaomba fedha na kutoa maelekezo ilhali haijafanya kazi yoyote katika eneo la mradi.
Uthibitisho mwingine ulioonwa na JAMHURI ni barua ya Novemba 28, 2022 iliyosainiwa na Goodluck Lukumay kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Garda World Tanzania Limited yenye muhuri wa Kenya Kazi Security (T) Ltd inayowataka wateja wao kulipa ankara zao mapema.
“Mtindo unaotumika kukwepa kodi ni kampuni moja kuomba kulipwa lakini katika malipo hayo hayo inaagiza malipo yalipwe kwenye kampuni nyingine ambayo ni mbia wake. Hiki kinachofanyika kwenye invoice kama si uhuni ni nini?
“Hawa watu wanachanganya hesabu makusudi wakilenga kuichanganya TRA ili wasigundue kama kampuni hizo zote ni kampuni moja iliyojigawa katika matawi matatu,” kinaeleza chanzo kingine.
Katika kutafuta ukweli wa madai hayo JAMHURI imefika mara kadhaa Mikocheni zilipo ofisi za Garda World Tanzania Limited, pamoja na mambo mengine wahusika walielekeza kuandikiwa barua.
“Mkurugenzi wa Garda World si mtu anayepatikana kwa urahisi, ana shughuli nyingi mno, kwa sasa yuko kwenye vikao Kenya, ujue kwanza ofisi zetu zina matawi hadi nchini Kenya, kwa hiyo kama suala lenu ni nyeti ni vema mngelileta kwa njia ya maandishi hapo ingekuwa rahisi kupatiwa majibu yenu,” anaeleza ofisa mmoja aliyeko mapokezi ya ofisi hiyo.
Mei 22, mwaka huu JAMHURI imeandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Garda World Tanzania Limited ambayo pamoja na kupokewa hadi leo haijajibiwa.
Baada ya barua hiyo kuwasilishwa, mwandishi wa habari hii alifuatilia na kupatiwa namba ya simu ya Meneja Undeshaji wa Garda World Tanzania Limited, Goodluck Lukumay, ambaye mara kadhaa alipowasiliana naye alimjibu kuwa majibu yanashughulikiwa.
Wakati Lukumay akitoa majibu hayo kwamba maswali yanafanyiwa kazi, imebainika kampuni hiyo ilikuwa kwenye mikakati ya kuficha ukweli kwa kubadilisha mikataba ya wafanyakazi wenye mikataba ya KK Security waliopelekwa katika maeneo ya ulinzi ya EACOP.
Awali, JAMHURI imeelezwa kuwa walinzi wa KK Security walipelekwa kulinda wakiwa na sare na mikataba ya kampuni hiyo lakini baada ya sakata hilo kuanza kufuatiliwa wamebadilishiwa sare na mikataba kwa kuondoa nembo kwenye mikataba ya awali na kuweka nembo ya Garda World West Security Limited.
“Tuliitwa ghafla na kuelezwa kwamba kuna mabadiliko yamejitokeza kwenye mikataba yetu. Kwanza tulijua tumefukuzwa kazi, kumbe tulikuwa tunaelezwa kuwa mikataba yetu imehamishwa kutoka KK Security kwenda Garda World West Security.
“Wengi wetu tulishituka kwanza, tukahoji masilahi yetu kwenye mkataba mpya yatakuwaje lakini wakatutuliza kuwa mwajiri ameekezwa kuzingatia sera na sheria za nchi, hivyo tukubali kupewa mikataba ya Garda World West Security. Tulihamaki lakini wakatueleza kilichobadilishwa tu ni nembo kwenye mkataba lakini mambo yote yako vilevile,” anasema mmoja wa walinzi wa KK Security aliyebadilishiwa mkataba wa mwanzo Juni, mwaka huu (jina lake linahifadhiwa).
Katika hatua nyingine, JAMHURI imewasiliana na ofisa mwandamizi ndani ya EACOP kwa upande wa Tanzania (jina linahifadhiwa), alijibu kwa ufupi kuwa hakuna zabuni ya ulinzi iliyotangazwa rasmi kwa ajili ya kampuni kuanza kuomba.
“Kwanza hili suala halipo kwetu EACOP bali lipo EWURA, hao ndio wenye jukumu la kutangaza zabuni zote za mradi wa ujenzi wa bomba,” amesema.
Aidha, amesema inawezekana Garda World West Security Limited walipata zabuni hiyo kupitia kwa makandarasi walioko eneo la mradi wakifanya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya EACOP, muundo wa kisheria na kibiashara wa mradi huo ulianzishwa katika mkataba wa nchi hodhi uliosainiwa Aprili 11, 2021 na Mei 20, 2021 kati ya EACOP na serikali za Uganda na Tanzania.
Kwa upande wa Uganda, EACOP inasimamiwa na Mamlaka ya Petroli ya nchini humo pamoja na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira.
Kwa upande wa hapa nchini Tanzania, EACOP inasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Pia kwa upande wa Uganda, mfumo wa EACOP una kilomita 296 za bomba linalojengwa na vituo viwili vya kusukuma mafuta, huku Tanzania mfumo wa EACOP una kilomita 1,147 za bomba, kituo cha kuhifadhi mafuta, vituo vinne vya kusukuma mafuta na vituo viwili vya kupunguza mgandamizo wa mafuta, huku uzalishaji wa mafuta ukitarajiwa kuanza rasmi mwakani.
EACOP inakusudia kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda kwenda Bandari ya Tanga kupitia Bahari ya Hindi, na baada ya kukamilika litakuwa bomba refu zaidi duniani linalopashwa moto.
Bomba hilo litaanzia katika kaunti ndogo ya Buseruka, Wilaya ya Hoima, Mkoa wa Magharibi mwa Uganda.
Kisha litaelekea kusini mashariki kupita Masaka nchini Uganda na kuzunguka pwani ya kusini mwa Ziwa Victoria kupitia Shinyanga, Singida, Kagera, Geita, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na kuishia Tanga. Pia linapita katika wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.