Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepata mafanikio makubwa kufuatia kuhukumiwa kwa watuhumiwa kadhaa wa makosa ya kikatili ambao mashauri yao yalikuwepo katika Mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameyataja mashauri hayo kuwa ni kubaka, kulawiti pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kamanda Muliro amewataja watu hao ambao wameufunga mwaka vibaya baada ya kukutwa na hatia na kuhukumiwa, kuwa ni Sadock Foreni (30), mkazi wa Mbagala Dar es Salaam, amehukumiwa katika Mahakama ya Temeke, kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.
Joseph Fedinand (35), mkazi wa Mbagala, nae amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.
Ayoub Khatib (32), mkazi wa Tabata Dar es Salaam, amehukumiwa katika Mahakama ya Kinyerezi kwenda Jela miaka 30 kwa kosa la kubaka.
Salmon Athuman (30), Kitunda Dar es Salaam, amehukumiwa jela miaka 30 kwa kosa la unyanga’nyi wa kutumia silaha.
Henry Peter, mkazi wa Mbezi Dar es Salaam, amehukumiwa katika Mahakama ya Ubungo kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka.
Naye Ramadhan Amiri (30), mkazi za Kawe, amehukumiwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kinondoni kwenda jela miaka 30 kwa kosa la unyanga’nyi wa kutumia silaha.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Ally Ismail (22), mkazi wa Kipunguni Mashariki, kwa tuhuma za uvunjaji.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Desemba 17, 2024 na kupatikana na vitu mbalimbali vya wizi vikiwemo Redio, kompyuta za mezani 3, kompyuta mpakato 2, Simu janja 8, ndogo 6, Kamera Samsung 1, Vinga’muzi 4, Keyboard aina ya Dell 4, Televisheni 3, begi kubwa moja lenye nyaya mbalimbali, jiko 1, mtungi wa gesi 1 na mashine ya kunyunyizia dawa shambani.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni.
Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi limejipanga kushuka chini, kuwa karibu na wananchi, kupokea taarifa na kuzifanyia kazi, na kuahidi kuwa halitakuwa na huruma na mtu yeyote, atakayekamatwa atashughulikiwa vikali kwa kuzingatia misingi ya kisheria.