Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Tabora

WATU wawili wakazi wa Wilaya ya Nzega na Uyui mkoani Tabora wamefikishwa mahakamani na Jeshi la Polisi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la ubakaji watoto.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa ACP Richard Abwao amethibitisha kutiwa hatiani watuhumiwa hao baada ya kukamatwa kwa nyakati tofauti na kufunguliwa mashtaka ya ubakaji.

Alitaja waliohukumiwa kuwa ni Josephati Jackson (59) mkazi wa Nzega ambaye alikuwa anatuhumiwa kubaka mtoto wa miaka 9 katika kijiji na kata ya Semembela, tarafa ya Bukene, Wilayani Nzega.

Mwingine ni Katanga Adamu John mkazi wa Wilaya ya Uyui Mkoani hapa ambaye alishtakiwa kwa kosa kama hilo baada ya kutuhumiwa kufanya mapenzi na binti pasipo ridhaa yake.

Aidha Kamanda Abwao alieleza kuwa watuhumiwa 3 wamefikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma za kukutwa na mali za wizi, watuhumiwa hao wamekamatwa hivi karibuni katika maeneo ya Kanyenye mjini hapa.

Alitaja vitu walivyokutwa navyo kuwa ni pikipiki aina ya SunLG yenye namba za usajili MC 156 DMG rangi nyeusi, pikipiki SunLG yenye rangi nyekundu iliyokuwa imefichwa namba kwa gundi na pikipiki SunLG yenye namba za usajili MC 665 DLG.

Kamanda alisema pikipiki hizo zilikuwa zikitumika kupora simu za watu nyakati za usiku na watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Watuhumiwa wengine 3 wamefikishwa mahakamani katika mtaa wa Mapolomoko kata ya Nzega Mashariki Wilayani Nzega wakiwa na vitu mbalimbali vya wizi ikiwemo runinga 5, pad za play station 9, play station 3, stendi tv 4 na waya za play station 9.

Kamanda Abwao aliongeza kuwa katika operesheni inayoendelea kufanywa na jeshi hilo wamefanikiwa pia kukamata jumla ya kete 150 na debe 5 za bangi na watuhumiwa 3 wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Alitoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuendelea kuuweka mkoa huo katika hali ya usalama.