Mwamvua Mwinyi, Pwani
Watu watatu waliojihusisha na vitendo vya ulawiti na ubakaji Mkoani Pwani wamehukumiwa kifungo cha maisha na mwingine miaka 33 jela.
Hayo yalisemwa na kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, huku ikiwa ni kampeni ya siku 16 ya kupinga Ukatili wa Kijinsia ikiendelea.
Lutumo alieleza, matukio hayo yalitokea katika kipindi cha miezi miwili ya Oktoba na Novemba mwaka huu ambapo watuhumiwa wawili walihukumiwa kwenda jela maisha kwa ulawiti na mmoja jela miaka 33 kwa ubakaji.
“Katika kipindi hicho makosa madogo madogo na makubwa ya jinai yalikuwa 80 kukiwa na watuhumiwa 100 ambapo makubwa yalikuwa 18 yalifunguliwa yakiwemo hayo ya ulawiti, ubakaji na unyanganyi wa kutumia nguvu na silaha,”alisema Lutumo.
Alieleza ,kwa upande wa makosa madogo madogo kama shambulio, wizi, kujeruhi na makosa mengine kesi 68 zilifunguliwa huku watuhumiwa 79 wakifikishwa mahakamani na walihukumiwa vifungo mbalimbali.
“Upande wa shambulio nane walihukumiwa vifungo vya miezi sita hadi 12 jela, huku watuhumiwa wa 14 matukio ya wizi walihukumiwa miezi sita hadi 12 jela,”alifafanua Lutumo.
Alielezea, makosa ya usalama barabarani kesi 12 zilitolewa hukumu mahakamani kwa kulipa faini na wengine kupewa onyo kali kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani.