Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka 10 kwa nyakati tofauti. Watuhumiwa hao ni Daudi Ochieng (37), ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi na Adon Sospiter (53), wote wakazi wa Ibisabageni wilayani Sengerema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, inadaiwa kuwa mtoto huyo amefanyiwa ukatili huo kuanzia Oktoba 2024 hadi Februari 2025.

Mtuhumiwa Adon Sospiter alikuwa akimuita mtoto huyo mara kwa mara katika chumba chake kwa kisingizio cha kuangalia tamthilia, kisha kutekeleza kitendo hicho.

Aidha, mtuhumiwa wa pili, Daudi Ochieng ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi anakosoma mtoto huyo, alitumia nafasi yake vibaya kwa kumuita chumbani kwake kwa madai ya kumfundisha masomo ya ziada, lakini ikawa tofauti.

Tukio hili lilikuja kugundulika mnamo Februari 26, 2025, majira ya saa 5 asubuhi, baada ya mama mzazi wa mtoto huyo kubaini kuwa afya ya mwanawe inazidi kudhoofika. Alimpeleka hospitalini kwa uchunguzi wa kitabibu, ambapo madaktari waligundua kuwa mtoto huyo alikuwa na michubuko sehemu za siri.

Baada ya kugundua hali hiyo, mama wa mtoto alitoa taarifa Polisi, na uchunguzi ulianza mara moja. Watuhumiwa hao walikamatwa na kwa sasa wapo mahabusu, wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Jeshi la Polisi limewataka wazazi na walezi kuwa makini na usalama wa watoto wao, hasa wanapowaachia watu wazima kwa sababu mbalimbali, ili kuepusha matukio kama haya ya unyanyasaji wa watoto.