Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imedhamiria kuishauri Serikali , kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji wa ndani (wazawa)ili waweze kumudu ushindani katika kuwekeza nchini.
Aidha kamati hiyo ,imetoa rai kwa wawekezaji kuheshimu sheria za nchi kupitia makubaliano na mikataba wanayoingia na Serikali pasipo kuipindisha.
Akizungumza baada ya kamati hiyo kutembelea Kongani ya Viwanda Modern Industrial Park (KAMAKA) iliyopo Disunyara, Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dkt. Joseph Mhagama alieleza , mazingira rafiki yatasaidia ongezeko la wawekezaji wazawa .
Anaeleza wawekezaji wa nje wamewekewa mazingira bora kwenye nchi zao, tayari wamejengewa uwezo wa kuwekeza.
“Na sisi watanzania tunapopata wawekezaji wa kitanzania wanaoibuka ni vizuri tukawajengea mazingira rafiki zaidi, :;ukiwa na mtu mfupi na mrefu ili kuwawezesha wote waweze kuona nje ya fensi ni lazima aliyemfupi akawekewa sturi amfikie aliye mrefu, kwahiyo ni lazima wawekezaji wazawa tuwawekee sturi waendane na ushindani katika uwekezaji”alisisitiza Mhagama.
Mhagama alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye sekta ya Viwanda na Uwekezaji, ambapo wawekezaji wanazidi kuchipua kama uyoga na hii ni kutokana na kazi kubwa anayoifanya kuhamasisha na kuvutia wawekezaji nje ya nchi kuja kuwekeza nchini.
“Tangu Jana tumetembelea miradi ya uwekezaji mitano na yote inatarajia kutengeneza ajira zaidi ya milioni moja,hii inaonyesha ndoto ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)ikienda kutimia kuzalisha ajira milioni nane”
Hata hivyo Mhagama ,aliahidi kubeba changamoto mbalimbali ikiwemo ya vivutio vya kikodi ,umeme, miundombinu ya barabara na maji na kwenda kuzifikisha katika kamati husika za bunge ,kujadili namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , Mipango na Uwekezaji Prof.Kitila Mkumbo , aliipongeza mwekezaji huyo mzawa Modern Industrial Park ( KAMAKA )kwa uwekezaji mkubwa ,kuonyesha njia na kuwa mfano wa kuigwa.
“Wakati tunaandaa ziara hii tulitaka mjionee sio kwamba wenye ngozi nyeupe pekee wazungu,wachina ,wahindi ndio wanawekeza nchini Ila wapo wawekezaji wenye ngozi nyeusi kama KAMAKA wamehamasika ,kuwekeza na kushika uchumi kwenye nchi yao”
Mkumbo alieleza ,kwa takwimu za TIC hadi sasa ni asilimia 61 ya wawekezaji Tanzania ni wazawa ambao wamethubutu kuunga mkono juhudi za Serikali kuinua sekta ya uwekezaji.
Awali Meneja Masoko na Mauzo wa Turnkey Real Estate (Wauzaji wa Viwanja vya Viwanda katika mradi wa Modern Industrial Park), Angela Leila Maingu alitaja changamoto wanayokabiliana nayo ni pamoja na maji na kukosekana vivutio vya kikodi, umeme kwa ajili Ujenzi wa kituo cha umeme utakaofika kwenye viwanda.
“Kwa kuanzia inahitajika kuwa na kituo cha MVA 240 (192MW) na baadae
kuongezwa hadi MVA 500 (400MW) eneo lote litakapokuwa limejengwa viwanda
vyote, mbadala ni kujenga 100MW kila mwaka kuanzia mwaka 2024 mpaka kufikia
400MW, kwa kuanzia mwekezaji anagharamia kituo cha 54MW, mwekezaji
anaomba msaada wa serikali katika kutatua changamoto ya umeme”
Mradi huo unatekelezwa katika ardhi yenye ukubwa wa hekari 1077 yenye viwanja 202, ukikamilika utatoa ajira 200,000 na za moja kwa moja 30,000, unatarajia kugharimu trilioni 3.5 kati ya fedha hizo bilioni 122.4 zitajenga miundombinu ndani ya kipindi cha miaka mitano.