Kampuni ya uchimbaji madini ya kinywe – Mahenge Resources imejitolea kuboresha sekta ya elimu katika Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro.

Kampuni hiyo kwa kushirikiana na serikali ya wilaya imechangia Sh milioni 16 kwenye harambee maalumu iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, lengo likiwa ni kuboresha majengo na miundombinu ya shule wilayani humo.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi fedha hizo, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya, ameishukuru kampuni hiyo kwa ushirikiano wake endelevu ambao imekuwa ikiutoa katika shughuli za maendeleo ya wilaya.

“Naamini kwamba mshikamano uliojengeka kati ya serikali ya wilaya yetu na kampuni hii utachangia kuleta manufaa zaidi siku zijazo kwa masilahi ya pande zote mbili,” amesema Malenya.

Malenya amesema ni jambo la kujivunia kuona wawekezaji wakubwa wanaona umuhimu wa kushiriki shughuli za maendeleo ya jamii inayowazunguka na ya taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mahenge Resources, Hekima Raymond, anasema kwamba kampuni hiyo itahakikisha inawekeza katika shughuli za maendeleo hasa ya watoto ili kuwawezesha kufikia malengo.

“Tunachofanya Mahenge Resources ni kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya watoto wetu na taifa kwa ujumla, uwekezaji chanya kwa ajili ya watu wanaotuzunguka ni jambo lenye kipaumbele cha muda wote kwenye malengo yetu ya muda mrefu, na hata katika utaratibu wetu wa kurudisha manufaa kwa jamii, maarufu kama CSR,” amesema Raymond.

Raymond anasema kiasi hicho cha fedha kilichotolewa ni sawa na asilimia 18 ya fedha zote zilizopatikana katika harambee hiyo iliyoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe.

Pamoja na kampuni hiyo kutoa kiasi hicho cha fedha, bado haijaanza hatua ya ujenzi wa mgodi wala uchimbaji wa kibiashara utakaoiingizia kampuni faida.

“Wakati tunashughulikia hatua za leseni na vibali vya uchimbaji, pamoja na kukamilisha uwezo wa kifedha kwa ajili ya uchimbaji wenyewe, tutaendelea kutilia mkazo maendeleo ya jamii inayotunzunguka sambamba na ukamilishwaji wa hatua ya utekelezaji wa sera ya fidia, uhamishaji na urasimishaji wa makazi ili kuendeleza manufaa chanya kwa jamii,” anasema Raymond.

Mahenge Resources inamiliki kwa asilimia 100 mradi mkubwa wa madini ya kinywe ulioko wilayani Ulanga, Morogoro.

Mradi huu umevuka hatua ya upembuzi yakinifu mwezi Oktoba mwaka jana, na kusajili maombi rasmi kwa ajili ya leseni za uchimbaji mwezi uliofuata.

Mradi unatambulika duniani katika sekta ya madini, ambapo mgodi huo unashika nafasi ya pili duniani kwa maana ya akiba ya madini-ghafi yote yaliyomo ardhini, na nafasi ya nne duniani kwa maana ya kiwango cha madini kinachokadiriwa kisayansi kwamba kitaweza kuchimbwa na kufaa kibiashara na kiuchumi.

Akiba hii itauwezesha mgodi kuzalisha tani 250,000 za kinywe kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 25. Mradi huo unakadiriwa kuanza na uwekezaji wa dola za Marekani milioni 125 na kutoa ajira ya watu wasiopungua 400, huku idadi ya waajiriwa wa ajira za kudumu na za mikataba ikikadiriwa kuongezeka mpaka kufikia 900 baada ya miaka mitano.