Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
SERIKALI itaendelea kuhimiza wawekezaji wa viwanda kuzalisha bidhaa bora zitakazoongeza ushindani wa Tanzania katika soko la Afrika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alieleza hayo katika ziara yake akiwa ameambatana na timu kutoka kituo cha uwekezaji (TIC) Machi 27, 2025, kwenye kiwanda cha mabati meupe, pikipiki za matairi matatu (Kinglion), na kiwanda cha kuunganisha magari (GFA) vilivyopo Kibaha, mkoani Pwani.
Alisema kuwa ,Tanzania kwa sasa inaelekea kujenga uchumi shindanishi, na kwamba ili kufikia malengo haya, ni lazima tuunge mkono juhudi za viwanda.

Kwa mujibu wa Mkumbo, serikali ina mpango wa kuhakikisha viwanda vinadumu na sio kufa, na kuwa huu ni wakati wa kuweka mkazo katika viwanda vya ndani ili kuvutia uwekezaji.
Aliongeza kusema, kiwanda cha Kinglion ni moja ya viwanda vikubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo matarajio ni kuwekeza dola za kimarekani milioni 62 (sawa na shilingi bilioni 150 za Kitanzania).
Alifafanua hadi sasa, kiwanda hicho kimeshatumia dola za kimarekani milioni 42 (sawa na shilingi bilioni 90).
“Kiwanda hiki kinazalisha mabati meupe ambayo yalikuwa yakiagizwa kutoka China na Afrika Kusini, lakini sasa tunapata nchini kwetu, haya ni mafanikio yaliyotokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza nchini,” alieleza Mkumbo.

Vilevile, Mkumbo alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, serikali itaelekeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo ya uzalishaji wa kiuchumi.
Akiwa katika kiwanda cha GFA, Mkumbo alieleza ,Serikali itakuja na muelekeo wa kisera ambao itasimamia kudhibiti uingizaji wa magari chakavu kutoka nje ya nchi.
Alieleza kwamba, sera hiyo itawezesha uzalishaji wa magari nchini, badala ya kuingiza magari ya zamani yaliyochakaa kutoka nje ya nchi.
Awali Meneja Mkuu wa kiwanda cha Kinglion, Arnold Lyimo, alieleza kiwanda hicho kimeshaajiri wafanyakazi 800 moja kwa moja, na wengine 1,200 kwa njia zisizo za moja kwa moja.
Alitaja changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na ubovu wa barabara kilomita 2 kuelekea kiwandani, uunganishaji kwenye matumizi ya bomba la gesi, na umeme usio wa uhakika.

Naye Meneja Mkuu wa kiwanda cha GFA, Ezra Mereng, alibainisha walianza na kuunganisha magari 100, lakini sasa wameshaunganisha magari zaidi ya 3,000.
“Mtaji wetu ni wa bilioni 10, tumeshatoa ajira 220, na tumeshaingia kwenye hatua ya tatu ya kuunganisha magari,” alifafanua Mereng.


