Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Poland waje nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uchumi wa bluu na madini.
Waziri Tax ameyasema hayo,wakati akihutubia mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland. Mkutano huo ambao uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Poland na Ubalozi wa Tanzania nchini humo umefanyika katika Ofisi za Taasisi ya Uwekezaji na Biashara ya Poland zilizopo jijini Warsaw.
Dkt.Tax amesema Serikali chini ya uongozi imara wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wengi wenye tija na mitaji waje kuwekeza nchini.
Ameyataja maeneo ambayo yanahitaji wawekezaji kutoka Poland na sehemu nyingine duniani kuwa ni pamoja uchimbaji madini, uchumi wa bluu, teknolojia ya habari na mawasiliano, viwanda vya sukari na nguo na miundombinu.
Amesema ili kuhakikisha wawekezaji wanaofika nchini wanafikia malengo yao, Serikali inaendelea kuboresha mifumo mbalimbali ikiwemo, kuboresha upatikanaji wa viza na vibali mbalimbali lakini pia Serikali inaboresha mikataba mbalimbali ili kuondokana na urasimu wote kwenye sekta hiyo mmuhimu ya uwekezaji.
Pia Serikali imeendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo Bandari ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wawekezaji. Huduma zingine zinazoboreshwa ni kuwa na umeme wa uhakika ambapo hadi sasa ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115 na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea nchini.
Amesema ziara yake nchini Poland pamoja na mambo mengine inalenga kukuza baiashara na uwekezaji kati ya nchini hizi mbili.
“Ninawakaribisha wafanyabaiasha na wawekezaji kutoka Poland kuja Tanzania. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia imejipanga kikamilifu kuwahudumia. Tunaendelea siku hadi siku kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini” amesema Dkt. Tax.
Amesema mbali na maboresho hayo, Tanzania ni nchi sahihi kwa wawekezaji kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo amani, miundombinu ya kisasa ya barabara, reli,bandari na soko la uhakika kupitia uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya za kikanda za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Biashara Barani Afrika (CFTA)
“Serikali imeendelea kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kuendesha biashara kwa kupitia upya sheria,kanuni na taratibu za biashara na kuzifuta zile ambazo zimethibitika kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu.” amesema.
Waziri amesema kwa kuwa nchi ya Poland imepiga hatua kubwa katika masuala mengi ikiwemo teknolojia ya usimamizi wa maji,Tanzania ingefurahi kuona wawekezaji kutoka nchi hiyo wanawekeza kwenye
sekta hiyo kwa wingi.
Amesema kuwa uchimbaji wa madini kama vile Tanzanite na mengine mengi, ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Poland wanakaribishwa kuichangamkia hapa nchini.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo,Zbigniew Sokal alitumia fursa hiyo kumweleza utayari wa Taasisi yake kushirikiana na Taasisi za Uwekezaji nchini ikiwemo TIC na ZIPA ili kujiimarisha zaidi. Alisema tayari makampuni kadhaa ya Poland yapo tayari kuwekeza nchini Tanzania.
Wakati wa mkutano huo Wawakilishi kutoka Kampuni 10 za Poland zinazojishughulisha na masuala mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa mitambo ya kilimo, uchimbaji visima virefu, usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, teknolojia mpya ya uchomeleaji vyuma na umeme wa jua waliwasilisha mada kuhusu kampuni zao.
Wakati huhuo, Mhe. Waziri Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea Mradi mkubwa wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfera uliopo katika mji wa Jozefow. Mradi huo wa aina yake pamoja na mambo mengine hususanya majitaka kutoka majumbani na kuyatibu kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji miti na maua katika mji huo. Kadhalika takangumu zingine hutayarishwa kitaalam na kuwa mbolea ya samadi kwa ajili ya mazao hayo ya miti na maua.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Rais wa Kampuni hiyo,Stanslaw Zdanowicz amesema mradi huo ambao unaendeshwa kisasa, pamoja na mambo mengine umesaidia kuwapunguzia wananchi gharama za uondoshaji majitaka majumbani kwao.
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Tax alishukuru kupata fursa ya kutembelea Kampuni hiyo na kujionea teknolojia ya hali ya juu ya usimamizi wa kisasa wa majitaka na alitumia fursa hiyo kuwakaribisha nchini kuja kuwekeza pamoja na kutembelea vivutio vya utalii vya nchini ikiwemo Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.
Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.
Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Ukuzaji Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).