Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Wawekezaji 58 kutoka nje ya nchi wameonyesha nia ya kuwekeza katika kongani ya kisasa ya Modern Industrial Park -KAMAKA Co. Ltd iliyopo Disunyara, Mlandizi Kibaha mkoani Pwani .
Licha ya nia hiyo ya wawekezaji ,Kongani hiyo inaiomba Serikali kutupia macho changamoto ya barabara kwa kiwango cha lami kutokea Mlandizi huduma ya maji na umeme wa uhakika ili kuendelea kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi ambao wakwenda kuomba kuweka ndani ya Kongani hiyo.
Hayo ameyaeleza Afisa Fedha na Masoko wa Turnkey Real Estate Tumaini Kabengula, kampuni ambayo inahusika na mauzo na masoko,na kuingia mkataba wa kutafuta wawekezaji kuwekeza viwanda kwenye viwanja 202 vilivyoko ndani ya Kongani ,kwa Waziri wa Viwanda ambae alifika kwenye eneo hilo kujionea changamoto zinazowakabili.
Ameeleza, hadi sasa wawekezaji 58 wametembelea kongani na kuonyesha nia ya kuwekeza wakitokea nchi ya India, China ,Uturuki,Sudan ya Kusini ,Afrika ya Kusini ,Rwanda ,Somalia ,Tanzania , Pakistan,Yemen ,Zambia ,Falme za kiarabu ,Misri,Uganda ,Kenya na Canada.
“Mikataba iliyopo ni kumi ya ununuzi wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, pamoja na viwanja 24 vilivyoshikiliwa vikisubiri kusainiwa kwa mikataba.” amesema.
Kabengula ameeleza, wawekezaji watatu wamekwishaanza hatua za awali za ujenzi za ujenzi zinazohusisha michakato ya vibali vya mazingira (EIA) na michoro kwa ajili ya ujenzi na wanatarajia wengine watano waliosaini mikataba wataanza hatua za ujenzi mwaka huu.
Afisa huyo amefafanua kuwa, wawekezaji wengi ambao wameshaingia mikataba ya ununuzi wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda wangependa watakapoanza ujenzi changamoto hasa ya maji na umeme iwe imetatuliwa.
Hata hivyo ameeleza miundombinu rafiki na wezeshi ndio kiungo pekee cha kuvutia wawekezaji zaidi.
“Tunaiomba Serikali kutatua hasa changamoto ya maji na umeme “amesisitiza Kabengula.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni utoaji wa vivutio vya kodi kwa kongani jirani na kutokuwepo vivutio hivyo katika kongani ya modern industrial park licha ya uwekezaji mkubwa uliofanyika na unaoendelea kufanyika kuna haribu ushindani wa haki wa kibiashara.
“Baadhi ya wawekezaji wanaamua kutokuchukua viwanja ndani ya Kongani kwa sababu ya kukosekana kwa vivutio vya kikodi kama ambavyo vinapatikana katika kongani jirani.” ametaja.
Kabengula ameeleza, wawekezaji wengi wanakiri kuvutiwa na uzuri wa kongani ya modern industrial park lakini wanakwazwa na kutokuwepo kwa vivutio hivyo vya kikodi kama ambavyo vinapatikana kwenye kongani jirani.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameeleza ,kuhusu Changamoto ya maji alishaongea na waziri wa maji Jumaa Aweso na ameahidi kufika kwenye kongani hiyo kujionea uhalisia wa tatizo.
“Tunajivunia kuifungua Mkoa wa Pwani kwa ujenzi wa viwanda ,tuna kongani tatu na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Kongani 23 ,ambapo tunaishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuvutia wawekezaji na kuboresha na kuweka mazingira wezeshi hatua kwa hatua ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili “ameeleza Kunenge.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji alieleza miundombinu wezeshi ni suala muhimu kwenye uwekezaji.
Kuhusu masuala ya kikodi alisema, watafuatilia ili kuona namna ya kuliweka sawa tatizo hilo.
“Ninashauri upande huo wa masoko ,waongeze taarifa ambazo hazipo kwenye taarifa ya mradi,wekeni wazi kila kitu hatua itakayosaidia ili ziwafikie wawekezaji kwa urahisi”ameeleza Kijaji.
Nae Mkurugenzi Mtendaji, Mkandarasi Mkuu Afriq Engineering and Construction Co.Ltd mhandisi Charles Bilinga , alisema wamefikia asilimia 93 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ambao utakamilika mwezi Februari mwaka huu .
Kongani ya KAMAKA ni mradi ambao ukikamilika utagharimu trilioni 3.5 kati ya fedha hizo bilioni 122.4 zitajenga miundombinu ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo hadi sasa sh .bilioni 35 zimetumika kwa ujenzi wa miundombinu na gharama zinazohusiana na uwekezaji huo.