Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa kushirikiana na viongozi waadilifu katika Jiji la Dar es Salaam, wamelikomboa eneo la wazi lililovamiwa na mfanyabiashara na kujengwa jengo la biashara.
Gazeti la JAMHURI lilikuwa la kwanza kuandika habari ndefu Novemba, mwaka jana, iliyohusu uvamizi huo katika Mtaa wa Samora.
Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene; na wajumbe kadhaa wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, walishuhudia kubomolewa kwa jengo la mvamizi huyo.
Mamia ya wananchi walioshuhudia kazi hiyo hawakuficha hisia zao. Walionesha furaha ya kipekee kwa uamuzi wa Serikali katika kuhakikisha kuwa eneo hilo linaendelea kuwa wazi kwa manufaa ya wananchi wote.
Tunachukua fursa hii kuipongeza Serikali, na hasa watendaji ambao wanatambua na kuthamini utunzaji wa maeneo ya wazi.
Mara zote Serikali imekuwa ikitoa makaripio na vitisho visivyokuwa na utekelezaji. Kwa kuutambua udhaifu wa Serikali, wavamizi wameendelea kutamba kana kwamba nchi hii haina viongozi au watendaji wanaopaswa kusimamia sheria.
Maeneo mengi katika miji yote nchini yamevamiwa na watu wenye ukwasi. Wananchi wamekoseshwa sehemu za kupumzikia. Si hivyo tu, bali ujenzi wa majengo bila kuzingatia maeneo ya wazi yenye miti na maua ni mambo ambayo kisayansi yana athari kwa afya za watu.
Wananchi wameshuhudia maeneo mengi ya wazi, tena yakiwamo ya viwanja vya michezo, yakivamiwa. Kuna watendaji katika halmashauri na hata ndani ya Serikali Kuu ambao hugawa maeneo hayo; vitendo vinavyoashiria rushwa.
Uamuzi huu uliosimamiwa na Simbachawene tunaamini hautaishia Mtaa wa Samora pekee, bali utaonekana katika majiji, miji na vijiji vyote nchini.
Maeneo ya wazi ni haki ya wananchi. Yanasaidia kuboresha mandhari ya sehemu husika, lakini pia yanasaidia kuchuja hali ya hewa kutokana na uchafuzi unaotokana na shughuli za kibinadamu, magari na viwanda.
Kwa kuwa mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, matukio ya uvamizi wa maeneo ya wazi yanaweza kuwa mengi kwa sababu kuna wanasiasa na watendaji wanaojipendekeza kwa wafanyabiashara.
Serikali ina wajibu wa kuonesha kuwa sheria za nchi hazina likizo. Wale waliojenga maeneo ya wazi, yakiwamo ya baharini na katika viwanja vya michezo, hawana budi kushughulikiwa kama alivyoshughulikiwa huyu wa Mtaa wa Samora.
Pamoja na dosari kadha wa kadha za utendaji kazi serikalini, wananchi kwa umoja wetu tunayo sababu ya kuwapongeza viongozi na watendaji waliothubutu walau kumshikisha adabu mvamizi huyu wa Mtaa wa Samora. Hongera sana.