Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Kiteto
SERIKALI imetoa siku saba kwa wavamizi wanaofanya shuguli za kilimo kwenye maeneo ya kongani za malisho ya mifugo zilizotegwa kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi za vijiji wilayani Kiteto mkoani Manyara wawe wameshaondoka bila kujali kama ni wafugaji au ni wakulima.
Aidha, watakaokaidi agizo hilo baada ya muda huo itaendeshwa oparesheni ya kuwaondoa kwa nguvu watu wote waliovamia maeneo hayo na kuwafikisha mahakamani.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi msaidizi wa uendelezaji wa maeneo ya malisho Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Gabriel Bura kwenye kikao cha viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai (malaigwanani) na Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kilichofanyika wilayani hapa.
Amesema maeneo hayo ya kongani za malisho kwa ajili ya mifugo yalitengwa kwa mujibu wa sheria hivyo watu wote ambao wamevamia hivi sasa na kufanya shughuli nyingine tofauti na ufugaji wanatakiwa kuondoka mara moja.
“Siku saba zunatisha kabisa kwa watu wote kuwa wameondoka kwenye maeneo hayo, mnapaswa kujua kuwa maeneo yale yametengwa kwa ajili ya ufugaji tuu na siyo kitu kingine na kwa yule ambaye atafanya shughuli nyingine zaidi ya ufugaji anavunja sheria;
Mpango wa matumizi bora ya ardhi nchini umefanyika kwa asilimia 45 na maeneo ambayo yametekeleza zaidi ni Manyara na Arusha hapa kwenu mpango umefanyika ni jukumu leo kuzilinda hizi kongani za malisho, sheria ya malisho inakataza maeneo haya mtu kulima, kujenga au kuchimba madini” anasisitiza
Amesema katika kipindi hicho cha siku saba watu wote wanapaswa kuondoka bila kujali kama ni wafugaji au ni wakulima.
“Nitoe wiki moja viongozi wote wanaofanya shughuli yoyote ambayo haihusiki kisheria watoke kwani wote ni wavamizi bila kujali walipotoka lakini pia niwaombe nyinyi wafugaji kuwa walinzi wa maeneo haya kwani nyinyi ndiyo umekuwa mnawakaribisha watu kwenye hizi kongani za malisho”amesema
Mwenyekiti wa Malaigwanani wilaya ya Kiteto Laigwanani Emmanuel Sinogoro, ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wafugaji waliokaidi agizo la kutoka kwenye maeneo ya nyanda za malisho.
Amesema hali hiyo itasaidia kuondokana na kero ya maeneo ya malisho katika wilaya hiyo inayosababisha migogoro ya muda mrefu baina ya wafugaji na wakulima.
Sinogoro, amesema moja ya sababu inayochangia maeneo ya malisho kuvamiwa inatokana na wafugaji wenyewe kukaribisha watu kwa ajili ya shughuli za kilimo kwenye kongani za malisho.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Kusundwa Wamalwa, amesema mara baada ya kipindi hicho cha siku saba kupita wataziomba mamlaka husika kuchukua hatua kali .
“Ili jamii ya wafugaji nchini ipate mafanikio inapaswa kushirikiana kwa kila jambo ikiwemo kupinga vitendo vya unyanyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali na askari wa mapori ya akiba nchini, ” amesisitiza