Nimesoma tamko la serikali linalohusu uamuzi ‘mgumu’ ilioamua kuuchukua dhidi ya wavamizi wa hifadhi mkoani Kigoma.
Tathmini iliyofanyika mkoani humo imeonyesha hifadhi za misitu na mapori ya akiba yamevamiwa kwa shughuli za kilimo, ufugaji, ukataji miti na baadhi ya vijiji vimesajiliwa ndani ya maeneo hayo.
Uvamizi huu umesababisha athari nyingi zikiwamo za kupotea kwa uoto wa asili na viumbe hai, wakiwamo wanyamapori, kuharibiwa kwa vyanzo vya maji (mfano Mto Malagarasi), mmomonyoko wa ardhi na kusababisha mito na mabwawa kujaa udongo, magonjwa ya binadamu na mifugo, ongezeko la ujangili wa wanyamapori, uvunaji haramu wa misitu na kuongezeka kwa tishio la kiusalama kutokana na wakimbizi na wahamiaji haramu mkoani Kigoma na kwingineko nchini.
Kutokana na baa hilo, mawaziri sita wamekutana na kutoa msimamo ili kukabiliana na hali hiyo mbaya.
Miongoni mwa yaliyokubaliwa ni kwa serikali kuendesha operesheni kubwa kuondoa uvamizi wa wakulima, wafugaji na watu wengine wanaofanya shughuli zisizo halali kwenye misitu na mapori yaliyohifadhiwa kisheria, zikiwemo hifadhi za misitu ya serikali kuu, hifadhi za misitu za halmashauri za wilaya na vijiji.
Wavamizi wametakiwa waondoke mara moja kwa hiari kabla ya kuwaondoa kwa lazima. Tumeambiwa operesheni hiyo itafanyika wakati wowote ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hii.
Wahamiaji haramu wametangaziwa kiama kwa kuwa wanachangia katika uharibifu wa misitu na mapori. Wametakiwa waondoke nchini mara moja. Haya ni baadhi tu ya maazimio ambayo utekelezaji wake, kama tulivyohakikishiwa, utaanza Januari hii.
Ndugu zangu, yaliyotokea Kigoma yanatokea nchini kote. Hali ya mazingira katika nchi yetu kwa sasa ni mbaya mno. Kuna uharibifu mkubwa sana wa misitu na rasilimali asilia, kuanzia misituni hadi ndani ya maji (bahari, mito na maziwa).
Kigoma ni tone tu katika bahari kubwa ya matatizo yanayoikabili sekta nzima ya uhifadhi nchini kote. Hili si suala la Kigoma pekee, bali ni la nchi nzima.
Tumeyaharibu mazingira kwa visingizio vingi vya uongo. Kwa mfano, tunazungumzia ongezeko la watu kama miongoni mwa sababu za kuwapo hali hii. Hii si kweli hata kidogo. Kama wingi wa watu ungekuwa hoja, basi leo China isingesalia na msitu au mazao ya baharini. Tumefika hapa kwa sababu ya kukosa uzalendo na Tanzania kuonekana kama nchi isiyokuwa na mwenyewe.
Sina hakika, lakini naweza kupiga ramli kubaini nani ameagiza haya ya Kigoma yafanyike. Kama si Makamu wa Rais, basi atakuwa Rais mwenyewe. Tunao viongozi wengi wasiothubutu kufanya lolote la maana pasipo kusukumwa. Haiwezekani misitu imalizwe katika kijiji, wilaya na mkoani ilhali ngazi zote hizo zikiwa na viongozi.
Hata pale walipojaribu kufanya mikutano, walicholenga ni mambo ya siasa na zimamoto ya miradi kama ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kadhalika. Ni wachache mno wanaodiriki kuwa na vipaumbele kama kwenye upande huu wa kulinda maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa kisheria.
Hili suala la wahamiaji haramu wala tusilionee aibu. Leo tunao watu ambao ukithubutu kuwazungumzia wahamiaji haramu, basi wewe unaonekana mbaguzi. Tukubali kuwa Tanzania ni shamba la bibi, tena aliyekwisha kufariki dunia kitambo! Ni Tanzania pekee ambako mgeni yeyote awaye anaweza kuingia na kufanya lolote analotaka.
Sijafanya utafiti, lakini nadiriki kuamini kuwa maovu mengi nchini mwetu yanachangiwa na wageni. Tuliona tatizo la ujambazi wa kutumia silaha namna wageni kutoka mataifa jirani walivyoshiriki kuwaua na kuwapora Watanzania.
Kwenye makala yangu moja nimepata kuhoji ni Watanzania gani hawa walioamua kuteketeza rasilimali za nchi bila huruma? Nilijaribu kueleza kuwa kama mtu anajua Tanzania si kwao hawezi kuwa na huruma na chochote.
Tunaambiwa mkoani Kigoma kuna wahamiaji haramu wameingia misituni na kuanzisha vijiji. Hili si jambo rahisi. Ni lazima liwe na mtandao. Hawa wanayafanya haya kwa sababu kwenye uongozi wa vijiji kuna wageni wengi wa mataifa jirani waliojipenyeza. Hao ndio wanaotumika kuwakaribisha wenzao. Haya hayako Kigoma tu, bali tumeyaona hata wilayani Ngorongoro. Zipo taarifa zisizotiliwa shaka kuwa uongozi wa vijiji, kata na wilaya una wageni wengi. Viongozi waandamizi wa CCM Wilaya ya Ngorongoro wamo Wakenya wengi. Wanajulikana. Hawa ni miungu-watu. Wanawakaribisha wenzao na kujijengea himaya.
Pamoja na kupinga hatua ya wakoloni ya kuigawa Afrika, kwa hali tuliyonayo sasa hatuwezi kuipuuza mipaka hiyo. Hatuna budi tuikubali. Hili haliko kwenye nchi tu, bali tunaliona hata katika familia zetu. Watoto wanagawiwa ardhi huhakikisha kila mmoja analinda sehemu yake hata kama wote wametoka tumbo moja. Haiwezekani mtoto mmoja akaondoka eneo lake na kwenda la mwenzake, akajimilikisha haki za hilo eneo kwa kigezo tu kuwa wote ni watoto wa baba au mama mmoja.
Vivyo hivyo, majirani zetu wana nchi yao. Wana ardhi yao. Wale wanaoona Tanzania ni mahali panapowafaa kuja kuishi, wafuate taratibu. Wapokewe na wawe tayari kuheshimu sheria za nchi yetu.
Watanzania wengi ni watiifu wa rasilimali za nchi yao, kwa sababu wanajua hapa ndipo kwao. Wahamiaji haramu wanajua wanaweza kuua wanyamapori wote wakawamaliza, wanaweza kuvua kwa kutumia mabomu, wanaweza kukata misitu yote wakaimaliza; na watakapoona nchi imebaki jangwa au imekwisha kufilisika, watarejea kwao kwenye asili yao. Haya mambo yapo.
Kuna genge kubwa mno la waendesha pikipiki wanaomaliza misitu katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa sehemu kubwa ya genge hili ni wageni kutoka nchi jirani. Wanaingia misituni ndani kuchoma na kulangua mkaa. Bahati mbaya wanapita kwenye vizuizi vyote bila kuulizwa. Nchi inaangamia tukiwa tunatazama!
Serikali imetangaza kuwaondoa wahamiaji haramu Kigoma na kwingineko nchini. Kwa hali ilivyo hili halitawezekana. Tutarajie kusikia kelele nyingi kutoka kwa ‘manabii’ wa utetezi wa haki za binadamu. Kwao, mhamiaji haramu ana haki ya kufanya mabaya kadiri anavyotaka, lakini kumdhibiti au kumwondoa nchini ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Idadi ya ‘Watanzania’ inaongezeka mno. Takwimu zinatisha. Haihitaji utafiti wa kuumiza kichwa kutambua kuwa miongoni mwa hawa wanaoitwa Watanzania kuna wahamiaji haramu wengi sana. Bahati mbaya Tanzania ndipo mahali ambako unaweza kuishi na mtu bila kumuuliza ametoka wapi na ana uhalali gani wa kuishi nchini. Tumejifunga akili kwa kuamini kuwa kumhoji mtu anayetiliwa shaka uhalali wake ni kuendekeza ukabila! Hii si kweli hata kidogo.
Wahamiaji haramu wana athari kubwa mno kwa maendeleo ya nchi. Ukiweka kando vitendo vya uhalifu wanavyofanya, wahamiaji haramu wanapunguza wigo wa Watanzania wenye sifa za uraia kupata huduma muhimu za kijamii.
Hao hao wanajipenyeza kwenye afya na elimu na kuliongezea taifa mzigo wa kugharimia huduma hizo. Kwa maneno mengine ni kama tunajaza maji kwenye chombo kilichotoboka. Hayatajaa kamwe.
Tumetangaza elimu bure, tunadhani nani hatapenda kuingia nchini akazaa watoto ili mwishowe wapate hiyo elimu bure? Tumeona wangapi waliosomeshwa na nchi hii wakijulikana kuwa ni Watanzania lakini leo wako makwao wakiwa na nyadhifa kubwa?
Nayasema haya si kwa sababu nawachukia wageni, la hasha! Huo ndio ukweli wenyewe. Nchi hii tutapiga ‘mark time’ kweli kweli kimaendeleo kama tutaendelea kuwa chumba kisichokuwa na mlango. Tuwapokee wageni (kama ilivyo ada yetu) lakini tuhakikishe wanaheshimu sheria za nchi.
Uvamizi na uteketezaji wa misitu ndilo janga kubwa pengine kuliko majanga mengine tunayofikiria. Misituni ndimo tunapopata dawa. Misitu ndiyo inatuletea mvua. Misitu ndiyo chanzo cha mvua zitakazojaza mabwawa kama lile ya Stiegler’s Gorge kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Misitu ndiyo inayochangia asilimia 24 za pato la taifa linaloonekana moja kwa moja. Misitu ndiyo inayowezesha kilimo na kutupatia chakula na ziada tukauza. Misitu ndiyo chanzo cha hewa safi tunayoitumia. Misitu ni kila kitu katika uhai wa mwanadamu. Kunapotokea genge la watu – wawe wa ndani au nje ya nchi – la kuiharibu misitu, hilo genge lazima lishughulikiwe kwa kila aina ya silaha tuliyonayo.
Mwisho, wale manabii wa utetezi watakaojitokeza kukwamisha operesheni hii wasiachwe watambe maana utetezi wao ni mauti kwa taifa letu. Wavamizi hawa si wa kuchekewa. Hii ni vita. Tuipigane kwa umoja wetu.