Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewaagiza waajiri wa taasisi za umma kuwarudisha kazini watumishi wanaoshinda mashauri ya rufaa za kinidhamu kadiri ya maelekezo yaliyotoka kwenye Tume ya Utumishi wa Umma.
Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Deus Sangu ametoa agizo hilo akiwa Morogoro katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi kuhusu mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kieletroniki wa kushughulikia rufaa na malalamiko na Ukaguzi wa Usimamzi wa Masuala ya Rasilimali Watu (PSCMIS) yaliyoandaliwa na tume hiyo.
Sangu amesema kuna baadhi ya viongozi wa taasisi za umma ambazo majina yake ameyahifadhi kuwa wamekaindi maelekezo ya tume hiyo na itabidi wachukuliwe hatua zinazostahiki.
Naibu Waziri amesema kwenye ziara zake aliyoifanya mikoani amekutana na watumishi wakiwa na wana barua halali zilizowaarejesha kazini kutoka Tume ya Utumishi wa Umma.
“Kuna baadhi ya waajiri hawajawarudisha watumishi kazini ,watumishi hao wameandikiwa barua na hawajawarudisha na huu ni mwaka wanne sitazitaja taasisi hizo lakini zipo kama tano wamewagomea watumishi wale,” amesema Sangu.
Kutokana na kukaidi huko, Naibu Waziri ametoa maelekezo kwao ya kwamba wahakikishe hao watumishi wao wanawarudisha kadiri ya maelekezo yaliyotoka kwenye Tume ya Utumishi wa Umma.
“Kama wanashauri la kinidhamu waanze upya na wasipofanya hivyo, Ofisi ya Rais ,Utumishi itabidi tuanze kuchukua hatua stahiki,” ameonya Naibu Waziri Sangu.
Naibu Waziri amesema watumishi hawa walikata rufaa kwenye tume , na tume ikasema rudini mashauri yakaanze upya, lakini waajiri wamegoma wanawazungusha mwaka wa tatu, wengine mwaka wa pili.
Sangu amesema taasisi hizo majina yake ataipatia Tume ya Utumishi wa Umma kupitia kwa Katibu wake ili awasiliane nao na endapo watashindwa kutekeleza jambo hilo, Ofisi ya Rais, Utumishi ijulishwe ambayo itawafundisha namna ya kutekeleza.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa Tume hiyo, John Mbisso amesema ni matarajio ya Tume kuwa baada ya mafunzo haya washiriki watakuwa wamepata ufahamu wa namna ya kuwasilisha Tume vielelezo vya rufaa na malalamiko na taarifa za kiutumishi za robo ya mwaka.
Mbisso amesema washiriki hao watakuwa wameongeza kiwango cha uelewa wa sheria katika usimamizi wa utumishi wa umma .
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image-31-1024x570.png)