Serikali imewakumbusha watumishi wa umma nchini kutotumika kisiasa, badala yake watimize majukumu yao kikamilifu.
Maelezo hayo kwa watumishi hao wa serikali yametolewa hivi karibuni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akiwa wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani.
Katika ziara yake hiyo, naibu waziri huyo licha ya kukutana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwao, aliwatembelea wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini wilayani humo ili kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
Dk. Mwanjelwa alisema serikali inahitaji utaalamu wa watumishi wa umma katika kujenga tasnia imara ya utumishi wa umma utakaoziwezesha taasisi zote za umma nchini kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa hatarajii kumuona mtumishi wa umma akijihusisha na harakati za kisiasa na kukwamisha azima ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi kikamilifu.
Aliwataka makatibu tawala wa mikoa kuwasimamia kikamilifu wakurugenzi watendaji wa halmashauri ili kujenga ushirikiano wa kiutendaji kati ya makatibu tawala wa wilaya na wakuu wa wilaya, kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa umma.
Dk. Mwanjelwa alihimiza ushirikiano wa watendaji hao ili kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za serikali kwa ujumla, na kuongeza kuwa serikali iliyopo madarakani ni moja tu inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, na kuhoji; inakuwaje makatibu tawala wa wilaya wasiarifiwe masuala yanayoendelea katika halmashauri?
“Kuanzia sasa barua yoyote ya kiutendaji itakayotoka mkoani kuelekezwa kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri ni lazima nakala ya barua hiyo ielekezwe pia kwa makatibu tawala wa wilaya ili wafahamu kinachoendelea na kumuarifu mkuu wa wilaya kufanya ufuatiliaji wa utendaji kazi,” alisisitiza Dk. Mwanjelwa.
Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 na kisha kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa kwanza ndani ya mfumo huo mwaka 1995, watumishi wa umma wamekuwa wakitakiwa kutojihusisha na masuala ya siasa moja kwa moja, ingawa ni ruksa kwao kuchagua viongozi wa kisiasa kwa njia ya kupiga kura.
Kanuni za utumishi wa umma nchini sambamba na sheria ya utumishi wa umma zimekuwa zikizingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayoweka bayana kuhusu haki ya kuchagua na kuchaguliwa kwa Mtanzania mwenye sifa husika.