Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa baraza hilo lililofanyika mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati), akizungumza na wajumbe wa baraza hilo pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi zilizo chini ya sekta hiyo katika kikao cha baraza la wafanyakazi, mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Bi. Elizabeth Tagora akiwasilisha rasimu ya bajeti na mpango wa utekelezaji wa sekta hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi, mkoani Morogoro.
Baadhi ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) wakifuatilia maelekezo ya mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika mkoani Morogoro.
Katibu wa baraza la wafanyakazi (Sekta ya Ujenzi), Bw. Vendeline Massawe, akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa baraza kwa kumchagua kushika nafasi hiyo mara baada ya katibu wa zamani kupata uhamisho, Mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati), pamoja na viongozi wengine wakishiriki kuimba nyimbo ya ‘Solidarity forever’ kuonyesha mshikamano katika utendaji kazi wakati wa Kikao cha baraza la wafanyakazi, Mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi mara baada ya kufungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika Mkoani Morogoro.
 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi kujitathimini yale waliyoazimia kutekeleza kwa mwaka wa Fedha 2017/18 kama yamefikia lengo ili kuweza kusaidia kuboresha utendaji na kutafutia ufumbuzi masuala ambayo yanakwamisha ufanisi wa kazi na kuwezesha mazingira wezeshi kwa wafanyakazi.
Prof. Mbarawa amesema hayo mkoani Morogoro, wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi ambapo pamoja na mambo mengime amesisitiza umuhimu wa baraza hilo katika kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi wenye tija, staha na upendo.
“Ni matarajio yangu kuwa kila mjumbe kwa nafasi aliyonayo katika baraza hili atatumia fursa hii kutoa michango ya mawazo ili iweze kuwa mwongozo mzuri wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, ametoa wito kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa Wizara inashiriki kikamilifu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwajengea watanzania miundombinu bora na imara ili kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda na hivyo kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya kuifanya nchi yetu iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Profesa Mbarawa, amewataka wajumbe hao kujadili kwa kina Rasimu ya Bajeti na Mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2018/19 ili kuweza kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Waziri Prof. Mbarawa, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi za Umma kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Ameongeza majukumu mengine kuwa ni kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi; kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi; maslahi ya Wanyakazi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.