Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dodoma

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Hamza Johari amewataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma ili waweze kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezungumza hayo wakati akifungua Mafunzo elekezi kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yaliyofanyika tarehe 13 Machi, 2025 Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati akifungua Mafunzo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Watumishi umuhimu wa utoaji wa huduma za ushauri wa kisheria, ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ambayo imetolewa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Tunatakiwa kuendelea kuzingatia Sheria na Kanuni tulizojiwekea ili tuweze kutoa huduma bora na stahiki kwa wananchi. amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Aidha, Johari amewahimiza Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kusoma Mpango Kazi wa Ofisi ili kuwianisha Mipango na Programu mbalimbali za Maendeleo ya Taifa ikiwemo kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoelekea kuisha na kuangalia namna bora ya kutekeleza malengo yaliyoainishwa katika Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tunapaswa tushirikiane kwa pamoja kuitekeleza kwa vitendo Dira ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tuendane na uelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050”.amesema Johari

Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa Watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kuwahudumia wadau wote wanaohitaji huduma katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia misingi ya taaluma ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kujenga taswira nzuri ya Ofisi.

Awali, akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Onorius Njole aliwataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa watulivu wakati wote wa mafunzo hayo kwani mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuboresha utendaji kazi wao.