Kilichowakuta watumishi wa umma waliokuwa na mtindo wa kusafiri nje ya nchi mara kwa mara sasa kimewakumba pia watumishi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi.
Ruhusa ya watumishi wa Tamisemi kusafiri kwa ajili ya kuhudhuria mikutano, warsha, makongamano na semina imefutwa kupitia waraka uliotolewa Februari 7, mwaka huu na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Nyamhanga.
Nyamhanga anasema ofisi yake imelazimika kufuta vibali vya safari hizo kwa sababu mialiko hiyo imesababisha watumishi wengi wa Tamisemi kutokaa katika vituo vyao vya kazi na badala yake kutumia muda mwingi wakihudhuria shughuli zinazotokana na mialiko hiyo.
Waraka huo unawataka watumishi wote wa Tamisemi kuhakikisha wanabakia katika vituo vyao vya kazi na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Pamoja na kufuta vibali vya safari hizo kwa siku zijazo, pia kupitia waraka huo, Nyamhanga ameeleza kuwa ofisi yake imefuta vibali vyote vilivyokuwa vimetolewa kwa watumishi kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi lakini bado hawajasafiri.
Katika waraka huo ambao nakala yake imepelekwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Nyamhanga anasema kuwa Ofisi ya Rais, Tamisemi imekuwa ikipokea mialiko mingi kwa viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka wizara, idara zinazojitegemea, taasisi za umma na taasisi binafsi kwa ajili ya kuhudhuria mikutano, mafunzo, warsha, semina na makongamano.
Nyamhanga anasema pamoja na kutambua umuhimu wa mialiko hiyo, lakini katika siku za hivi karibuni imekuwa mingi sana kiasi cha kusababisha viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia muda mwingi nje ya vituo vyao vya kazi wakihudhuria mialiko hiyo.
“Jambo hilo limeathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa majukumu yao,” anasema Nyamhanga.
Kusitishwa kwa vibali hivyo kunalenga kuwapatia muda viongozi na watumishi hao kuhakikisha wanasimamia kikamilifu shughuli zinazofanywa na serikali kwa wakati huu.
Kwa mujibu wa Nyamhanga hivi sasa serikali inatekeleza shughuli nyingi katika ngazi zote nchini ikiwemo miradi ya kimkakati, miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma mbalimbali.
Imetaja shughuli nyingine ambazo zinatekelezwa na serikali hivi sasa katika maeneo yote nchini kuwa ni ujenzi wa hospitali za halmashauri na vituo vya afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, maafa yanayosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kuanza kwa msimu wa kilimo.
“Shughuli hizi zinahitaji usimamizi wa karibu wa viongozi na watumishi wa serikali katika ngazi ya mkoa, wilaya na mamlaka za Serikali za Mitaa,” anabainisha Nyamhanga.
Hivyo, Nyamhanga anasema katika waraka huo ulioelekezwa kwa makatibu Tawala wa mikoa yote Tanzania Bara kutokana na kuwepo kwa shughuli hizo, Ofisi ya Rais – Tamisemi imesitisha utoaji wa vibali kwa ajili ya kuhudhuria mikutano, mafunzo, semina, warsha na makongamano kwa viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na mamlaka za Serikali za Mitaa.
Nyamhanga hakutoa muda wa usitishaji huo.
“Aidha, kwa viongozi na watumishi ambao tayari wamepata vibali vya kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi kwa sababu zilizotajwa hapo juu, ninapenda kuwataarifu kuwa vibali hivyo vimefutwa,” anasema Nyamhanga.
Katazo hili linakuja miaka minne baada ya Rais Dk. John Magufuli kupiga marufuku safari za nje ya nchi kwa watumishi wa umma kwa lengo la kupunguza matumizi ya serikali.
Rais alitoa agizo hilo baada ya kikao baina yake na makatibu wa wizara kilichofanyika Ikulu siku chache baada ya kuapishwa, akisema ofisi yake ndiyo itakayotoa kibali kwa watumishi ambao wana safari za nje.
Akifafanua baadaye kuhusiana na agizo hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, alitoa mwongozo ulioweka masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi watatakiwa kutimiza ili wapewe kibali.
Kwa mujibu wa muongozo huo, sharti la kwanza linalotakiwa kuzingatiwa na watumishi hao ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Lakini kabla ombi hilo halijafikishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, linapaswa kupitia kwa Msajili wa Hazina. Lengo hapa ni kuangalia faida za kiuchumi zitakazopatikana mtumishi huyo atakaposafiri dhidi ya gharama za safari husika.
Sharti jingine katika mwongozo huo ni kabla ya kutuma ombi hilo, mwombaji au mtendaji mkuu wa shirika au taasisi, lipime maombi ya safari husika ili kuona kama yana tija na yana umuhimu wa kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, hilo linapaswa kufanyika kabla ombi hilo halijapelekwa kwa Msajili wa Hazina.
Sharti jingine ambalo lina vipengele vitano ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa wakati wa kuwasilisha hoja ya safari, ni kueleza nini chanzo cha safari husika, faida ya safari hiyo, umuhimu wake na madhara yatakayotokana na safari kutofanyika.
Pia katika sharti hilo kuna kipengele kuhusiana na gharama za safari, likiweka masharti yanayomtaka mwombaji aainishe gharama ya tiketi ya ndege, posho za safari husika, mlipaji wa gharama za safari na uwezo wa taasisi kifedha.
Aidha, masharti hayo pia yanamtaka mwombaji aeleze manufaa ya safari hiyo kwa taasisi na taifa.
Agizo hilo la Rais Magufuli limepunguza safari za watumishi wa umma nje ya nchi kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa ni nadra kusikia waziri akiwa nje ya nchi, kwani safari wanazozifanya ni zile ambazo zimeruhusiwa na Ofisi ya Rais mwenyewe.
Kwa kuonyesha mfano, Rais Magufuli mwenyewe amesafiri mara chache sana nje ya nchi katika kipindi cha miaka minne aliyokuwa madarakani na katika safari hizo hakuna aliyoifanya nje ya Bara la Afrika.