Katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Juni 1 hadi Julai 8, 2024 Jeshi la Polisi wamefanya oparesheni dhidi ya wahalifu na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 179 wa makosa mbalimbali na kuwafikisha mahakamani huku wengine upelelezi wa kesi zao bado unaendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea na oparesheni, doria na misako katika maeneo yote ya mkoa huo ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa Salama.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Julai 18,2024 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,Naibu Kamishina wa Polisi (DCP) Wilbroad Mutafungwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

“Kupitia oparesheni hiyo tumefanikiwa kumkamata mtuhumiwa Lupande Ng’wandu (43) mkulima na mkazi wa Kasela kwa kosa la mauaji ya Mwajuma Yugele yaliyotokea Julai 13,2024 majira ya saa 11:00 alfajiri katika Kijiji cha Kasela Kata ya Nyakalilo Wilaya ya Sengerema aliyeuwawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani upande wa kulia ambapo chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi”, amesema Mutafungwa.

Ameeleza kuwa baada ya upelelezi wa kina kufanyika Julai 16, 2024 majira ya saa mbili asubuhi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji hayo Lupande Ng’wandu akiwa amejificha katika Kijiji cha Busango Kata ya Segese Wilaya ya Masalala Mkoa wa Shinyanga.

Aidha, Kamanda Mutafungwa amesema katika misako hiyo watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na makundi ya wahalifu na vielelezo vyao.

“Tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 39 wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi kg 14.2,watuhumiwa 63 wakiwa na lita 134.5 za pombe haramu ya moshi na mitambo mitano ya kutengenezea pombe hiyo, watuhumiwa 63 wakiwa na vifaa vya kupigia ramli chonganishi na watuhumiwa wawili wakiwa na injector pump mtambo unaotumika kutengenezea barabara sanjari na vielelezo mbalimbali zikiwemo deki tatu,pikipiki tano aina ya Tvs,Sunlg,Bajaji na Kinglioni mbili mali zinazozaniwa kuwa ni za wizi”, amesema Mutafungwa.

Amesema kati ya watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni pamoja na aliekuwa mchungaji wa Kanisa la T.A.G Kata ya Buhongwa George Ernest kwa tuhuma za mauaji ya Majuto Seif yaliyotokea Juni 28, 2024 katika Wilaya ya Ilemela.