Na Abel Paul, Jeshi la Polisi, Arusha

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema hali ya Ulinzi na usalama kwa kipindi cha kuanzia mwezi Octoba, 2024 hadi sasa ni shwari huku likibaiinisha kuwa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa ubakaji na usafirishaji dawa za kulevya ambapo watuhumiwa wawili wamefungwa Maisha na wengine sita wamehukumiwa miaka 30 kila mmoja na mmoja miaka 18.

Akitoa taarifa hiyo kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema kuwa Kupitia operesheni dhidi ya dawa za kulevya walifanikiwa kukamata Watuhumiwa 40 wakiwa na Mirungi Kilogramu 646.62, na Watuhumiwa 25 wakiwa na Bhangi kilogramu 178.5 pamoja na kuteketeza hekari 16 za bhangi.

SACP Masejo ameongeza kuwa baada ya kufikishwa Mahakamani, watuhumiwa 03 wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa makosa ya kusafirisha bhangi na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.

Aidha kwa upande wa makosa ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, amebainisha kuwa wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 51 na kuwafikisha Mahakamani. ambapo 20 walikamatwa kwa tuhuma za kubaka na mtuhumiwa 01 alihukumia kifungo cha Maisha na watuhumiwa 02 walihukumiwa kwenda jela miaka 30 na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.

Vilevile Kamanda Masejo ameendelea kufafanua kuwa watuhumiwa wengine 31 walikamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa tuhuma za Ulawiti ambapo kati yao Watuhumiwa 02 wamehukumiwa vifungo vya maisha jela na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.

Sambamba na hayo ameweka wazi kuwa mtuhumiwa 01 wa kosa la udhalilishaji wa kingono alikamatwa ambapo baada ya kufikishwa Mahakamani alihukumiwa kwenda jela miaka 18.

Halikadhalika kwa kipindi hicho walifanikiwa kukamata Watuhumiwa 35 wakiwa na pombe haramu ya Moshi lita 128 na mitambo 02 ya kutengenezea pombe hiyo ambapo watuhumiwa wote tayari wameshafikishwa Mahakamani kwa taratibu za kisheria.

Pia katika opereseheni hiyo, tulifanikiwa kukamata watuhumiwa 186 wa makosa mbalimbali ikiwemo wizi.

Akatumia nafasi hiyo kuwataka baadhi ya watu wachache wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja vitendo hivyo kwani Jeshi hilo halitowaonea muhali, kwa watakao bainika Kutenda uhalifu.

Masejo akasisitiza kuwa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka Jeshi hilo linawataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani ambapo Kwa madereva walevi au wanaojaribu na kutaka kuvunja sheria, watakamatwa na kuwafikisha mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoani humo akatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika jamii ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika Kutenda makosa husika.