Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa kumi wa mauaji ya Yumen Elias (54) aliekuwa mlinzi katika eneo la Mwananchi lililopo Kata ya Mahina Wilaya ya Nyamagana na mkazi wa Nyashishi aliyeuwawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Hayo yamebainishwa leo Januari 23, 2024 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa wakati akitoa taarifa ya mauaji hayo kwa waandishi wa habari.
Kamanda Mutafungwa amesema mauaji hayo yalitokea Januari 16,2024 majira ya saa tisa usiku na baada ya tukio hilo kuripotiwa kwa Jeshi la Polisi uchunguzi wa haraka ulianza kufanyika na ilipofika Januari 18 mwaka huu Jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti tofauti na maeneo tofauti.
“Watuhumiwa hao ni Julias Joseph (22) mkazi wa Igoma,Paul John (23) mkazi wa Mwananchi, Leonidas Juma Bukwimba (19) mkazi wa Buhongwa,Abdullah Hassan (31) mkazi wa Nundu, Edward Boniface (19) mkazi wa Mahina,Mussa Robert (22) fundi magari mkazi wa Ilemela Kanisani,Steven Emmanuel (18) mkazi wa Nyakato Sokoni, George Mang’era Koloso (50) mfanyabiashara mkazi wa Nyegezi,Hamis Omary (21) mfanyabiashara mkazi wa Mabatini pamoja na Charles Chacha (27) mkazi wa Mahina Kati”, amesema Kamanda Mutafungwa .
Ameeleza kuwa watuhumiwa hao wamehojiwa na uchunguzi unaendele kufanyika ili mashahidi waweze kupatikana kwaajili ya kukamilisha taratibu ili hatua za kisheria za kuwafikisha mahakamani zifanyike.
Aidha, Mutafungwa ametoa wito kwa makampuni binafsi ya ulinzi kuhakikisha wanaweka walinzi wakutosha kwaajili ya kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ya malindo sanjari na kuwapatia vitendea kazi vitakavyowasaidia kujihami pindi wanapovamiwa na wahalifu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutoa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa akionesha vifaa walivyovitumia watuhumiwa wa mauaji