Mapigano makali yameripotiwa kati ya vikosi vya Kikurdi na vikosi vinavyoungwa mkono na Uturuki kaskazini mwa Syria, ambapo zaidi ya watu 100 wameuawa ndani ya masaa 48 yaliyopita.
Taarifa iliyotolewa jana na Shirika la Haki za Binaadamu la Syria imesema waliouawa kwenye mapigano hayo ni wapiganaji 85 wanaoungwa mkono na Uturuki na 16 kutoka kundi la Syrian Democratic Forces (SDF), jeshi la Wakurdi wa Syria wanaoungwa mkono na Marekani.
Hali kwenye mji wa kaskazini mwa Syria, Manbij, imezidi kuwa mbaya baada ya wanajeshi wa Uturuki kuzidisha mashambulizi yao ya angani na ardhini. Pande hizo mbili zinawania udhibit wa Bwawa la Tishrin, ambalo ni muhimu kwa rasilimali za maji na umeme.
Bwawa lenyewe linaripotiwa kuwa limeanza kuharibiwa kutokana na mapigano hayo. Sehemu kubwa ya kaskazini mwa Syria iko mikononi mwa wapiganaji wa SDF, ambao waliongoza vita vilivyolishinda kundi lijiitalo Dola la Kiislamu mnamo mwaka 2019.