Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Jeshi la Polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kujifanya maofisa wa serikali na kutengeneza nyaraka za kughushi ili kusajili vijana wapate ajira idara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa baadhi ya walalamikaji walilipishwa fedha.
Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea huko Chalinze Wilaya ya Bagamoyo ambapo walikutwa na vifaa wanavyofanyia uhalifu.
“Walikutwa na walalamikaji wanne ambapo mmoja alikuwa tayari ametoa kiasi cha shilingi 500,000 huku walalamikaji watatu wakiwa wanafanyiwa usaili feki,”alisema Lutumo.
Alisema kuwa watuhumiwa walikutwa na vifaa vya kufanyia uhalifu huo ikiwa ni pamoja na nyaraka feki za namna ya kujiunga na idara hiyo, fomu feki ya malipo ya kujaza maombi, kompyuta na kompyuta mpakato.
Aidha aliwataka watumiaji wa vyombo vya moto kama magari, bajaji na pikipiki wanapaswa kukagua vyombo vyao kabla ya kuanza safari ili kuepusha ajali zinazoepukika na kufuata sheria za usalama barabarani pamoja na kujiepusha na utumiaji wa vileo.
Kwenye tukio lingine watu 32 wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na vitu mbalimbali vya wizi ambavyo walikamatwa navyo kufuatia operesheni iliyofanywa katika kipindi cha wiki moja.
Alitaja vitu vilivyokamatwa ni bajaji, pikipiki nne, jokofu, televisheni saba, redio nne, magodoro mawili na vitu mbalimbali huku wengine wakikutwa na pombe ya moshi lita 55, bangi puli 29 na kete 349 na bidhaa za vilevi zilizokwisha muda wake aina ya zed boxi 19 na samsoni boxi moja.