Kama kuna neno ambalo limewafanya watu wabaki palepale walipo miaka nenda – rudi ni neno: “Watu watanifikiriaje au watu watasemaje.”

Watu wengi wana ndoto kubwa, maono makubwa, mawazo makubwa ya kuibadili dunia na vipaji vingi, lakini wanafikiria watu wengine watawafikiriaje na watasemaje kwa wanachokifanya.

Hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa na kufikia hatua kubwa kwa kufikiria watu wengine watamfikiriaje au watasemaje kwa anachokifanya.

“Kama hakuna adui wa ndani, adui wa nje hawezi kutujeruhi,” ni methali ya Kiafrika. Watu wengi wamekuwa maadui wao wenyewe kwa kuzima ndoto zao wenyewe. Ukiwa mtu wa kwanza kujiaminisha kwamba watu watakuona wewe ni kichaa, kweli watu watakuona hivyo na huwezi kupiga hatua yoyote.

“Jinsi mtu anavyofikiri ndivyo alivyo,” alisema James Allen. Ulivyo sasa ni matokeo ya mambo yote ambayo umekuwa ukiyafikiri. Fikra zako ni za muhimu sana kabla ya fikra za watu wengine. Fikra zako na maono yako yakiwa makubwa huwezi kusumbuliwa na watu wenye fikra ndogo. Ukiwaza kufanya mambo makubwa huwezi kamwe kusumbuliwa na watu wanaowaza mambo madogo.

Acha kuogopa watu watakufikiriaje, acha kuwaza watu watasemaje, maana vinakuchelewesha. “Jambo la kuogopa ni kuogopa,” alisema Franklin Roosevelt, aliyekuwa Rais wa Marekani kuanzia mwaka 1933 hadi 1945. “Woga ni mojawapo ya maadui wakubwa wa mafanikio,” ameandika Reginald Mengi katika kitabu chake cha ‘I Can, I Must, I Will.’

Kuna watu wengi wamekufa wakiwa na vitu vikubwa ndani yao kwa sababu tu waliogopa kufanya vitu hivyo kutokana na kuwaza watu wengine watawafikiriaje. Ndiyo maana Myles Munroe aliwahi kusema: “Sehemu tajiri kuliko zote hapa duniani siyo kule Kuwait, Iraq au Saudi Arabia, wala siyo machimbo ya dhahabu na almasi yaliyoko nchini Afrika Kusini.

“Ingawa inaweza kushangaza, lakini sehemu tajiri kuliko zote hapa duniani ni umbali mchache kutoka nyumbani kwako. Sehemu hiyo ni makaburini. Huko zimezikwa ndoto ambazo hazijawahi kukamilishwa, nyimbo ambazo hazijawahi kuimbwa, vitabu ambavyo havijawahi kuandikwa, michoro ambayo haijawahi kuchorwa, mawazo ambayo hayajawahi kushirikishwa, uvumbuzi ambao haujawahi kufanyika, maono ambayo hayajawahi kufikiwa na kusudi ambazo hazijawahi kutimizwa. Makaburi yamejaa utajiri uliozikwa. Ni shida iliyoje.”

Ukiendelea kuogopa na kufikiri watu watasemaje au watu watakufikiriaje, kuna siku utakwenda kuutajirisha udongo badala ya kuitajirisha dunia.

Amka sasa, toka katika kitanda cha ‘watu watasemaje, watu watanifikiriaje’ na anza kufanya mambo ambayo umedhamiria kuyafanya. Anza biashara uliyopanga kuifanya.

Nunua kiwanja ulichopanga kununua ingawa sehemu hiyo inaonekana ni nje ya mji. Kuna siku patakuwa mjini. Zamani Tegeta yalikuwa ni mashamba ya mikorosho, Mbezi kote kulilimwa katani. Leo huko kote ni mjini.

Soma masomo uliyopanga kuyasoma, anza kuonyesha kipaji chako ambacho Mungu amekujalia. “Kubali majukumu ya maisha yako. Jua kwamba ni wewe atakayefika anakotaka kufika na si mtu mwingine,” anatuasa Les Brown.

Nguvu ambayo watu wanayo juu yako ni nguvu unayowapa wewe. Yesu pamoja na kuandamwa na waandishi na mafarisayo hakuwahi kukatishwa tamaa na maneno waliyoyasema juu yake.

“Ukisimama na kuanza kumrushia jiwe kila mbwa anayekubwekea njiani, utachelewa kufika unakokwenda,” alisema Ben Carson.

Hata watu wakisema jambo fulani haliwezekani, wewe sema ninaweza, wakisema biashara fulani aliifanya mtu fulani na kushindwa, waambie mimi siyo yeye.

Meli haizami kutokana na maji yaliyo nje, bali huzama kutokana na maji yanayoingia ndani yake. Usiruhusu hata siku moja watu wengine wakuamulie hatima yako.

Ili kuua hofu ya watu watafikiria nini au watasema nini, ni muhimu kuifahamu kanuni ya 20-40-60. Kanuni hiyo ilianzishwa na mwigizaji wa kike anayeitwa Shirley Maclaine aliyezaliwa mwaka 1934, huko Richmond, Marekani. Kanuni hiyo inasema:

“Ukiwa na miaka 20, muda mrefu huwa unahofu watu wengine wanakufikiriaje, ukifikia miaka 40, unashtuka na kusema, ‘sijali watu wengine wanasema nini kuhusu mimi’. Ukifika miaka 60, unagundua hakuna mtu yeyote anayekufikiria, kila mtu anafikiria mambo yake.” Sisi hatukufikirii wewe, “Watu watanifikiriaje, inakuchelewesha.”