Na Dotto Kwilasa ,JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi Ajira na Wenye ulemavu  Profesa.Joyce Ndalichako   amesema zaidi ya watu milioni 2.9 kwa mwaka  hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi hali inayochangia jamii kupoteza nguvu kazi.

Ameyasema hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani itakayofanyika Aprili  28 mwaka huu mkoani Morogoro na kueleza kuwa takwimu hizo ni za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa mwaka 2022 .

Prof.Ndalichako amefafanua kuwa kati ya watu hao  zaidi ya wafanyakazi milioni 402 huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu hadi hapo watakapopona.

Amebainisha kuwa kwa upande wa  Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249 ambapo katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217.

“Takwimu hizo ni kubwa sana zinaathiri utendaji kwa kuwa zinasababisha upotevu wa maisha ya Wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati wafanyakazi walioumia wakiendelea kupata matibabu,.

Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kwamba suala la ajali na  magonjwa yatokanayo na kazi linahitaji jitihada za makusudi katika kukabilia nalo,”amesema 

Amesema lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha na kuweka mazingira salama katika sehemu za kazi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Mazingira Salama na Afya kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi”.

”Serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvuKazi ya Taifa  inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi Nchini yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi,”amesema.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA Khadija Mwenda amesema katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi tarehe serikali kwa kushirikiana na wadau itaendesha kampeni maalum ya uhamasishaji .

Amesema uhamasishaji huo utakuwa kwa njia ya mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu.