Shirika la Madaktari wasio na mipaka la MSF limesema takriban watu 85 wamefariki katika hospitali moja kwenye mji wa El-Fasher huko Darfur tangu mapigano yalipozuka kati ya pande zinazozozana nchini Sudan Mei 10.
Mkuu wa mpango wa dharura wa shirika hilo Claire Nicolet, amesema siku ya Jumatatu pekee majeruhi tisa kati ya 60 waliopokewa katika hospitali ya kusini ya El-Fasher, walikufa kutokana na majeraha waliyoyapata.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, mapigano yamekuwa yakiendelea kati ya jeshi la serikali chini ya Abdel Fattah al-Burhan, na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo.
El-Fasher ni mji mkuu pekee katika mkoa wa Darfur, ambao hauko chini ya udhibiti wa RSF na ni kitovu cha misaada ya kiutu katika kanda hiyo iliyo kwenye ukingo wa njaa.