Watu 700 wamepata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika maonyesho ya kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika jijini Arusha.
Huduma hizo zilitolewa kwa muda wa siku saba katika viwanja vya TBA Kaloleni na wataalamu wanawake wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Arusha daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto na Mkuu wa Kitengo cha Utoaji wa Huduma Bora wa Taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani alisema upimaji huo ulikuwa maalumu kwaajili ya wanawake, wajawazito na watoto lakini pia waliwahudumia na wanaume waliohitaji kufanyiwa uchunguzi wa moyo.
Dkt. Naiz alisema wamefanya upimaji wa kipimo cha Echokardiografia ya moyo wa mtoto aliyepo tumboni kwa wajawazito 189 ambapo saba kati yao walionekana kuwa na shida ya moyo na wamewaandikia barua maalumu ya rufaa kwenda katika hospitali watakazojifungulia pia wamechukuwa taarifa zao na tarehe watakazo jifungua ili wawafuatilia na kujua maendeleo ya watoto hao ikiwa ni pamoja na kuanzishiwa matibabu mapema.
“Tumefanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa watoto 114 kati ya hao tisa tumewagundua kuwa na magonjwa ya moyo ya ambayo ni matundu, mishipa ya damu kutokukaa katika mpangilio wake na shida za valvu za moyo tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”.
“Ninatoa wito kwa wazazi kuwaleta watoto wao kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo pale zinapotokea nafasi za upimaji kama huu tulioufanya Arusha kwani magonjwa mengi ya moyo kwa watoto kama yatagundulika mapema watoto wanatibiwa na kupona kabisa”, alisema Dkt. Naiz.

Dkt. Naiz alisema watu wazima waliowapima walikuwa 397 wanaume wakiwa 99 kati ya hao 397 waliopewa rufaa ya kwenda kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupata matibabu ya kibingwa katika taasisi yao iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam walikuwa 19.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkuu wa Kitengo cha Vipimo vya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Engerasia Kifai alisema magonjwa ya moyo waliyokutwa nayo watu wazima yalikuwa ni shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa vyumba vya moyo, makovu kwenye valvu za moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, hitilafu kwenye mfumo wa umeme wa moyo na magonjwa ya kuzaliwa kama vile tundu kwenye moyo huyu alikuwa mgojwa mmoja.
Dkt. Kifai alivitaja visababishi vya magonjwa wa moyo kwa watu wazima kuwa ni uzito mkubwa, utumiaji wa vilevi kuzidi kiwango kinachotakiwa, utumiaji wa tumbaku, utumiaji wa chumvi zaidi ya kiwango kinachotakiwa, kuwa na kiwango kikubwa cha lehamu kwenye damu, kutokufanya mazoezi, kuwa na shinikizo la juu la damu, kuwa na ugonjwa wa kisukari, kuwepo na magonjwa ya moyo kwenye familia, kutokula mlo kamili, kupumzika muda kidogo au kutopata muda wa kutosha wa kupumzika na msongo wa mawazo
“Baadhi ya dalili za magojwa ya moyo kwa watu wazima ni kuumwa kwa kifua mara nyingi huambatana na uzito ama mgandamizo wa kifua, kupungukiwa na pumzi, kukohoa, kuchoka bila sababu, mapigo ya moyo kwenda haraka haraka au mapigo ya moyo kutokupiga kwa mpangilio au kuwa chini ya kiwango ikiambatana na kuchoka sana ama kudondoka na kupoteza fahamu na uvimba kwa miguu ambapo hubonyea ukiikandamiza”, alisema Dkt. Kifai.
Dkt. Kifai alisema ili kuepukana na magonjwa ya moyo ni muhimu kwa watu wakafuata mtindo bora wa maisha hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula chakula bora, kutotumia bidhaa aina ya tumbaku na kutokunywa pombe kupitiliza na kujenga tabia ya kupima afya japo mara moja kwa mwaka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakazi wa Arusha waliishuru Serikali kwa kuwapatia huduma hiyo bila ya malipo yoyote yale.
Lemaiya Laizer mkazi wa Loliondo ambaye mtoto wake alifanyiwa uchunguzi na kugundulikwa kuwa na tatizo la tundu kwenye moyo alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema kuwa imempunguzia safari ya kwenda KCMC kufanyiwa vipimo vya moyo na kupata matibabu.
“Mwanangu anashida akicheza kidogo anachoka pia ukuaji wake ni tofauti na watoto wengine, nikiwa Loliondo niliandikiwa rufaa ya kwenda KCMC baada ya kusikia kuna wataalamu wa moyo hapa nimemleta mwanangu ambaye amepima na kukutwa na shida na nimepewa rufaa ya kwenda Dar es salaam ili akapate matibabu ya kuzibwa tundu hilo”, alisema Laizer.
“Baada ya kusikia upimaji wa moyo unafanyika hapa kwa wanawake na watoto niliona nije kujaribu bahati yangu kwani mimi ni mwanaume na kuna wakati moyo wangu unakwenda kasi sana na ninashindwa kulala vizuri hasa usiku. Namshukuru Mungu nimefika hapa hawajanifukuza na nimepata huduma ya vipimo, ushauri na matibabu ya moyo na sijalipia chochote, alishukuru Mohamed Juma mkazi wa Sanawari.