Mexico
Bomba la mafuta nchini Mexico limelipuka na kuua watu zaidi ya 70 huku wengine 71 wakijeruhiwa vibaya baada ya watu wasiofahamika kutoboa bomba hilo kwa nia ya kuiba mafuta.
Katika mji wa Tlahuelilpan, Jimbo la Hidalgo, mwishoni mwa wiki ulikuwa katika kilio kikubwa kutokana na mlipuko huo.
Taarifa zinasema mamia ya watu walikuwa waking’angania kuchota mafuta kabla ya moto kuzuka ghafla siku ya Ijumaa. Watu watano wanaodhaniwa kuwa ndio waliotoboa bomba hilo, tayari wamefikishwa mahakamani.
Picha za televisheni zilionyesha moto mkubwa na watu walioungua vibaya kutokana na moto huo. Kundi la wezi wa mafuta linalofahamika kwa jina ‘Huachicoleo’ limezidi kupata wafuasi nchini hapa.
Miili ilikuwa imetapakaa katika eneo la tukio baada ya maofisa wa usalama kufanikiwa kuuzima moto huo.
“Miongo mwa waliofariki dunia ni mwanamke na mtoto wa miaka 12,” amesema Gavana wa Jimbo la Hidalgo, Omar Fayad.
Wananchi waliojawa majonzi wamefurika eneo la tukio huku maofisa wataalamu wa uchunguzi wa maiti wakiendelea kupiga picha maiti zilizotapakaa kila mahali.
Serikali imesema wizi wa mafuta umeligharimu taifa hilo karibu dola bilioni tatu mwaka jana.
Rais Andrés Manuel López Obrador, ambaye aliingia madarakani mwezi Desemba amezindua msako mkali dhidi ya wahalifu hao.
Shirika la Mafuta la Pemex, linalomilikiwa na serikali, limesema moto huo ulitokana na mabomba yaliyounganishwa kwa njia haramu.
Maelfu ya wanajeshi wamepelekwa katika maeneo tofauti kutoa ulinzi wa mabomba ya mafuta katika hatua ambayo imefanya usafiri kuwa mgumu maeneo hayo.
Waziri wa Usalama, Alfonso Durazo, amethibitisha kuwa moto huo ulizimwa Jumamosi asubuhi. Maofisa wa huduma za dharura walipelekwa hospitalini kwa kutumia helikopta.
Gavana wa Jimbo la Hidalgo, Omar Fayad, ameonya kuwa idadi ya waliofariki dunia huenda ikaongezeka huku shughuli ya kuwatafuta walioungua kutokana na mlipuko huo ikiendelea.
Shirika la Habari la AFP limeripoti kuwa wananchi walikwenda kuteka mafuta bila kuogopa athari zinazoweza kutokea.
“Watu wengi walifika katika bomba hilo na mitungi yao kujichotea mafuta kwa sababu mafuta yamekuwa haba sana nchini,” mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Martin Trejo, aliiambia AFP.
Martin, mwenye umri wa mika 55 alikuwa katika eneo la mkasa huo kumtafuta mwanawe aliyekuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakichota mafuta.
Baada ya mlipuko huo Gavana Fayad alitoa wito kupitia mtandao wake wa Twitter kuwahimiza watu kuepuka eneo hilo la mkasa.
Rais wa Mexico, López Obrador, amesema msako dhidi ya wezi wa mafuta umeimarishwa. “Nawaomba mjiepushe na wizi wa mafuta,” Fayad aliandika (kwa lugha ya Kihispania). “Kando na kuwa ni uvunjaji wa sheria unahatarisha maisha ya wale wanaohusika.
“Kile kilichofanyika leo Tlahuelilpan hakifai kushuhudiwa tena,” alisema. Rais López Obrador alifika eneo la tukio mapema Jumamosi.
Katika mahojiano na vyombo vya habari nchini humo, aliapa kubuni sera kali dhidi ya wezi wa mafuta hadi uhalifu huo utakapotokomezwa.
“Badala ya kukabiliana na mikasa, tutaimarisha sheria dhidi ya wizi wa mafuta,” amesema.
“Jambo la mmsingi kwa sasa nikuwahudumia wale waliojeruhiwa, kuokoa maisha, hilo ndilo jambo muhimu,” amesema.
Hii si mara ya kwanza mkasa wa moto katika bomba la mafuta kutokea Mexico.
Mwaka 2013 watu 37 walifariki dunia baada ya mlipuko kutokea katika makao makuu ya Shirika la Mafuta la Pemex mjini Mexico City.
Watu wengine 26 walikufa baada ya moto kuzuka katika kiwanda kingine cha mafuta mwaka 2012.