Zaidi ya watu 50 wameuawa karibu na mji wa kaskazini-mashariki mwa Mali wa Gao siku ya Ijumaa baada ya washambuliaji waliokuwa na silaha kuvizia msafara uliokuwa ukilindwa na jeshi lake, amesema afisa wa eneo hilo na wakaazi.

Shambulio hilo lilitokea karibu na kijiji cha Kobe, karibu kilomita 30 (maili 19) kutoka Gao katika eneo ambalo makundi ya Islamic State na Al Qaeda yamekuwa yakifanya shughuli zao kwa zaidi ya muongo mmoja, na kuikosesha utulivu Mali na majirani zake Burkina Faso na Niger.

“Watu waliruka kutoka kwenye magari ili kukimbia. Kulikuwa na raia wengi waliokufa na waliojeruhiwa,” afisa wa eneo hilo alisema siku ya Jumamosi, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na wasiwasi wa usalama.

Takribani miili 56 ilirikodiwa katika hospitali ya Gao, amesema afisa huyo, na kuongeza kuwa pia kulikuwa na idadi isiyojulikana ya wanajeshi majeruhi.

Jeshi la Mali halijasema chochote hadi sasa.

Mkazi wa Gao pia amesema karibu 50 waliuawa na magari kuchomwa. Mashambulizi mabaya yamekuwa ya mara kwa mara, na jeshi linalazimika kusindikiza magari ya raia karibu kila siku, amesema mkazi huyo.

Uasi huo ulianza katika eneo kame la kaskazini mwa Mali kufuatia uasi wa watu wa Tuareg waliotaka kujitenga mwaka 2012. Wanamgambo hao wa Kiislamu wameenea katika nchi nyingine katika eneo maskini la Sahel kusini mwa Sahara.

Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuchangia mgogoro wa kibinadamu ambapo zaidi ya watu milioni 3.2 wameyakimbia makazi yao kufikia Januari, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.