Watu 38 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine zaidi ya 100 kupotea baada ya Feri iliyokuwa imejaa watu kupinduka kwenye mto Busira Kaskazini – Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo.
Katika ajali hiyo ya Feri ambayo ilibeba watu waliokuwa wakirejea nyumbani kwa ajili ya Krismasi, watu 20 pekee ndiyo wamefanikiwa kuokolewa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meya wa Inende, Joseph Kangolingoli imesema kivuko hicho kilikuwa kikisafiri kama sehemu ya msafara wa meli nyingine na abiria walikuwa wafanyabiashara waliokuwa wakirejea nyumbani kwa ajili ya Krismasi.
Mara kadhaa Maafisa wa polisi wa Congo wamekuwa wakionya tabia ya kupakia abiria wengi kupita kiasi kwenye boti, ambapo wameapa kuwaadhibu wale wote wanaokiuka maagizo hayo.
Ajali za boti kuzama na kupinduka zimekuwa zikiongezeka nchini humo kutokana na kujaza abiria na wingi wa boti unaosababisha wengine kuacha njia yake.
Kwa mwezi Oktoba pekee, watu takriban 78 walikufa maji, baada ya boti iliyokuwa imejaa mizigo kuzama Mashariki mwa nchi hiyo.