MAHAKAMA ya Kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliwahukumu kifo watu 37, wakiwemo raia watatu wa Marekani, baada ya kuwatia hatiani kwenye mashitaka ya kushiriki katika jaribio la mapinduzi.

Akisoma hukumu hiyo siku ya juzi mjini Kinshasa, Jaji Meja Freddy Ehuma alisema watuhumiwa hao wanapewa “adhabu kali kabisa, adhabu ya kifo”.

Raia hao watatu wa Wamarekani, wakiwa wamevalia sare za buluu kwa manjano za jela na wakiwa wamekaa kwenye viti vya plastiki, walionekana wakiwa wameduwaa wakati mkalimani akiwaelezea hukumu yao iliyosomwa kwa lugha ya Kifaransa na Jaji Ehuma.

Mbali na raia hao wa Marekani, kulikuwapo pia raia mmoja wa Uingereza, mmoja wa Ubelgiji na mmoja wa Kanada.

Wote kwa pamoja wana siku tano za kukata rufaa kwa hukumu hiyo ambayo ilijumuisha mashitaka ya jaribio la mapinduzi, ugaidi na kujihusisha na uhalifu. Watuhumiwa 14 waliachiliwa huru kwenye kesi hiyo iliyoanza mwezi Juni.

Wakili wa raia hao sita wa kigeni, Richard Bondo, alipinga uwezekano wa hukumu ya kifo kuweza kutekelezwa kwa sasa nchini Kongo, licha ya kurejeshwa tena mapema mwaka huu na alisema wateja wake walikuwa na wakalimani wasiokuwa na uwezo wakati kesi hiyo ilipokuwa ikichunguzwa.

“Tutapinga uamuzi huu kwa kukata rufaa,” alisema Bondo.

Watu sita waliuawa wakati wa jaribio hilo la mapinduzi lililoongozwa na kiongozi wa upinzani asiyefahamika sana, Christian Malanga, mnamo mwezi Mei, ambaye aliyalenga makaazi ya Rais Felix Tshisekedi na mshirika wake wa karibu, Vital Kamerhe, ambaye kwa sasa ndiye spika wa bunge.

Jeshi la Kongo lilisema Malanga mwenyewe aliuawa kwenye makabiliano muda mfupi baada ya kutangaza mashambulizi yake moja kwa moja kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii.