Mvua zinazoendelea kunyesha nchini Niger zimesababisha vifo vya watu 339 na kuwaacha zaidi ya watu milioni 1.1 bila makaazi rasmi tangu mwezi Juni.
Waziri wa mambo ya ndani mwezi uliopita alifahamisha kuwa takriban watu 273 walipoteza maisha na wengine 700,000 waliathirika baada ya mvua kubwa kushuhudiwa katika taifa hilo la ukanda wa Sahel.
Shirika la habari la serikali ANP limeripoti jana kwamba kufikia Septemba 23, mafuriko yameathiri zaidi ya watu milioni 1.1 na kusababisha vifo vya watu 339 na wengine 383 kujeruhiwa.
Maeneo mbalimbali yaliathirika na mvua ukiwemo mji mkuu Niamey ambapo watu tisa walipoteza maisha. Mafuriko pia yalisababisha hasara kubwa ya vifaa, mifugo na chakula.
Kutokana na uharibifu wa shule na idadi kubwa ya watu kuhamishwa makwao, serikali imeahirisha kuanza kwa muhula mpya wa shule hadi mwishoni mwa mwezi Oktoba.